Pages

Tuesday, May 12, 2015

PROSEFA MARK MWANDOSYA: WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS

Profesa Mark Mwandosya 
Mwaka huohuo 1974 aliunganisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza akibobea katika uhandisi wa umeme na kuhitimu mwaka 1977.
Historia yake
Profesa Mark Mwandosya alizaliwa Desemba 28, 1949 mkoani Mbeya (atafikisha miaka 68 Desemba mwaka huu). Alianza elimu yake katika Shule ya Msingi Majengo iliyoko Mbeya Mjini (mwaka 1957 – 1958), kisha akahamia Shule ya Msingi Chunya iliyokuwa inamilikiwa na “White Fathers” mwaka 1959 – 1960. Aliendelea katika Shule ya Msingi Chunya “Middle School” kati ya mwaka 1961 – 1964.
Alipata elimu ya sekondari (kidato cha I – IV) katika Shule ya Malangali kabla ya kujiunga na kidato cha V na VI katika Shule ya Chuo Cha Ufundi, Dar es Salaam (DIT) mwaka 1969 – 1970.
Mwaka 1971, Profesa Mwandosya alikwenda Uingereza kusomea Shahada ya Sayansi katika Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Aston na kuhitimu kwa viwango vya juu mwaka 1974.
Mwaka huohuo 1974 aliunganisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza akibobea katika uhandisi wa umeme na kuhitimu mwaka 1977.
Miaka miwili ya kwanza wakati anasomea shahada ya uzamivu (1974 – 1976) alikuwa ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na alipomaliza “ubobezi” huo, alianza kufundisha chuo hicho akiwa mhadhiri kamili mwaka 1970 – 1980.
Walimu wa UDSM waliomfahamu Mwandosya tangu akianza kazi wamenijulisha kuwa alikuwa mtu wa kujibidiisha sana na ndiyo maana alipanda harakaharaka katika kazi zake kitaaluma. Mwaka 1980-1983 alikuwa Mhadhiri Mwandamizi kabla ya kuwa Profesa Mshiriki mwaka 1983 – 1987 na baadaye miaka iliyofuata akawa Profesa kamili.
Profesa Mwandosya alihamishiwa serikalini kuwa kamishna katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini mwaka 1985 – 1990, akapandishwa na kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo mwaka 1990 – 1992, akapelekwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuwa Katibu Mkuu mwaka 1992 – 1993 kabla ya kurudi kufundisha UDSM akiwa Profesa kamili mwaka 1994 – 2000. Ndani ya chama chake CCM, Profesa Mwandosya amepitia safari ndefu tangu akiwa Shule ya Sekondari Malangali.
Amekuwa kiongozi wa vijana wa Tanu miaka ya 1967, mwanachama mtiifu wa Tanu mwaka 1971-1977 na baadaye aliendelea kuwa mwanachama wa CCM. Kuanzia mwaka 2000, alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya yake na kuanzia mwaka 2002 ,aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Profesa Mwandosya amemuoa Lucy na wana watoto na familia imara.

Mbio za ubunge
Profesa Mwandosya alipoamua kuingia katika siasa za majukwaani katika ubunge, alikwenda jimboni kwake Rungwe Mashariki. Hii ilikuwa mwaka 2000. Alipokea kijiti kutoka kwa mbunge wa CCM aliyekuwa amemaliza muda wake na hakukutana na upinzani imara. Alishinda kwa kipindi cha mwaka 2000 – 2005 na wakati wote wa ubunge wake, alitumikia awamu ya pili ya urais wa Benjamin Mkapa akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.
Mwaka 2005 ulikuwa mwepesi zaidi kwa Profesa Mwandosya, CCM ilimpitisha kwa mara ya pili jimboni hapo na kufumba na kufumbua wapinzani “wakalala mbele”. Profesa Mwandosya akawa mbunge anayesubiri tu kuapishwa baada ya kupita bila kupingwa.
Wakati awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete unaanza, Profesa Mwandosya aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira),  2006-2008 na baadaye akawa Waziri wa Maji na Umwagiliaji 2008-2010.
Mwaka 2010, ulikuwa na matukio yaleyale ya 2005 katika jimbo la Rungwe Mashariki. Profesa Mwandosya alikosa mpinzani na akapita bila kupingwa na kuapishwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu.
(Vyama vya upinzani havikuweka wagombea). Aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) hadi hivi leo.
Profesa Mwandosya amekutwa na misukosuko kadhaa ya kiafya ikihusishwa na mazingira ya kuwekewa sumu na wapinzani wake wa kisiasa “mapambano ya uongozi ndani ya CCM” au kupigwa vita kutokana na misimamo yake ya kisiasa”.

Mbio za urais
Profesa Mwandosya alianza mbio za kusaka urais wa Tanzania mwaka 2005 alipochukua fomu na kuomba ridhaa hiyo kabla ya kushindwa katika hatua za upigaji kura na Kikwete ndiye aliyeshinda.
Hata hivyo, ameitumikia miaka 10 ya uongozi wa Kikwete katika utulivu mkubwa akionyesha busara za kiuongozi kila mara na wachambuzi wengi wanaichukulia hali hiyo kama maandalizi ya mara nyingine ya kuomba ridhaa ya uongozi wa nchi kupitia kwenye chama chake.
Tayari Profesa Mwandosya ameshaeleza kuwa hatagombea tena ubunge katika Jimbo la Rungwe Mashariki na kwamba ana mipango mingine. Mipango hiyo inachukuliwa kuwa ni kuingia tena katika mbio za urais.
Katika kuonyesha kwamba yuko makini na atashiriki katika safari ya urais mwaka huu, amewahi kukaririwa na gazeti moja la kila wiki akisisitiza kwamba “…kuteuliwa na chama kuwa mgombea urais ni heshima kubwa na ni kilele cha utumishi ambao mwanachama anaweza kutoa kwa chama na kwa Taifa. Itakuwa ni heshima iliyoje kwangu iwapo chama kitaweza kunifikiria na hatimaye kuniteua kufika hapo.”
Profesa Mwandosya hajatangaza rasmi kuwa atawania urais kupitia CCM, lakini maneno na vitendo vyake vinaonyesha kuwa anahitaji na atakuwa mmoja wa wagombea.
Pia, ni mmoja wa wanachama wa CCM ambao wanatajwa na kuonekana kama Watanzania ambao walau wanaweza kusimama na kuomba ridhaa hiyo.

Nguvu yake
Profesa Mwandosya ni mwanataaluma aliyebobea, tena katika elimu adhimu, uhandisi wa masuala ya umeme na ametumia taaluma yake kuandika mambo mengi yanayohusu nishati na hata maendeleo yatokanayo na nishati.
Amefanya tafiti mbalimbali na kuchapisha vitabu kadhaa ndani na nje ya nchi, kupitia taaluma yake, amezidi kuwa mweledi na anajua anachokisimamia. Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi anayehitaji kuongoza dola.
Walau kuwa na taaluma ya jambo fulani na ukaonekana umelisimamia na unalimudu.
Lakini kuna jambo la pili linalompa nguvu Profesa Mwandosya. Mzee huyu amefanya kazi Tanzania kwa muda mrefu kushinda wasomi wengine kama yeye wanaotafuta urais.
Tangu mwaka 1974 hadi sasa (miaka 40), amekuwa ama akifundisha UDSM, akiongoza wizara katika wadhifa wa katibu mkuu, akiwa mbunge na au waziri. Vyote hivyo amevifanya akiwa ndani ya nchi kwa hiyo amekuwa karibu na wananchi na anayajua matatizo yao.
Jambo la tatu ni utulivu na busara. Profesa Mwandosya si mtu wa kubeba mambo kwa pupa na kusimamia uamuzi wake huku ukiwa hauna tija. Ni mtu anayehitaji kila kitu kifanywe kwa utaratibu na kwa kuelewana.
Waziri mmoja alinijulisha kuwa, hata ndani ya Baraza la Mawaziri la Kikwete, yeye ni mtu ambaye hutumiwa katika kamati ndogo za mawaziri za kutatua mambo magumu yaliyowashinda vikaoni na kwamba busara zake zimetumiwa mara nyingi kuifanya Serikali ya Rais Kikwete iweze kuwa na utulivu.
Jambo la tatu ni kufahamika, jina la Profesa Mwandosya si geni kwa Watanzania. Limesikika sana. Katika kufanikiwa kuongoza nchi au kuvuka vinyang’anyiro vya ndani ya vyama, umaarufu wenye tija ni jambo la msingi. Watanzania wanamfahamu Profesa Mwandosya kama waziri wa muda mrefu na mtu anayejiheshimu. Hii ni silaha ya kawaida kwake.
Mwisho, yeye ni miongoni mwa maprofesa wanaoishi maisha ya kawaida sana. Baadhi ya wasomi wa ngazi ya u - profesa na tena wakifikia hizo za uwaziri na nyinginezo, huwa ni watu wa dharau, majivuno na kujisikia. Profesa Mwandosya si miongoni mwao, labda aina ya jamii aliyotoka ndiyo inayombeba na kumuondolea dharau na kiburi, lakini jamii ilimkuza na kumuachia tangu zamani, nadhani yeye mwenyewe si mpenda makuu.
Hataki kuishi maisha ya anasa, yasiyo na maana na ambayo haoni faida yake. Watu wengi wa karibu wanamuona kama Mtanzania wa kawaida. Hili ni jambo muhimu.

Udhaifu wake
Profesa Mwandosya ni mmoja wa wanasiasa wapole sana. Utulivu na upole uliopitiliza ni vitu viwili tofauti. Utulivu ni sifa kubwa ya kiongozi lakini upole uliopitiliza ni udhaifu mkubwa kwa kiongozi.
Mawaziri wengi waliofanya kazi na Profesa Mwandosya, wananiambia kuwa ni mpole sana na anapoona mambo yamemzidia huwa na tabia ya kukaa kimya.
Ni mtu wa namna hiyo. Ikiwa unataka kuwa Rais wa Tanzania, nchi ambayo imeporomoka kiutendaji ndani ya Serikali, hupaswi kuwa mpole kupita kiasi. Nimetafuta rekodi nzito za kiuongozi alizozisimamia Profesa Mwandosya na hadi sasa sijazipata. Kwamba tumkumbuke kwa lipi katika wizara alizopitia nimelikosa.
Hana rekodi nzito kwenye wizara alizopitia, amewahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati wa Mkapa, akawa Waziri wa Maji na Umwagiliaji wakati wa Kikwete na sasa akiwa ni Waziri akishughulikia Kazi Maalumu. Sielewi Watanzania watakaa wamkumbuke kwa mabadiliko yapi makubwa aliyoyasimamia katika utumishi wake wa juu serikalini.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Ikiwa CCM itahitaji mgombea mwenye uzoefu mkubwa ndani ya chama hicho na Serikali, basi Profesa Mwandosya ni mmoja wao. Miaka 40 ya utendaji ndani ya Serikali na ndani ya CCM kwa nyakati na vipindi tofauti, vinaweza kumfanya avuke kizingiti hiki.
Naweza kusema kuwa Profesa Mwandosya anaifahamu vizuri Serikali, nchi na hata wizara na idara zake kwa weledi mzuri na usio na shaka. Profesa Mwandosya hana makundi na hii ni tabia yake. Ninapozungumzia makundi simaanishi kamati ya kusaidia kwenye kampeni.
CCM kuna makundi na makundi hayo hufanya jambo lolote hata liwe chafu au hatari kwa watu wengine,  maisha yao na ustawi wao, wao hulifanya tu. Kamati ya kampeni yenyewe hufanya yale tu yaliyo ndani ya sheria na taratibu. Naambiwa Profesa Mwandosya anaamini anastahili kuupata urais kwa njia sahihi na za kidemokrasia kuliko hila, fitina na makundi. Jambo hili nalo ni silaha muhimu kwake.
Jambo la tatu linalombeba ni uadilifu. Huenda Profesa Mwandosya ni mwana CCM mwingine ambaye kwake ‘kupokea rushwa na kuiba au kutapanya mali na fedha za umma ni mwiko” (kama zilivyo zile ahadi za mwana Tanu). Tangu amekuwa waziri kwa miaka 15 sasa, katibu mkuu wa wizara kwa miaka kadhaa sasa, hakuwahi kuhisiwa, kutuhumiwa au kufikiriwa kuwa mmoja wa viongozi wala rushwa.
Lakini juhudi za waziwazi za vitendo na mapambano makubwa yakuzuia rushwa serikalini na katika maeneo aliyopata kuongoza havikuwahi kuonekana, ndiyo kusema kuwa yeye anachukia rushwa lakini hajaonyesha kama ana uwezo mkubwa wa kupambana nayo.

Nini kinaweza kumwangusha?
Sababu zilizomwangusha mwaka 2005 zinaweza kuwa kikwazo cha kwanza katika kuvuka mchujo ndani ya CCM mwaka huu. Ikumbukwe kuwa, mwaka 2005 Profesa Mwandosya aliangushwa na Kikwete. Inawezekana mbinu alizotumia kutafuta urais mwaka 2005 akaukosa, ndizo anazotumia kutafuta urais mwaka 2015 katika chama ambacho watu ambao hupita vikwazo na kuwa wagombea urais huhitaji mipango fulani kama aliyopitia Kikwete mwaka na hata ile ya kupigiwa debe na mtu mwenye nguvu kama Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995.
Ikiwa Profesa Mwandosya hajabadilisha mipango yake, yaleyale ya 2005 yatamwangusha mara nyingine kwa sababu chama ni kilekile na washindi wake hupita michujo kwa staili zilezile. Pia, Profesa Mwandosya anaweza kupimwa kutokana na utendaji wake katika wizara alizopitia.
Hii ni changamoto kubwa. Suala la utendaji katika Serikali nadhani litazingatiwa, nimeshaeleza kuwa kwa wana jamii hakuna rekodi nzito ya mambo ya kujivunia ambayo aliwahi kuyasimamia.
Hivi karibuni, ndiyo kwanza amekuwa waziri, kazi maalumu (kazi zake ni maalumu tu na wananchi hawazijui).
Ikiwa mgombea wa urais ajae atapimwa pia kwa kigezo cha utendaji wake alipokuwa waziri, Profesa Mwandosya anaweza kuonekana kama waziri wa kawaida mno na hili litaweza kumwangusha. Nguvu ya makundi yenye fedha ndani ya CCM ni kitisho chake cha tatu.
Kama nilivyoeleza Profesa Mwandosya ni mwadilifu sana na baadhi ya makundi ya kusaka uongozi ndani ya CCM yanawachukia watu waadilifu maana wanaweza kuharibu safari ya makundi hayo. Nathubutu kusema kuwa Profesa Mwandosya ni mmoja wa wana CCM ambao anaweza kuyatia woga makundi hayo na kama ndivyo basi anaweza kung’olewa kwenye safari hii kirahisi tu.

Asipopitishwa (Mpango B)
Kama ilivyo kwa maprofesa nguli kama yeye, moja ya mipango ya Profesa Mwandosya inaweza kuwa ni kurudi vyuoni kufundisha. Sekta ya nishati hususani umeme inahitaji mabadiliko makubwa Tanzania.
Profesa Mwandosya anaweza kuwa na mchango mkubwa kuendelea kuzalisha vijana wapya wengi huko, ikiwa hatagombea urais.
Lakini pili, kwa sababu ya busara, utulivu na upole wake, yeye ni mshauri mzuri. Nadhani anaweza kujihusisha na shughuli za kidiplomasia na utatuzi wa migogoro ndani na hata nje ya nchi. Tukumbuke kuwa hadi leo, bado wakulima na wafugaji wanauana, wafanyakazi wanagoma kila siku, watu wenye uwezo, ujuzi, maarifa na stadi kama Profesa Mwandosya wanaweza kabisa kutusaidia katika eneo hilo.

Hitimisho
Profesa Mwandosya amekuwa kiongozi ambaye ametimiza wajibu wake kwa kiasi kikubwa katika Taifa hili, pamoja na udhaifu wake, amekuwa na mchango mkubwa na anaheshimika mno.
Naamini pamoja na yote niliyoyaeleza juu yake, anaendelea kuwa mmoja wa watu wanaoonekana kuwa afadhali ndani ya CCM katika kurithi mikoba ya Rais Kikwete. Namtakia kila la heri katika kutimiza ndoto yake ya utumishi wa umma kwa vitendo.

CHANZO: MWANACHI

No comments:

Post a Comment