
Tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe, limeendelea kupingwa na asasi mbalimbali huku
asasi ya kiraia inayotoa msaada kisheria na kutetea haki za binadamu
nchini (SLPC), ikitaka serikali kuacha kutoa matamko ya vitisho.Mwenyekiti Mtendaji wa SLPC, Masesa Mashauri, alisema serikali
kupitia waziri wake iache kuendelea kutoa matamko ya kutishia kuchukua
hatua bali ichukue hatua hasa pale inapoonekana na kuthibitika kuwa kuna
kila dalili za uvunjifu wa amani.
Jumanne wiki hii, Waziri Chikawe, alitishia kuchukua hatua kali kwa
watu binafsi, vyama vya siasa, kijamii na vya kidini vitakavyobainika
kuvuruga usalama na utulivu wan chi katika kipindi cha kura ya maoni kwa
Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu, huku akitishia kufuta asasi
kadhaa kuanzia wiki ijayo.
Mashauri alisema: “Serikali iache kuendelea kutoa matamko ya
kutishia kuchukua hatua bali ichukue hatua hasa pale inapoonekana na
kuthibitika kuwa kuna kila dalili za uvunjifu wa amani ya nchi yetu,
maana ikitoweka haitakuwa rahisi kuirejesha.”
Alisema ni vema ikamuacha mwananchi huru kutoa uamuzi wa ama kuikubali au kuikataa Katiba inayopendekezwa. “Elimu inayotakiwa kutolewa juu ya jambo fulani kama vile kupiga
kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa, kisha mtu aachwe huru
kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushinikizwa.
Mkoani Morogoro, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk.
Joel Mmasa, alisema anapinga msimamo wa Serikali kuhusu kusudio au hatua
yoyote ile ya kutaka kuvifuta vyama vya kiraia na kidini kwani inaweza
kuchochea migogoro mingine.
Alisema kufuta vyama hivyo ambavyo vimekuwa vikisaidia kwa kiasi
kikubwa kuleta amani ya nchi pamoja na kuchochea shughuli mbalimbali za
maendeleo, kutaanzisha uchochezi, machafuko na kwamba Chikawe
amekurupuka kutoa maamuzi hayo ambayo hayana tija kwa Watanzania.
Mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Dini ya Kiislam mkoani Morogoro,
Abdallah Sareh, alisema kuwa kutishia kufuta taasisi za dini kutokana na
kukiuka Katiba zake sio suluhisho bali sasa ni wakati mwafaka kwa
Serikali kukaa meza moja nao ili kutatua masuala mbalimbali.
Alisema ikiwa Serikali itashikiria msimamo wake, itaanza kuchochea
migogoro mingine ambayo sio mwafaka wakati huu wa kuelekea uchaguzi
mkuu. Mwenyekiti wa Muungano wa vyama visivyo vya Kiserikali mkoani
Morogoro (Ungo), Maliki Malupo, alisema yapo mashirika ambayo yameacha
kazi yao ya kuelimisha umma kupitia usajili wao, hivyo badala ya
kufikilia kuyafuta kwa sasa, ni vizuri Serikali kwanza ikayaonya ili
kurudi katika mstari.
Alisema suala la kuabudu huku likihusisha siasa halihitaji kutolewa
tishio na Serikali bali inapaswa kuwaelimisha viongozi wa dini na kukaa
nao kuzungumza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment