Ni wazi kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo
yaliyopatikana kwenye tasnia ya filamu nchini bila kutaja Nyota
Academia, Kaole Sanaa Group, Kidedea, Kidedea Original, Mambo Hayo na
makundi mengine ya sanaa za maigizo.
Kimsingi makundi haya ndiyo yaliwaibua wasanii wakubwa nchini kama marehemu Steven Kanumba, Vicent Kigosi (Ray), Jacob Stephen (JB), Yvonne Cherry (Monalisa), Blandina Chagula (Johari), Jengua na wengine wengi ambao wanaendelea kuipeperusha vyema bendera ya filamu za Bongo ndani na nje ya Tanzania.
Makundi ya sanaa za maigizo bado yapo, tena siku
hizi yamekuwa mengi zaidi. Takriban makundi matatu hadi matano kwa kila
kata hasa jijini Dar es Salaam huku mengine yakiwa hayana hata usajili
kutoka Basata.
Hata hivyo, licha ya makundi haya kuwa mengi na
kuashiria kwamba Tanzania tuna vipaji vingi lakini bado naona utofauti
mkubwa wa ubora kati ya makundi ya sasa na yale zamani.
Haya ya siku hizi yameacha kutoa wasanii kama Kemi
wa Kaole, Tabia wa Kidedea (kwa sasa ni marehemu), Richie Richie wa
Nyota Academia na wengine wa mfano huo.
Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa siyo sekta ya
kuzalisha waigizaji bora bali ni sehemu ya kupotezea muda kwa wale
wasiokuwa na kazi. Mengi yamesheheni watu wanaopenda kujionyesha lukuki
kuliko kuwa na shauku ya kutimiza ndoto zao za kimaisha kupitia sanaa ya
maigizo.
Hali hiyo imesababisha wachache wenye nia ya dhati
ama kuvunjika au kuvunjwa moyo na wengi waliojiunga na makundi haya
wakidhani kwamba baada ya wiki mbili wataonekana kwenye runinga na kuwa
maarufu kama wasanii waliotangulia.
Makundi mengi ya siku hizi yamesheheni walimu
wasio na sifa wasioifahamu kwa kina sanaa pana ya maigizo. Wengi ni
wenzangu na mimi ambao wamejipachika taji la ualimu mara tu baada ya
kuigiza kwenye filamu mbili tatu ambazo hazijauza hata kopi mia moja.
Nao tayari wamejiona wamekwiva kuwafunza wengine
na matokeo yake ni kujazana ujinga kwa kusifiana wenyewe kwa wenyewe
kila wanapokutana kwenye mazoezi. Wanasahau kwamba sanaa ya uigizaji ni
kazi kama ilivyo uhasibu na ukandarasi. Sanaa hii imewahi kubadilisha
maisha ya baadhi ya watu duniani, kutoka walalahoi kuwa mabilionea hivyo
ni tasnia inayotakiwa kuheshimiwa tena siyo kidogo.
Makundi mengi ya siku hizi yamesheni michango kila
kukicha tena mingi ni ile iliyokosa kichwa wala mkia. Pia hiyo
inasababishwa na makundi haya kugubikwa viongozi wenye njaa, wasio na
kazi wala kibarua hivyo kuamua kuwageuza wasanii kuwa kitega uchumi.
Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa kichaka cha
wapenda ngono zembe. Ngono ya kuchanganyana wenyewe kwa wenyewe. Pia,
mara nyingi uchafu huo hufanywa na watu wenye vyeo ndani ya makundi
haya. Usishangae mwalimu, mwenyekiti au hata katibu wa kundi akawa na
uhusiano na wasichana zaidi ya watatu katika kundi hilo hilo moja.
Mchezo huu mchafu umekuwa moja ya magonjwa sugu
yanayosababisha kufa kwa makundi haya kwa sababu pindi wasichana husika
wanapogundua kuwa wanachanganywa huzua tafrani na kutoelewana na
husababisha kundi kuyumba na hata kuvunjika kabisa.
Makundi mengi ya siku hizi yametawaliwa na wasanii wasiokuwa na
uvumilivu, wengi hutaka mafanikio ya haraka. Hawataki shida wala tabu ya
kutangatanga ili kutafuata nafasi zaidi za kuonyesha uwezo ama kipawa
walichojaaliwa na Mungu.
Wamekaa wakisubiri fursa ziwafuate kwenye makundi
yao. Pengine walitakiwa kupata nafasi ya kukaa na watu ambao
wamefanikiwa kutoka na wawaeleze jinsi mlima wa kukubalika ulivyo mgumu
kuupanda. Mtu asiye mvumilivu ni lazima ataishia kati tu. Msanii ni
lazima ajitoe mwenyewe, kuhangaika huku na kule ili kutafuta chochoro ya
kuibukia kileleni kwani siku nzote hakuna ‘shortcut’ ya mafanikio.
Makundi mengi ya siku hizi siyo ya muda mrefu,
mengi huanzishwa na kudumu kwa miezi michache kabla ya wanakikundi
kusambaratishwa na sababu hizo nilizotangulia kuzisema.
Hata hivyo, bado nina matumaini na makundi ya
sanaa za maigizo, naamini kama wanavikundi wataamua kufanya kazi kweli,
basi wale wauza sura wataogopa hata kusogeza pua zao karibu na makundi
haya. Wasanii wa kweli pekee ndiyo watakaosalia na kazi itafanyika.
Wale walimu wasio na sifa nao watatafuta shule za
sanaa na kusoma ili watakoporudi kwenye makundi yetu wawe walimu wa
uhakika na watuivishe vilivyo.
Viongozi wanaojifanya viwembe kwa kuwachanganya
madada zetu nao watakoma na hata ile michango yao ya ovyoovyo itapungua
kama siyo kufa kabisa na tasnia yetu itasonga.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment