Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal akitoa heshima za mwisho mbele
ya jeneza lenye mwili wa marehemu John Nyerere, wakati wa kuaga mwili
huo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msasani, Dar es
Salaam jana.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil
Mramba amesema kupungua kwa umaskini kunakoelezwa na baadhi ya wataalamu
na wasomi ni suala la kitakwimu ambalo ni gumu kulithibitisha.
Aliyasema hayo jana, Msasani, Dar es Salaam muda
mfupi baada ya kuaga mwili wa John Nyerere. Mtoto huyo wa hayati Mwalimu
Julius Nyerere, alifariki dunia Mei 9, mwaka huu katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili na anasafirishwa leo kwenda Butiama kwa maziko.
Alisema ugumu wa maisha umeongezeka na akafafanua
kuwa licha ya taarifa zinazotolewa na wataalamu kwamba uchumi umekua ni
vyema kila mmoja akajitathmini kuanzia ngazi ya kaya kwani huko ndiko
hali halisi iliko. “Mimi katika kaya yangu bado hatujaendelea.
Maendeleo hayajafika kwa kiwango cha kumudu gharama zote kwa kila mmoja
wetu. Hatuhitaji kuambiwa juu ya maendeleo yetu kwa kutumia taarifa za
kisomi ambazo mara nyingi ni wastani. Angalia familia yako ikoje,”
alisema Mramba.
Kauli ya Mramba imekuja siku chache baada ya Benki
ya Dunia (WB) kuzindua ripoti yake juu ya maendeleo ya uchumi wa
Tanzania, mapema mwezi huu, ambayo inabainisha kuwa katika kipindi kati
ya 2007 mpaka 2012, umaskini umepungua kwa asilimia 70 jijini Dar hapa
huku ukishuka kwa asilimia 15 mikoani.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa katika kipindi hicho, umaskini unapungua kwa asilimia moja kila mwaka. Pia, alielezea kuporomoka kwa shilingi na kubainisha kuwa ni moja ya sababu zinazochangia ugumu wa maisha kwa Watanzania maskini na kueleza kuwa ni jambo linalotaka mikakati makini kukabiliana nalo.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa katika kipindi hicho, umaskini unapungua kwa asilimia moja kila mwaka. Pia, alielezea kuporomoka kwa shilingi na kubainisha kuwa ni moja ya sababu zinazochangia ugumu wa maisha kwa Watanzania maskini na kueleza kuwa ni jambo linalotaka mikakati makini kukabiliana nalo.
“Dola moja ya Marekani imewahi kuwa sawa na Sh7.
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa kinaweza kununua mbuzi wakati huo lakini
dola hiyo hivi sasa ni Sh2,000. Hebu niambie kiasi hicho kinanunua nini
wakati huu?” alihoji Mramba.
Wakati huo huo, familia ya Baba wa Taifa,
imelishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa msaada ilioutoa
katika kipindi chote cha kumuuguza hadi kufariki kwa ndugu yao. Shukrani hizo zilitolewa na mdogo wa marehemu,
Makongoro Nyerere alipokuwa akisoma wasifu wa marehemu mbele ya Makamu
wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na viongozi wengine waandamizi wa
Serikali.
Makongoro alimaliza kusoma wasifu huo kwa taabu
kwani alishikwa na majonzi kiasi cha kulia kwa kwikwi na kuwahuzunisha
mamia ya waombolezaji msibani hapo.
Aidha, Mbunge wa Monduli, Edward Lowasa ametuma
salamu za rambirambi za kumfariji Mama Maria Nyerere na familia ya Baba
wa Taifa. “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha John Nyerere,
mtoto wa mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere. Kifo chake
kimetonesha kidonda siyo kwa familia tu, bali kwa Watanzania wote,
kidonda cha kifo cha Mwalimu ambacho bado ni kibichi miaka 16 baada ya
kifo chake,” alisema Lowassa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment