
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa sasa, Paulo Makonda.
Jalada la kesi ya madai ya Sh. milioni 100
iliyofunguliwa na waliokuwa Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa
wa Singida, Mgana Msindai na Mkoa Dar es Salaam, John Guninita, dhidi ya
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa sasa, Paulo Makonda,
linasubiri kupangiwa hakimu kwa ajili ya kusikilizwa usuluhishi Mei 21,
mwaka huu.Hatua hiyo ilifikiwa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa kwamba
jalada la kesi hiyo litahamishiwa kwa hakimu mwingine kwa ajili ya
kusikiliza usuluhishi kati ya pande hizo mbili. Katika kesi ya msingi, Msindai na Guninita, wanaiomba mahakama hiyo
kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh. milioni
100.
Msindai na Guninita wanadai kiasi hicho cha fedha kwa madai ya
Makonda wakati akiwa Katibu wa Uhamasishaji Chipukizi CCM, kutoa maneno
ya kuwadhalilisha katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Benjamin Mwakagamba,
wanaiomba mahakama imwamuru pamoja na mambo mengine, itoe zuio la kudumu
kwa Makonda kutozungumza tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama
alivyofanya awali.
Pia wanaomba Makonda kulipa riba pamoja na gharama za kesi na malipo mengine ambayo mahakama itaona yanafaa. Makonda anadaiwa kuwa akiwa Katibu wa Uhamasishaji Chipukizi wa
CCM, katika mkutano wake, alitoa maneno akidai kuwa Msindai na Guninita
ni vibaraka wanaotumiwa kuiharibu CCM kwa nguvu ya fedha.
Aidha, Msindai na Guninita wanadai kuwa maneno hayo yaliyotolewa na
Makonda yamewadhalilisha na kufanya waonekane ni viongozi ambao
hawafai kuongoza CCM. Wameongeza kudai kuwa maneno hayo ya Makonda yamewadhalilisha mbele ya jamii na CCM kwa ujumla.
Katika hati hiyo ya madai inaonyesha kuwa Makonda alipelekewa barua ya madai ambayo ilimtaka kuomba msamaha. Hata hivyo, katika majibu yake, Makonda alisema hataomba msamaha kwa
kuwa aliyatamka kwa nafasi yake kichama na kwa mujibu wa katiba,
muongozo na kanuni za Chama.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment