Social Icons

Pages

Monday, May 18, 2015

MAJENERALI WATANO WAKAMATWA BURUNDI


Maofisa wa ngazi za juu wa Burundi wamekamatwa kwa tuhuma za kupanga njama za kumpindua Rais Pierre Nkurunziza.
Wakati jaribio la kumng’oa mpiganaji huyo wa zamani wa msituni likiwa limeshindikana, wananchi wamerejea mitaani kuandamana ikiwa ni ishara ya kupinga mpango wake wa kugombeas urais kwa kipindi cha tatu kinyume na katiba.
Msemaji wa Rais, Gervais Abayeho alisema jana kwamba majenerali watatu wa jeshi na wawili wa polisi walikamatwa jana. Pia maofisa watatu wa ngazi za chini na askari wanane, walikamatwa. Jaribio la kumpindua kiongozi huyo lilifanywa wakati akiwa Tanzania kuhudhuria mkutano wa amani uliopanga kujadili machafuko ya Burundi yaliyotokana na wananchi kupinga mpango wa Nkuruzinza kutaka kugombea tena urais.

Watu warudi mitaani
Hali jijini Bujumbura ambayo ilitulia juzi, jana ilianza tena kuharibika baada ya zaidi ya waandamanaji 30 kuandamana kushinikiza rais huyo afute mpango wake wa kugombea tena urais. “Tutaendeleza maandamano kupinga mpango wa Rais kujiongezea muda wa kutawala. Unaona wanataka kutuzuia, lakini sisi tunasema hatutaacha kuandamana.
Tunataka katiba iheshimiwe,” alisema mmoja wa waandamanaji, Jean Paul Ndayiragije.
Viongozi wa upinzani na vyombo vyua habari vya binafsi, vina wasiwasi na serikali ya Nkurunziza hasa baada ya jaribio las mapinduzi kukwama. Tume ya Uchaguzi Burundi imesema itapitia upya taratibu za uchaguzi ambao Rais Nkurunziza alisema kuwa ataheshimu matokeo yoyote.

Waiombea vikwazo
Raia wa Burundi wanaoishi Uingereza wamemuomba Waziri Mkuu David Cameron kusimamisha misaada ya kifedha kutokana na msimamo wa Rais Nkurunziza kuwania urais muhula wa tatu.
Raia hao walisema uamuzi wa Nkurunziza ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo. Watu hao waliandamana jana jijini London wakipinga Rais Nkurunziza kukiuka katiba, makubaliano ya Arusha na mauaji ya raia 22 wa nchi hiyo yaliyosababishwa na maadamano ya wiki mbili zilizopita.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera ya nchi hiyo, huku wakitaka serikali kulinda amani na kumtaka Nkurunziza aache kugombea urais muhula wa tatu.

Barua kwa David Cameron
Waandamanaji hao waliwasilisha barua Ikulu ya Uingereza iliyoko Mtaa wa 10 Downing wakitaka nchi yao kuwekewa vikwazo. Kwa mujibu wa Muungano wa Ulaya (EU), Burundi imekuwa ikipewa msaada wa Dola 6 hadi 9milioni za Marekani kwa ajili ya kusaidia shughuli za Uchaguzi Mkuu.
Kutokana na vurugu zinazoendelea nchini humo, waandamanaji jijini London walisema ushiriki wa Uingereza katika uchaguzi huo kwa namna moja au nyingine ni kinyume cha sheria za uchaguzi.
Mmoja wa waandamanaji hao nchini Uingereza alisema: “Kama Uingereza imekuwa ikizungumzia demokrasia na utawala bora, tunawaomba watende haki. Uingereza wanapaswa kuchukua uamuzi mgumu.
“Hakuna haja kwa Uingereza kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia uchaguzi Juni 26, mwaka huu katika nchi ambayo haina utawala bora. Asilimia 50 ya bajeti ya nchi hiyo inategemea nchi za Magharibi hivyo hakuna haja ya kuisaidia Burundi.

Mwanaharakati alonga
Mwanaharakati wa vuguvugu la maandamano ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha UPD –Zigamibanga cha Burundi, Mugwengezo Chauvineau ametaja sababu za maandamano nchini humo kuwa ni Rais Nkurunzinza kushindwa kuweka uwiano baina ya Warundi sambamba na kutekeleza haki za binadamu.
Alisema waandamanaji wamekuwa kiungo, njia, nguzo na sababu ya rais aliyepo madarakani kutaka kupinduliwa.
Akizungumza katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Chauvineau alisema kwa mtazamo wa wananchi wa Burundi kitendo cha Rais Nkurunzinza kuendelea kukaa madarakani, kimewafanya wengi wawe tayari hata kunywa sumu, ili kutoweka kinyume na kuishi katika utawala butu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: