
Aliyekuwa mwananchama namba saba
wa CCM, Hassan Nassor Moyo amesema hana matatizo na uamuzi wa chama
hicho kumvua uanachama kwa kuwa hakutarajia kama angezaliwa na kuwa
mwanachama wa chama hicho.
Moyo, ambaye amewaelezea waliomtimua kuwa ni
watoto wadogo, ameongeza kuwa pamoja na kutimuliwa hatarajii kujiunga na
chama chochote cha siasa kwa kuwa ni mzee muda huu na anahitaji
kupumzika. Akizungumza kwa simu na Mwananchi akiwa mkoani Tanga ambako
amesema amekwenda kupumzika kwa siku 30, Moyo alisema anachokiona ni
kuwa CCM ya sasa ni tofauti na Tanu na ASP vilivyokuwa vinakubali
kukosolewa. “Mimi nilikuwa ni mwanachama wa ASP, tulikuwa
tukikosoa maamuzi mengi tu vikaoni na (rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid
Amani) Karume hakuwa akikasirika.
“Naambiwa kuwa nimekwenda kinyume na msimamo wa
chama kwa kusema tuwe na muundo wa Muungano wa serikali tatu, kwani
msimamo wa chama ni kuwa na Muungano wa serikali mbili. Hiyo si kweli,
msimamo wa chama ulikuwa serikali mbili kuelekea moja, sasa mbona
hawazungumzii serikali moja, hasa ukizingatia kuwa muundo wa serikali
mbili ulikuwa ni wa mpito tu?” alihoji Mzee Moyo. Moyo, ambaye alikuwa
waziri wa kwanza wa elimu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amekuwa
akiikosoa Serikali ya Zanzibar kwenye mikutano mbalimbali, ikiwamo
anayoiitisha kuzungumzia masuala mbalimbali.
Alipinga bayana muundo wa serikali mbili na
kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kuwa na mamlaka kamili, mambo ambayo ni
kinyume na msimamo wa Serikali ya CCM. Moyo amekuwa akizungumzia umuhimu
wa kuandika Katiba mpya tangu mwaka 2009 na amekuwa akikiri kuwa
Zanzibar iliukubali Muungano bila ya matatizo, na hata suala la gesi
ambalo alisema liliingizwa mwaka 1968, lakini anasisitiza kuwa kama kuna
kosa lilifanyika, vijana hawana budi kulihoji kwa kuwa walisomeshwa ili
wapate ufahamu huo. Alipoulizwa kuhusu msimamo wake hivi sasa baada ya
kufukuzwa na chama chake, Mzee Moyo alisema msimamo wake bado ni
maridhiano. “Mimi nilikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano,
CCM wanasema kamati hiyo hawaitambui, ni sawa kabisa kwani kamati ile
haikuwa ya chama chochote kile, ilikuwa ni Kamati iliyoundwa na watu
wenye nia njema ili kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar,” alisema.
“Kamati hiyo iliundwa baada ya Kamati Kuu ya CCM
iliyoketi mjini Butiama na kuamua kuwa ipo haja ya kuwa na maridhiano
Zanzibar ili kutuliza hali ya hewa ya kisiasa iliyokuwa ikichafuka kila
uchao.
“Kwa kweli tulifanya kazi kubwa mpaka yakapatikana
maridhiano ambayo ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa. Kusema kweli kazi tuliyofanya ni nzuri, kwani nchi imetulia,
na hali hiyo mimi najivunia.”
Je, atajiunga na CUF?
Mwanasiasa huyo alisema ameshakuwa mtu mzima, hivi
sasa anahitaji kupumzika na alishaacha siasa zamani hadi wenzake
walipokwenda kumwomba aingie katika Kamati ya Maridhiano. “Sitaki
kujiunga na chama chochote cha siasa, mimi ni mzee sasa, nahitaji
kupumzika,” alisisitiza Mzee Moyo.
Kuhudhuria mikutano ya CUF
Moyo amekuwa mwana-CCM tofauti kutokana na
kuhudhuria vikao vya chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, lakini
anatetea kitendo hicho. “CUF walikuwa wakinialika walipokuwa wakifanya mikutano yao na
nilichokuwa nikizungumzia ni maridhiano na matakwa ya Wazanzibari kuwa
na muundo wa Muungano wenye maslahi na wao zaidi, na hayo ndiyo maoni ya
wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo hapo
hakuna langu jipya nililolibuni,” alisema.
Alisema CCM haijawahi kumwalika katika mikutano
yao ya hadhara na zaidi inasema kuwa Kamati ya Maridhiano hawaitambui,
hivyo yeye hakupata nafasi ya kuzungumza kwenye mikutano ya CCM na
angepewa nafasi hiyo angeyazungumza yale yale aliyoyazungumza kwenye
mikutano ya CUF.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment