Social Icons

Pages

Tuesday, May 12, 2015

KUCHANGANYA LUGHA

Waandishi na wazungumzaji  wengi hawako makini na hawajali kuzingatia ufasaha wa Kiswahili. Nilieleza kidogo katika makala zangu zilizopita kwamba watangazaji hasa wa redio na runinga zilizosajiliwa katika miaka ya hivi karibuni ndio wasiotilia mkazo matumizi fasaha ya Kiswahili.
Swali la kujiuliza ni kwa nini Watanzania wengi hasa wasomi hawathamini Kiswahili kama inavyostahili? Swali hili ni vigumu kulijibu lakini kwa kusoma makala haya labda utapata jibu.
Nimewahi kuandika kuwa kuchanganya Kiswahili na Kiingereza katika kuandika habari makala au katika mzungumzo rasmi ni kukidhalilisha Kiswahili. Waandishi na wazungumzaji  wengi hawako makini na hawajali kuzingatia ufasaha wa Kiswahili. Nilieleza kidogo katika makala zangu zilizopita kwamba watangazaji hasa wa redio na runinga zilizosajiliwa katika miaka ya hivi karibuni ndio wasiotilia mkazo matumizi fasaha ya Kiswahili. Hii innatokana na vyuo vya uandishi wa habari kutotilia mkazo mafunzo ya lugha kwa wafanyakazi wao ili kuwainua kitaaluma zao. Viongozi wa vyombo vya habari wanatakiwa kuwaandalia semina na warsha za kuboresha taaluma yao katika fani za uandishi na utangazaji.
Nitatoa mifano michache ya makosa yanayofanywa na watangazaji wa runinga na redio. Kwa mfano utawasikia watangazaji wakisema:
  1. Message unazopeleka ni za nani ?
  2. I remember kwenye semina ya ndoa mambo yalikuwa safi.
  3. Lakini a good office is well arranged
  4. Hiyo intrastructure ni mbovu.
  5. Lazima ufokasi kwenye future na maelezo mengine mengi.
Mifano hii michache inaonyesha jinsi tunavyoidhalilisha lugha yetu. Hivi kweli mzungumzaji alishindwa kupata visawe vya maneno kama ‘message, remember, infrastructure, a good office’ nk.? Kama ikishindikana angeweza kuwauliza  wenzake  wamsaidie na pengine angeweza kutumia kamusi. Polepole anajiongezeaauwezo wa kitaaluma ambao ni hazina kubwa kwake. Mazoea ya kujielimisha ama kwa kusoma au kuwatumia wenye ujuzi zaidi ni njia mojawapo ya kujijenga kwa kuongeza maarifa.
Pamoja na hayo liko kundi jingine ambalo lina sauti kubwa katika jamii. Kundi hili ni la wanasiasa na hasa wabunge ambao wanaokuwa wakijadili hoja zao wanapokuwa bungeni au wanapowahutubia wananchi. Wanasiasa hawa nao wanavunja maadili ya lugha kwa kuchanganya Kiingereza na Kiswahili katika mazungumzo yao. Watambue kuwa wanasikika kwa jamii nzima ya Watanzania na pia nje ya nchi kwani watu huwa macho kufuatilia kinachozungumzwa bungeni  au kwenye mikutano. Baadhi ya wanasiasa wanapozungumza hawako makini katika kuchagua misamiati au istilahi za kutumia. Kwa kuwa muda wa kuzungumza ni mfupi, wanachokabiliana na tatizo la uhaba wa maneno na hivyo uchaguzi wa maneno wanayotumia unawatatiza. Inashangaza kuona kuwa ile kanuni kwa wabunge kuwa wawapo bungeni wana uhuru wa  kutumia Kiswahili au Kiingereza. Kwa hiyo  matumizi ya lugha hizi mbili kwa ufasaha umekubalika bungeni. Hivyo uteuzi wa lugha moja ni wa hiyari ila  kuchanganya lugha hizi mbili katika kufafanua jambo ni makosa. Ninavyofahamu ni kuwa kama mbunge akiamua kutumia Kiswahili basi aendelee kukitumia moja kwa moja. Kama anataka kutumia Kiingereza basi atumie Kiingereza moja kwa moja. Ila kuchanganya lugha hizi mbili kwa pwakati mmoja katika majadiliano ni kuwakosea haki baadhi ya wasikilizaji.
Swali la kujiuliza ni kwa nini wanasiasa, wanataaluma na watangazaji siku hizi hawana umakini  katika matumizi ya lugha fasaha na sanifu wanapoelezea jambo kwa Watanzania na dunia kwa jumla? Ijapokuwa sijafanya utafiti wa kina lakini kwa uzoefu wangu wa miaka mingi katika fani hii ya matumizi ya Kiswahili katika shule na vyuo, nimegundua kuwa vijana wengi wanataka kujifanya  kuwa wao ni wasomi hata kama wamefikia kidato cha nne au sita. Ukweli ni kuwa kama una elimu ya sekondari na hata ya chuo kikuu bado huna haki ya kujigamba kuwa wewe ni msomi. Inashauriwa kuwa kujielimisha ni wajibu wetu sote kwani hatuko wakamilifu. Sifa mojawapo ya kuwa msomi ni kuzungumza lugha rahisi na inayoeleweka kwa jamii nzima ya wasikilizaji wako.
Nimewasema watangazaji katika vyombo vyetu vya habari pamoja na wanasiasa lakini ingekuwa bora zaidi na kwa ajili ya manufaa ya umma kama serikali ingekuwa na sera ya lugha inayotakiwa kufuatiliwa kwa makini. Nafahamu kuwa serikali imeunda Baraza la Kiswahili la Taifa kama  chombo cha kusimamia na kuratibu Kiswahili Tanzania tangu mwaka 1967 lakini hakina meno. Ili sheria ya kuliunda Baraza la Kiswahili la Taifa liwe na meno, inatakiwa ifanyiwe marekebisho ya kuliwezesha kuchukua hatua  za kisheria endapo asasi, taasisi, idara, kampuni au mtu binafsi atafanya makosa ambayo itajulikana ni ya kizembe, achukuliwe hatua. Hii ina maana kuwa na sheria iwafanye viongozi, waandishi na watangazaji kuwajibishwa kama vile kupewa maonyo, kufungiwa kwa muda au kufutiwa liseni zao moja kwa moja endapo watakiuka kanuni zilizowekwa.
Nimewasema wanasiasa, waandishi na watangazaji pamoja na serikali kila moja kutimiza wajibu wake. Hata hivyo, ieleweke kuwa hayupo mtu au chombo cha kunyooshewa kidole. Wote tuna wajibu wa kuona kuwa tunaithamini lugha yetu na huo ndiyo uzalendo tunaoupigania.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: