 
  
            
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara 
uliofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es 
Salaam jana.
Mwenyekiti wa 
Chadema, Freeman Mbowe amesema matamanio ya Baba wa Taifa, Mwalimu 
Julius Nyerere ya kuwaletea Watanzania mabadiliko waliyoyakosa ndani ya 
CCM yanaenda kutimia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mbowe aliyasema hayo jana katika mkutano wa chama 
wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe 
jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine alizindua kitabu cha
 mambo aliyoyafanya mbunge wa jimbo hilo, Halima Mdee na wimbo maalumu 
wa msanii wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha.
Akizungumza katika mkutano huo uliorushwa moja kwa
 moja na ITV, Mbowe alisema katika maeneo yote ya nchi, watu wamekata 
tamaa ya maisha kutokana na uongozi mbaya wa chama tawala, hivyo wako 
tayari kufanya mabadiliko ya mfumo wa utawala.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu matamanio ya 
Mwalimu Nyerere yanaenda kutimia. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo 
wameyakosa ndani ya CCM. Nimezunguka nchi nzima na kubaini kuwa wananchi
 wanazo sababu na uwezo wa kuyaleta mabadiliko kutokana na kiu 
waliyonayo,” alisema.
Mbowe aliyeanza mkutano huo kwa kukagua gwaride la
 kikundi cha Red Brigade, alitoa kauli hiyo akimnukuu Mwalimu Nyerere 
aliyepata kusema kuwa, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata 
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia mchakato wa 
uandikishaji wapigakura kuwa unahitaji kutazamwa kwa namna nyingine ili 
kuwatendea haki wananchi ambao wana shauku ya kutimiza haki hiyon ya 
kikatiba.
“Juzi nilikuwa Mbeya, nimeshuhudia wananchi 
wakilala katika vituo vya kuandikishia kutokana na hofu waliyonayo 
kukosa uchaguzi mkuu. Namkumbusha Jaji Lubuva (Damian, mwenyekiti wa 
Tume ya uchaguzi) aongeze muda na isiwe siku saba kama ilivyopangwa 
awali. Kutofanya hivyo atakuwa anajitafutia lawama ambazo hakutakuwa na 
kiongozi yeyote wa CCM atakayesimama kumtetea pindi wananchi 
watakapokuwa wanamlaumu hapo baadaye,” alisema.
Mwenyekiti huyo mwenza wa umoja wa Katiba ya 
wananchi (Ukawa), pia alibainisha mkakati wa umoja huo kugomea na 
kuipinga rasimu inayotaka vyombo vyote vya habari kujiunga na Shirika la
 Habari Tanzania (TBC) kwa taarifa ya habari ya saa 2.00 usiku. “Tutaleta vurugu. Tutasimamisha Bunge kupinga 
sheria hiyo kwa sababu hiyo ni hujuma ambayo wananchi hawaikubali na 
mimi kama kiongozi wa upinzani nitalisimamia hilo,” alieleza.
Akimakaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge 
wa Ubungo, John Mnyika alisema mkutano huo ni muhimu na chama 
kimeuandaaa ili kuthamini umuhimu wa wanawake katika jamii. “Mwenyekiti fikiria kama wewe unabeba mimba miezi 
tisa, ujifungue na kumlea mtoto. Hayo ndiyo wanayoyafanya wanawake hawa.
 Ni lazima tukubali ujasiri wao kwa kuyajali majukumu yao,” alisema 
Mnyika.
Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Mabere 
Marando alisema Chadema kimejipanga kuwaleta viongozi wake wote jijini 
hapa kufanya kampeni ya uandikishaji katika daftari la kudumu ili 
wapigakura wafike milioni 3.5 na kuiondoa CCM madarakani.
Gwajima ahutubia
Bavicha watishia
“Nimepokea malalamiko kutoka kwa askari mstaafu wa Jeshi la 
Wananchi (JWTZ) ambaye analipwa Sh22,000 kwa mwezi. Anaamini Chadema 
itamtendea haki ili kipato chake kiweze kukidhi mahitaji,” alisema 
Marando. Mkutano huo pia ulizindua kikosi cha Red Brigade 
ambao wapo 200 katika kila jimbo nchini, wakiwa na jukumu la kulinda 
kura katika vituo vyote kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Gwajima ahutubia
Katika mkutano huo, Askofu Josephat Gwajima wa 
Kanisa la Ufufuo na Uzima, mwimbaji Flora Mbasha pamoja na mumewe 
Emmanuel Mbasha ni miongoni mwa wageni walioalikwa katika mkutano huo. Baada ya Mbowe kuhutubia, mashabiki walipiga kelele wakitaka Askofu Gwajima naye ahutubie.
Askofu huyo alipopewa nafasi alisema kiongozi 
anapokaribia kupoteza madaraka Mungu humpa ukichaa na kuacha kuona 
matatizo ya watu. “Kwa hali ilivyo sasa, viongozi wa Serikali 
wamepewa ukichaa, hawanaoni matatizo ya watu. Muda wa mabadiliko ndio 
umewadia, alisema.
Bavicha watishia
Awali, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) 
lilieleza dhamira ya kufanya maandamano kuishinikiza NEC kama 
haitaongeza muda wa kuandikisha wapigakura. Katibu Mkuu wa Bavicha Taifa, Julius Mwita 
alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa 
kata wa chama hicho katika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam.
Katibu mkuu wa mstaafu wa Bavicha, Deogratias Munishi aliwataka 
viongozi hao kujiamini katika kufanya maamuzi na kusisitiza kuwa kila 
kizazi kina utume wake, hivyo matazamio ya Watanzania yapo kwao.
“Wananchi wanataka kuona maisha yao yanakuwa bora 
kwa kupata elimu bora, afya pamoja na chakula cha uhakika. Hayo yote 
Chadema inaweza kuyafanikisha na ninyi ndiyo wahusika wa kuwasikiliza,” 
alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
 

No comments:
Post a Comment