Mama na mtoto wake wakiwa ndani ya chandarua kijikinga dhidi ya mbu waenezao malaria na homa ya matende.
Ukitaja mbu, wazo litakalomjia mtu kwa haraka
ni ugonjwa wa malaria. Hiyo inatokana na mazoea yenye ukweli kwamba,
mdudu huyo hueneza ugonjwa huo kama ilivyo kwa malale na matende.
Lakini kuna baadhi ya mambo kuhusu tabia ya mbu
ambayo watu wengi hawayafahamu, mbali na sifa yake ya kueneza
magongwa, hasa malaria.
Hebu jiulize; hivi umewahi kukaa na wenzako watano
lakini ukajikuta ni wewe peke yako ndiye unayelalamika kwamba
unang’atwa na mbu?
Kama umekutwa na hali hiyo, basi unaweza kuwa mmoja wa watu walio kivutio kwa mbu.
Kwa kawaida, mvuto hutokana na harufu ya asili inayotoka mwilini mwa mtu anayeshambuliwa zaidi na mbu.
Wanasayansi wanasema kwamba mtu mmoja kati ya
watano huwa kivutio cha mbu na kwamba mdudu huyo akinusa harufu ya mtu
huyo, hata akiwa na wenzake zaidi wanne, basi atakwenda kwake na kwamba
hata akifukuzwa, mbu huyo atarudi na kumuuma tena mtu huyo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa Marekani, Joseph
Mercola anasema kuwa kuna aina nyingi za mbu, lakini asilimia kubwa ya
mbu wenye tabia hiyo ni mbu jike aina ya Anofelesi, ambao pia huambukiza
malaria.
Anasema kuwa mbali na tabia hiyo mbu hao huvutiwa
na maeneo yenye kemikali kwa kunusa harufu hiyo umbali wa mita 50
kutoka walipo kabla ya kwenda kwenye eneo hilo. Mbu jike ndiyo huvutiwa
zaidi na kupenda kunyonya damu ya binadamu kuliko mbu dume.
Dk Mercola ambaye ameandika majarida mbalimbali ya
afya, anasema kuwa mbu jike hupendelea kufanya hivyo kwa sababu madini
ya chuma na protini wanayonyonya kwenye damu ya binadamu huwasaidia
kutengeneza mayai na baadaye kuzaliana.
Kutokana na hilo, wanasayansi wamebaini kuwa mbu huvutiwa na bakteria.
Wanasema binadamu ana bakteria trilioni moja
kwenye ngozi, lakini kati ya hao, asilimia 10 tu ndiyo hufanana kwa
binadamu wote na asilimia nyingine hutofautiana, hali ambayo huchangia
baadhi ya watu kuumwa zaidi na mbu kuliko wengine.
Mazingira
Kwa mujibu wa wanasayansi hao, asilimia kubwa ya mbu huvutiwa
zaidi na harufu ya kemikali ya lactic, ammonia, carboxylic na octenol
ambazo hutoka kinywani kwa binadamu, kwenye jasho, pamoja na gesi carbon
dioxide anayotoa binadamu.
“Kadri unavyotoa hewa yenye gesi ya Carbon dioxide
ndipo unavyowavutia zaidi mbu. Kutokana na hilo, watu wanene hung’atwa
zaidi na mbu kwa sababu hutoa harufu hiyo zaidi ikilinganishwa na watu
wembamba,” anasema Dk Mercola.
Moyo
Kuhusu mapigo ya moyo, mtaalamu huyo anasema:
“Kadri moyo wako unavyodunda, ndivyo unavyoweza kuwa kivutio kwa mbu.
Mfano, kama unafanya mazoezi na mwili wako ukapata joto sana lazima mbu
watakung’ata zaidi hasa ukiwa na pumzi ndogo.”
Dk Mercola anasema mbu huvutiawa na harufu inayotokana na mabadiliko ya kemikali ndani ya mwili wa binadamu.
Anaeleza kuwa mara nyingi mabadiliko hayo hutokea na kusababisha mtu kutoa jasho na harufu ya kipekee.
“Kama unanukia harufu nzuri ambayo ni halisi, mbu
hawavutiwi na wewe. Lakini ikitokea unanuka uvundo, basi lazima utakuwa
kivutio chao na watakusumbua na kukuuma zaidi,” anasema.
Maelezo ya wanasayansi hao yanaendana na utafiti
uliofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Ifakara (IHI),
ulioangazia tabia ya mbu hasa harufu, ilipotafiti njia mbadala ya
kukinga binadamu dhidi ya wadudu hao.
Watafiti hao walibaini kuwa, mbali na maeneo yenye
unyevunyevu, mbu huvutiwa zaidi na harufu ya uvundo. Sehemu au kitu
chochote chenye harufu hiyo, huwa na mbu zaidi.
Utafiti huo wa Ifakara, umewawezesha kubuni mbinu
mbalimbali za kuuwa mbu, ikiwamo ya ‘mosquito landing box’, ambalo
hujazwa vitu vilivyovunda pamoja na kifaa chenye shoti na huwekwa nje ya
nyumba ili kuwavutia mbu ambao hufa kwa kupigwa shoti. Boski hilo
hufanya mbu wasiingie ndani ya nyumba.
Daktari kutoka Hospitali ya Mwanyamala, Dar es
Salaam, Dk Syriacus Buguzi anasema kuwa kuna tafiti kadhaa ambazo
zimeonyesha uhusiano uliopo kati ya harufu na tabia ya mbu.
Akitoa mfano wa watu wanaowavutia zaidi mbu
anasema: “Moja tafiti zilizowahi kufanywa ni zile zinazohusu wanawake
wajawazito, ambao hung’atwa zaidi na mbu kutokana na harufu wanayotoa
wakiwa katika hali hiyo.
“Ili kigundua kwa nini kina mama hawa walikuwa wakishambuliwa na
malaria zaidi wakati wa ujauzito, iligundulika kwamba hutoa harufu
fulani inayowavutia mbu … iliaminika kwamba kina mama hao hutoa jasho
lenye kemikali ambayo ina harufu inayovutia mbu.”
Pia, utafiti uliofanywa mwaka 1999 ulibaini kuwa
jasho la binadamu likikaa kwa siku mbili huanza kutoa harufu ya uvundo
na kuvutia mbu, hasa waenezao ugonjwa wa malaria.
Pia, bakteria wanaotengenezwa kutokana na joto, huoza na kutengeneza kemikali yenye harufu inayowavuatia mbu.
Kadhalika, mbu huvutiwa na harufu ya joto
linalotoka kwenye miguu, baada ya kuvaa viatu kwa muda mrefu. Daktari
huyo anasema hata ikitokea mtu amevua soksi na kuzihifadhi bila kuzifua,
mbu watajaa katika sehemu hiyo kutokana na harufu.
Hata hivyo, Dk Buguzi anasema mbali na mbu
kuvutiwa na harufu hizo, kuna wakati pia mwili wa binadamu hutoa harufu
ambayo huwafanya wakimbie.
Anasema harufu hiyo ambayo kitaalamu huitwa
‘methylpiperzine’ ndiyo wataalamu waliyotumia kutengeneza dawa ya
kufukuza mbu inayoitwa kitaalamu ‘DEET’ (N,N-diethyl-meta-toluamide)
Watu wanaotoa kamikali ya ‘1-methylpiperzine’ hawafuatwi na mbua kama ilivyo kwa wale ambao hawatoi kemikali hiyo.
Unawezaje kujikinga
Dk Mercola anabainisha kwamba namna bora na ya asili ya kujikinga na mbu ni kukaa ndani ya nyumba, ambako hakuna mbu.
Anasema ukikaa nje hasa sehemu zenye unyevunyevu ambazo mbu hupendelea lazima watakung’ata.
“Hakikisha unafanya usafi wa mazingira nje ya nyumba yako na kusiwe na unyevunyevu,” anasema.
Taasisi ya Kuzuia Mbu ya Marekani (AMCA) ilianisha
njia nyingine zinazoweza kusaidia watu kujizuia kuumwa na mbu ambazo ni
pamoja na kusafisha mazingira na kuondoa madimbwi ya maji nje ya
nyumba.
Pia, kuvaa mavazi ambayo hayaachi baadhi ya sehemu za mwili wazi
kama miguu na mikono kwa kuwa maeneo hayo yakifunikwa vizuri siyo
rahisi mbu kuuma.
Dk Janet Hull wa Marekani anasema utafiti
uliofanyika mwaka 1960 ulibainisha kuwa, unywaji wa vidonge vya Vitamini
B1 unasaidia kufukuza mbu asimuume binadamu. “Matone hayo husaidia mwili kutoa hafuru ambayo huwafanya mbu wasimsogelee binadamu huyo,” anasema.
Dk Hull anasema kunywa kidonge kimoja cha Vitamini
B1 kwa miezi saba ni njia nzuri inayoshauriwa na wataalamu wa afya ili
usiumwe na mbu.
Anaongeza kuwa ulaji wa vitunguu swaumu mara kwa
mara pia husaidia kutoa harufu ambayo hufanya mbu wakimbie
wanapokaribiana na mtu mwenye harufu hiyo.
Ufanyaje?
Daktari wa tiba ya magonjwa ya binadamu, Samweli Shitta anasema mbali na mbu waenezao malaria, kuna aina nyingi za mbu.
Anasema baadhi ya watu wakiumwa na mbu huvimba,
wengine huwashwa na wengine hupata vipele au harara ambazo huacha makovu
kwenye ngozi.
“Kuna mbu waenezao ugonjwa wa matende, kuna wengine wakikung’ata unawashwa, unapata upele na wengine kupata uvimbe kwa sababu ngozi zinatofautiana,” anasema.
“Kuna mbu waenezao ugonjwa wa matende, kuna wengine wakikung’ata unawashwa, unapata upele na wengine kupata uvimbe kwa sababu ngozi zinatofautiana,” anasema.
Anasema ikiwa mtu amepatwa na hali hiyo anaweza
kutumia dawa za kutibu mzio, ambazo husaidia kupunguza muwasho, kuondoa
harara pamoja na alama zinazoweza kutokea kwenye ngozi.
Dk Mercola anaongeza kuwa, njia nyingine ni
kutumia dawa za asili kama mdalasini kwa kuchanganya na asali, kisha
kupaka mwilini, mafuta ya mzeituni, sabuni ya ‘citronella’ na mafuta ya
nazi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment