
Mbunge wa Bahi (CCM), Omar Badwel,
amefanya ibada kubwa aliyoiita ya kumshukuru Mungu kutokana na kumsaidia
kushinda kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.Kesi hiyo ilikuwa ya madai ya kupokea rushwa ya Sh. milioni moja
kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkuranga.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimwachilia huru Badwel Mei 29, mwaka
huu ikieleza kuwa upande wa mashitaka yaliyofunguliwa na Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru) ulishindwa kuwasilisha
ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo na kumtia hatiani. Ibada hiyo
ilifanyika jana katika viwanja vya Bahi sokoni ilijumuisha madhehebu ya
dini ya Kiislamu kutoka Wilaya ya Bahi wakiongozwa na Shekhe wa Mkoa
wa Dodoma, Mustafa Rajabu pamoja na viongozi wengi wa dini hiyo.
Akizungumza katika ibada hiyo, Badwel alisema ameamua kufanya hivyo
kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa kumsaidia kwenye hali ngumu
aliyokabiliana nayo katika kesi hiyo. “Kama mnavyojua, hakuna jambo dogo katika kesi inayokukabili, hata
kama ni ya kusingiziwa lolote linaweza kutokea, unaweza ukahukumiwa
kifungo au ukawa huru, lakini mimi namshukuru Mungu niliachiwa huru,
hivyo ninamshukuru Allah,” alisema.
Aliwashukuru waumini wa dini zote kwa kumpa ushirikiano kwenye kazi
za maendeleo jimboni kwa kipindi cha miaka mitatu ya kesi yake
ilipokuwa ikiendeshwa. Badwel alisema kwa sasa atatumia muda mwingi
kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwa kuchapa kazi na kwamba hatakuwa
na muda wa malumbano ya kisiasa. Aidha, alisema baada ya ibada hiyo
itafuatiwa na nyingine Jumapili ijayo itakayofanyika katika kijiji cha
Mchito, wilayani hapa ikishirikisha madhehebu yote ya kikristo. Alisema
ibada hizo zinafanyika katika viwanja vya wazi ili kila muumini na
wananchi wengine wapate fursa ya kujumuika.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu alimshukuru Mbunge
huyo kwa kufanya tukio hilo aliloliita kubwa na kuwa ni wachache
wanaokumbuka kufanya hivyo. “Angeweza kuishia kusema kuwa nimeshinda kwa juhudi zake, lakini
yeye ameamua kuujulisha umma huu kuwa Mungu alimsaidia. Hata katika afya
ya akili na kimwili ingeweza kuyumba kama sio Mungu,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment