
Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya
Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu
na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma
kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya
Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 -
1978.
Historia yake
Historia yake
John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29
Oktoba 1959 huko wilayani Chato Mkoani Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya
ya mkoa mpya wa Geita) na atatimiza miaka 56 Oktoba mwaka huu.
Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya
Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu
na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma
kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya
Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 -
1978.
Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani
Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981.
Halafu alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya
Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa
mwaka 1981 – 1982.
Alipopata stashahada yake, moja kwa moja alikwenda
kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha
masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na
1983.
Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983),
kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na
akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na
Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha
Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza
masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford
nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako
alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa
maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo
aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa
shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke, watoto na familia imara.
Mbio za ubunge
Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995,
alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua
kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na
unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli
aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri
wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa
Mkapa kilipokamilika.
Mwaka 2005 aliendelea kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge
kwa kipindi cha tatu. Akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila
kupingwa. Lakini safari hii, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuongoza
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008
alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka
2010.
Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa
ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii hakupita bila
kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus
Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia
66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema. Na baada ya
kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete alimrudisha katika
Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Mbio za urais
Dk Magufuli ni mmoja wa wana CCM ambao wamekuwa
wakitajwa sana kuwa anaweza kuwa mgombea sahihi wa CCM baada ya kipindi
cha Rais Kikwete kumalizika. Lakini yeye mwenyewe amekuwa akikana na
kutotaka kuhusishwa na kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, watu wa karibu
na Dk Magufuli wanasema kuwa ameshafuatwa na vigogo wakubwa ndani ya CCM
wakimwomba, wakati ukifika, achukue fomu. Yeye amekuwa na msimamo kuwa
anapaswa kupima hali ya mambo kabla hajaamua kujihusisha na urais au la.
Nguvu zake
Nguvu ya kwanza ya Magufuli iko katika uwezo wake
wa kielimu. Inawezekana kuwa elimu si kila kitu katika siasa, lakini
ukweli unabakia kuwa mwanasiasa mwenye elimu ya kutosha akiwa na sifa
nyingine za kushika wadhifa fulani, ana nafasi kubwa sana ya kufikiriwa
kuliko yule ambaye hana elimu. Katika hili Magufuli amejizatiti na
amebobea sana. Elimu ukiichanganya na ujana vinamfanya awe mgombea wa
umri ambao ni karata muhimu ndani ya CCM.
Lakini jambo lingine linalompa nguvu, ni kukaa kwa
muda mrefu katika wizara zake. Amekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu kwa
miaka mitano na pia Waziri wa Miundombinu wakati wa Mkapa; akaongoza
wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa miaka mitatu kabla ya
kuongoza ile ya Uvuvi na Mifugo kwa miaka miwili. Lakini pia tangu
mwaka 2010 hadi hivi leo ameiongoza Wizara ya Miundombinu bila
kuhamishwa. Jambo hili hulikuti kwa mawaziri wengi sana, hasa katika
serikali ya Kikwete.
Jambo la tatu linalompa nguvu ni umakini na na
uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka. Watu wanaofanya kazi na Dk
Magufuli, kote alikopita wanasema kuwa, tofauti na mawaziri wengi
waliowazoea ambao huhitaji kuchambuliwa taarifa hadi zirahisishwe, kwake
ni tofauti. Yeye husoma kila jambo na kwamba anatumia muda mwingi sana
kusoma kila taarifa na hadi anaweka mistari na michoro kwenye taarifa.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na
Magufuli anasema kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Magufuli
taarifa ndefu lakini yenye uongo kwenye aya moja. Anasema kuwa aya hiyo
ilikuwa iko ukurasa wa 20 lakini ndani ya muda mfupi “Magufuli
aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi”. Utendaji huu wa kufuatilia
hadi vilivyomo kwenye maandishi ndani kabisa, umewashinda wanasiasa na
viongozi wengi, Magufuli anabebwa na jambo hilo.
Udhaifu wake
Moja ya udhaifu mkubwa wa Dk Magufuli ni tabia ya
“kufanya maamuzi haraka”. Baadhi ya watendaji wa wizara yake wanasema
kuwa anafanya maamuzi haraka mno na kuna wakati inaonekana maamuzi yake
hayana tija, au ni ya kung’ang’ania tu kwa sababu za kimsimamo. Kuna
mambo kadhaa ambayo yamekuwa na madhara makubwa katika wizara
alizoziongoza:
Kwa mfano, uamuzi alioufanya wa kukamata meli iliyotuhumiwa
kufanya uvuvi haramu na kukiuka sharia, haukuwa na tija kwa taifa kwani
baada ya kesi ile kwisha, serikali iliamriwa kulipa kiasi cha shilingi
za Kitanzania bilioni 2.8 pamoja na kurudisha meli husika kwani mahakama
ilijiridhisha kuwa ilikuwa inafanya shughuli zake kihalali.
Lakini pia amewahi kufanya mazoezi ya “bomoa
bomoa” kwa haraka mno tena kuna wakati bila kuzingatia haki za binadamu
za wanaovunjiwa nyumba na makazi yao. Hii, ndiyo sababu Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, tena akiwa katika ziara ya Wilaya ya Chato alimtaka
kutumia nguvu hizo kutumikia wananchi. Baadaye Rais Kikwete alifafanua
watu wanaostahili kubomolewa nyumba kuwa ni wale waliofuata barabara na
siyo wale wa asili na ambao barabara imewafuata. Kwa hiyo, wale ambao
wamefuatwa na barabara wanastahili kulipwa fidia.
Kosa jingine kubwa linalompa Magufuli udhaifu
usiomithilika, ni uamuzi na ushiriki wake katika mpango haramu wa uuzaji
wa nyumba za serikali ambao ulilalamikiwa sana wakati akiwa Waziri wa
Nyumba. Katika nchi ambayo wafanyakazi hawana nyumba na serikali
inahitaji sana viwanja katika maeneo maalum, haikutarajiwa uamuzi wa
namna ile ungekuwa na tija. Uamuzi ule uliisababishia serikali hasara
kubwa na uliacha manung’uniko mengi maana hata wasio wafanyakazi wa
serikali, nao walinufaika na nyumba zile.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Suala la kwanza linaloweza kumvusha Dk Magufuli
kwenye chekecheo la wagombea ndani ya CCM ni uchapakazi na nidhamu
kazini. Magufuli ni mchapakazi na mimi binafsi namwona kama waziri
mchapakazi kuliko mawaziri wote ambao wamebahatika kufanya kazi kwenye
serikali ya Kikwete. Ikiwa CCM inahitaji Rais ambaye atakuwa na uwezo
mkubwa wa kutenda na kusimamia kazi, basi Magufuli ndiye anaweza kabisa
kuchukua nafasi.
Jambo jingine linaloweza kumvusha Magufuli ni
msimamo. Yeye ni kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka. Hajui kuuma
maneno lakini anajua nini anachokisimamia. Watendaji wa Wizara ya
Miundombinu wanasema ni vigumu kumyumbisha Magufuli katika jambo ambalo
anaona hilo ndiyo njia, lazima mlitekeleze kwanza. Tabia ya namna hiyo
alikuwa nayo Mwalimu Julius Nyerere, kwamba akishaamua jambo fulani na
kama anajua njia yake, humtoi relini.
Alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi alithubutu hata kumtaja Naibu wake kwamba anahodhi viwanja. Mwaka
2013, aliwashangaza watu wakati alipopishana hadharani na Waziri Mkuu
Pinda, kuhusu suala la magari ya mizigo kupita katika barabara yakiwa
yamezidisha uzito.
Baada ya Pinda kuruhusu, Magufuli aliweka msimamo
kuwa jambo hilo halikubaliki na halitekelezeki na akalipiga marufuku.
Baadhi ya watu walichukulia msimamo wa Magufuli kama dharau kwa Waziri
Mkuu wake lakini wanaomfahamu wanasema angekuwa tayari kufa na msimamo
wake. Ikiwa CCM wanahitaji mgombea urais mwenye sifa ya msimamo thabiti,
namwona Magufuli akiwa mbele kabisa.
Jambo la tatu ni kutokuwa na makundi. Kati ya
mambo ambayo yanaiumiza CCM hivi sasa ni ikiwa itajikuta imepitisha
mgombea mwenye makundi na anayeweza kuleta migawanyiko. Chama hicho
kinahofia kuwa mtu wa namna hiyo atakosa uungwaji mkono wa makundi
yanayosigana na hivyo anaweza kuangushwa kwenye uchaguzi kutokana na
vita ya ndani ya chama.
Pamoja na Magufuli kuwa waziri muhimu sana kwenye
serikali ya Kikwete, angeweza kuwa mtu wa maana kwenye makundi ya kusaka
urais lakini amejiweka pembeni sana. Kwa sababu ya kusimama katikati,
anaweza kabisa kuwa mmoja wa watu watakaoonekana wanastahili kupewa
nafasi ili kutuliza nguvu ya makundi. Kuna wakati Samuel Sitta alidai
kwamba wakati ukifika atashirikiana na marafiki zake Bernard Membe,
Harrison Mwakyembe pamoja na Magufuli kumchagua anayefaa kuwania urais,
lakini Magufuli alikana na kujiweka kando na kundi hilo.
Kingine kinachoweza kumpitisha ni kufahamika na
kuuzika. Bila shaka CCM inahitaji mgombea anayeuzika na kufahamika ili
kupunguza mishale ambayo itakuwa inapigwa na UKAWA dhidi ya taswira
‘mbaya” ya chama hicho. Ili kujitoa katika hatari hiyo nadhani Magufuli
anaweza kuvushwa.
Asipopitishwa (mpango B)
Hitimisho
Na mwisho, Magufuli anaweza kuvuka mchujo kwa sababu ya taswira
yake kwa Rais Kikwete. Kama tunavyofahamu, rais anayeondoka anakuwa na
mchango mkubwa katika kusababisha uteuzi wa rais ajaye na tayari kuna
viashiria vingi mno vinavyoonesha kuwa Kikwete huenda anamchukulia
Magufuli kati ya wana CCM wachache anaowaamini.
Kikwete amewahi kuhutubia mkutano mmoja Kanda ya
Ziwa na wananchi wakawa hawamsikilizi, bali alipopanda jukwaani
Magufuli, wananchi wakanyamaza na Kikwete akarudishiwa kipaza sauti
akaendelea na hotuba yake huku akisisitiza kuwa Magufuli ni kiongozi
imara.
Lakini kama hiyo haitoshi, Rais Kikwete alipotoka
kwenye matibabu nchini Marekani aliwahi kunukuliwa akisema “…nilitaka
kutangaza mapema kuhusu ugonjwa wa kansa uliokuwa ukinisumbua, lakini
Magufuli ndiye alinikataza kufanya hivyo wakati wa kikao cha Baraza la
Mawaziri”. Kauli hii ya Kikwete inachukuliwa kama dalili ya kuonesha ni
jinsi gani anamwamini Magufuli. Na hata katika hotuba zake Dk Magufuli
hakosi kumsifu Dk Kikwete.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo la kwanza linaloweza kumwangusha Magufuli ni
dhana ya “ugeni” ndani ya CCM. Magufuli hakuwahi kuwa kiongozi wa CCM
na hakuwahi kuitumikia CCM. Yeye amefanya kazi serikalini kisha akawa
mbunge, na kwa miaka 20 sasa amekuwa waziri na si kiongozi wa CCM.
Wahafidhina na watu wasiokubali mabadiliko ndani ya CCM wanamchukulia
kama “mtu wa kuja” kwenye chama chao na ikiwa sauti zao zitakuwa nyingi
anaweza kuangushwa.
Kitu cha pili ni misimamo yake. Misimamo inaweza
kumvusha Magufuli kwenye mchujo wa wagombea wa CCM, pia inaweza kabisa
kumwangusha. Ikiwa upitishaji wagombea utafanywa kwa lengo la kupata mtu
ambaye ikiwa atakuwa rais atakuja kuendeleza mitandao, kujuana na
kubebana, nadhani Magufuli ataogopwa. Misimamo yake katika baadhi ya
mambo imekuwa ikiwakwaza makada wa chama hicho ambao wangependa ulaji
uendelee kuwepo, kwa hiyo, sifa hii inaweza kutumika kumpunguza.
Jambo la mwisho linaloweza kumwengua kwenye safari
hii ni kukosa kundi kubwa ndani ya chama linalomuunga mkono. Ndani ya
CCM, kwa wanachama wa kawaida, naambiwa hata katika vikao vya chama
hicho, Magufui hana uungwaji mkono mkubwa. Hali hii inaweza kuwa kikwazo
kwake, hasa itakapotokea kuwa makundi makubwa ya wasaka urais yakapenya
na kufanikiwa kuteka mwelekeo wa maamuzi ya chama hicho.
Asipopitishwa (mpango B)
Magufuli anaweza kuwa na mipango miwili muhimu kwa
sasa. Kwanza, kuendelea na ubunge katika jimbo la Chato. Pamoja na kuwa
hali yake ya kisiasa ndani ya jimbo si salama sana kwa maana ya nguvu
ya UKAWA kuzidi kuwa kubwa, bado anaweza kurejea na akafanikiwa na
huenda, kama chama chake bado kitachaguliwa kuongoza dola baada ya
uchaguzi, anaweza kupenya na kuchukua nafasi ya juu zaidi ya uwaziri.
Pili, aaweza kurudi chuo kikuu ili kufundisha
vijana. Kama tunavyofahamu nchi yetu iko kwenye kampeni kali ya
kuhamasisha vijana wasome sayansi na Magufuli ni mwanasayansi aliyebobea
katika masomo ya Kemia na Hisabati. Atakuwa na fursa nzuri sana ya
kulisaidia taifa kukuza uwezo wa taaluma ya vijana katika maeneo
aliyobobea.
Hitimisho
Wahenga walisema, “mwenda pole ndiye hula vinono”.
Mipango ya kimya kimya ya Magufuli katika safari ya ikulu kupitia CCM
inaweza kuwa na maana kubwa sana. Tayari tumekwishaona makada wote wa
chama hicho ambao walianza safari hiyo kwa fujo na mbwembwe wakionywa na
kuwekwa kwenye uangalizi maalum. Inawezekana Magufuli alisoma “mchezo”
huu mapema na akawa hataki “kudandia treni kwa mbele”.
Nachokiona mimi ni kuwa Magufuli ni mmoja wa wana CCM tishio sana dhidi ya makundi makubwa ya vigogo ambayo yamejipanga kuingia ikulu muongo mmoja uliopita. Namtakia ndugu John Pombe Joseph Magufuli, safari salama na ya heri katika mbio hizi.
CHANZO: MWANANCHI
Nachokiona mimi ni kuwa Magufuli ni mmoja wa wana CCM tishio sana dhidi ya makundi makubwa ya vigogo ambayo yamejipanga kuingia ikulu muongo mmoja uliopita. Namtakia ndugu John Pombe Joseph Magufuli, safari salama na ya heri katika mbio hizi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment