
Kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300
katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
imemuweka katika wakati mgumu Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, baada ya wananchi wa jimbo lake kumuweka kiti moto wakimtaka
atoe maelezo ya kina kuhusu Sh. milioni 40 alizopewa na mmiliki wa
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alikumbana na wakati
mgumu wakati akizungumza na wananchi wa jimbo lake kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Pambalu ambao
walipata fursa ya kumuuliza kihusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika Jumanne wiki hii, mkazi wa
Sengerema mjini, James John, alimuuliza Ngeleja fedha alizopewa na
Rugemalira zimesaidiaje katika miradi ya Jimbo la Sengerema. “Wakati unahojiwa na Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, ulisema
fedha hizo baadhi uligawa katika makanisa na misikiti je, zilizobaki
tueleze zimesaidia katika mradi gani kwenye jimbo la Sengerema, tutajie
hata mradi mmoja,” aliuliza John.
Ngeleja baada ya kuulizwa swali hilo, alidai kuwa fedha alizopewa
ulikuwa ni msaada kutoka kwa rafiki yake Rugemalira, na kwamba alilipa
kodi ya serikali Sh. 13,138,125 na kiasi cha Sh. 27,286,875 kilichobaki
alichangia harambee kwenye makanisa na misikiti jijini Dar es Salaam.
Alisema fedha nyingine alichangia ofisi za vyama vya siasa
majimboni, vikundi vya wajasiriamali na shughuri za maendeleo jimboni
mwake huku akionyesha baadhi ya majina ya watu walionufaika na misaada
hiyo. Ngeleja aliwataka wananchi hao kuacha kusikiliza maneno ya
wanasiasa ambao alidai walilenga kumchafua kutokana na kashfa ya Escrow
akidai wapo viongozi waliopata mgawo katika sakata hilo na kumtaja
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwamba hajaguswa. "Nina vielelezo na ushahidi kuhusu Zitto Kabwe...mtakumbuka
Mheshimiwa Livingistone Lusinde (Mbunge wa Mtera (CCM) alimtuhumu Zitto
kupokea msaada wa zaidi ya Shilingi milioni 30 kutoka kampuni ya Pan
African Power Limited, maarufu kama PAP,” alisema.
Wakati Ngeleja akijitetea baadhi ya wananchi walikuwa wakimzomea na kumweleza kuwa hawadanganyiki huku wengine wakimshangilia. Licha ya Ngeleja kujitetea kwa takribani saa moja, wananchi hao
walionekana kuchachamaa kutokana na ahadi ya upatikanaji wa maji safi na
salama ambayo yamegeuka kuwa hadithi kwao.
"Naomba mnisikilize kwa makini...huyu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) hakumtaja mtu yeyote kwamba alipata fedha
kinyume cha utaratibu...isipokuwa lilipofika kwenye kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), lilikuzwa...na mengine yalikuwa yakitolewa
kwenye magazeti,” alisema Ngeleja.
Machi 3, mwaka huu, Ngeleja alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili
ya Viongozi wa Umma kujibu malalamiko dhidi yake ya kupokea Sh. milioni
40.4 kutoka kwa Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili. Ngeleja akijitetea mbele ya Baraza hilo lililokuwa chini ya
Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alikiri kupokea fedha hizo
kutoka kwa Rugemalira, lakini alisema hazikutolewa kwake kama fadhila za
kiuchumi kama malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake.
Alidai fedha hizo aliomba na kupewa zikiwa ni msaada, ambao
hautofautiani na misaada inayopokelewa na wabunge wengine, ambayo
hubarikiwa na Bunge. Ngeleja alidai mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za
wafadhili, ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto
Kabwe, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
Alidai Zitto alinufaika na msaada wa zaidi ya Sh. milioni 30 na
dola za Marekani 5,000 kutoka PAP na Independent Power Tanzania Limited
(IPTL) alizopata kwa matumizi yake binafsi. Ngeleja alidai misaada
mingine, ambayo Zitto amewahi kuipata ni pamoja na unaohusu Sh. milioni
119.9 na Sh. milioni 79, ambazo alidai kuwa aliipata kutoka Shirika la
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Alidai suala hilo kuhusu Zitto liliwahi kuelezwa na Lusinde na
Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi wa CCM kwa nyakati katika mikutano ya
16 na 17, bungeni, mwishoni mwa Novemba, mwaka 2014. Februari 28, mwaka huu,viongozi watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wanaotuhumiwa kwenye Tegeta Escrow waliondolewa kwenye nafasi za ujumbe
wa Kamati Kuu na Halmashauri.
Waliondolewa ni Ngeleja; aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba, na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge . Tibaijuka na Chenge kila mmoja anadaiwa kupokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa Rugemalira.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment