Pages

Thursday, May 14, 2015

KESI YA GUNINITA, MSINDAI DHIDI YA MAKONDA KUPANGIWA HAKIMU MEI 21

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa sasa, Paulo Makonda.
Jalada la kesi  ya madai ya Sh. milioni 100 iliyofunguliwa na waliokuwa Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mkoa Dar es Salaam, John Guninita, dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa sasa, Paulo Makonda, linasubiri kupangiwa hakimu kwa ajili ya kusikilizwa usuluhishi Mei 21, mwaka huu.Hatua hiyo ilifikiwa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa kwamba jalada la kesi hiyo litahamishiwa kwa hakimu mwingine kwa ajili ya kusikiliza usuluhishi kati ya pande hizo mbili. Katika kesi ya msingi, Msindai na Guninita, wanaiomba mahakama hiyo kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh. milioni 100.
Msindai na Guninita wanadai kiasi hicho cha fedha kwa madai ya Makonda wakati akiwa Katibu wa Uhamasishaji Chipukizi CCM, kutoa maneno ya kuwadhalilisha katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Benjamin Mwakagamba, wanaiomba mahakama imwamuru pamoja na mambo mengine, itoe zuio la kudumu kwa Makonda  kutozungumza tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Pia wanaomba Makonda kulipa riba pamoja na gharama za kesi na malipo mengine ambayo mahakama itaona yanafaa. Makonda anadaiwa kuwa akiwa Katibu wa Uhamasishaji Chipukizi wa CCM, katika mkutano wake, alitoa maneno akidai kuwa Msindai na Guninita ni vibaraka wanaotumiwa kuiharibu CCM kwa nguvu ya fedha.
Aidha, Msindai na Guninita wanadai kuwa maneno hayo yaliyotolewa na Makonda  yamewadhalilisha na kufanya waonekane ni viongozi ambao hawafai kuongoza CCM. Wameongeza kudai kuwa maneno hayo ya Makonda yamewadhalilisha mbele ya jamii na CCM kwa ujumla.
Katika hati hiyo ya madai inaonyesha kuwa Makonda alipelekewa barua ya madai ambayo ilimtaka kuomba msamaha. Hata hivyo, katika majibu yake, Makonda alisema hataomba msamaha kwa kuwa aliyatamka kwa nafasi yake kichama na kwa mujibu wa katiba, muongozo na kanuni za Chama.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment