Rais Jakaya Kikwete, akiwa na mgeni wake Rais wa
Msumbiji, Filipe Nyusi, wakisalimia viongozi waliohudhuria kumpokea
mgeni huyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam jana.Rais wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi, amewasili
nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambayo pamoja na mambo mengine,
anatarajia kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini
Dodoma kesho. Aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam jana majira ya saa 6 mchana.
Baada ya kuwasili alipata burudani ya ngoma za asili kabla ya
kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na kupigiwa mizinga 21. Baada ya mapokezi hayo, Rais Nyusi alielekea Ikulu, ambako
alipokewa rasmi na mwenyeji wake, Rais Dk. Jakaya Kikwete, kabla ya
viongozi hao wawili kufanya mazungumzo ya faragha.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake iliyotangazwa juzi na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, leo Rais Nyusi atazungumza na
wafanyabiashara wa Msumbiji wanaoishi nchini na kisha kuendelea na ziara
yake Zanzibar, ambako atakutana na kuzungumza na Rais wa visiwa hivyo,
Dk. Ali Mohammed Shein.
Baadaye, Rais Nyusi ataelekea mjini Dodoma, ambako atakutana na
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete, makao makuu ya
chama hicho na baadaye ataelekea ukumbi wa Bunge kulihutubia Bunge kabla
ya kuhitimisha ziara yake na kurejea nchini kwake kesho.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment