
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amerejea kutoka Marekani huku akieleza
kuwa utoaji wa zabuni ya kuingiza nchini vifaa vya uandikishaji katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura (BVR kits), ulikubikwa na ufisadi na
usanii katika utoaji wa zabuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, baada ya
kuwasili, alisema Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ilikataa zabuni ya
kwanza ya uletaji wa vifaa hivyo nchini, lakini serikali ikachomeka
suala hilo bila kutangaza zabuni kama taratibu na sheria zinavyoelekeza. “BVR ni ufisadi na usanii na ndiyo maana hakuna anayejua na
hawataki kutoka hadharani kueleza mzabuni alipatikanaje,
PPRA walipokataa zabuni ya kwanza serikali ikaenda kuchomeka bila
kutangaza zabuni,” alisema.
Dk. Slaa alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekuwa
ikilalamikiwa kuhusiana na kuchelewa kuletwa kwa BVR, lakini dosari ya
msingi katika suala la BVR ni serikali kushindwa kutoa fedha kwa ajili
ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Alisema Agosti 30 na Septemba 8, mwaka jana, viongozi wa vyama vya siasa nchini walikutana na Rais Jakaya Kikwete kujadiliana masuala kadhaa likiwamo la uandikishaji wa daftari la
wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR na kukubaliana kuwa mambo
ambayo siyo ya kikatiba na yasiyo ya lazima yasifanyike kwanza katika
kipindi hiki ili kupunguza gharama.
Alisema miongoni mwa mambo waliyoyaomba yasifanyike kwanza ni kura
maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa kwa kuwa siyo jambo la
kikatiba, lakini katika hali ya kushangaza serikali ikatangaza tarehe ya
kufanyika kura ya maoni licha ya kuwapo makubaliano hayo. “Rais Kikwete alikubali na kupendekeza kuahirishwa kura ya maoni
hadi baada ya uchaguzi mkuu ili kuokoa fedha ili zitumike kwenye
uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, lakini hilo
halikuzingatiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa hadi sasa serikali imetumia fedha nyingi sana
kufanya kampeni kwa ajili ya kura ya maoni na cha kushangaza ni kuwa
serikali ndiyo inayofanya kampeni badala ya wananchi.
Dk. Slaa alisema wamebaini kuwa kuandikisha wapiga kura kwa kutumia
BVR ni mbinu inayofanywa na serikali kwa sababu kuna maeneo ambayo
wananchi hawataandikishwa na ndiyo maana wameanza maeneo ambayo ni ngome
za Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Tunataka kuwaambia kuwa tumeshtukia na tunatoa rai kwa Rais
Kikwete nchi hii ni muhimu kuliko yeye, nchi ni muhimu kuliko CCM na
kuliko Chadema, hata siku moja upinzani hauwezi kuleta vurugu utaletwa
na serikali yenyewe inayotaka kulazimisha mambo yake,” alisema.
Hata hivyo, alisema kukwama kuandikisha wananchi katika daftari kwa
kutumia BVR Chadema haiwezi kukimbilia mahakamani kwa sababu zipo kesi
nyingi za Chadema ambazo hazijaanza kusikilizwa.
MAJIBU YA TUME
Alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian
Lubuva, alisema mchakato wa kumpata mzabuni ulifuata taratibu zote za
kisheria na kama kuna ambaye hakuridhika, alipaswa kukata rufaa kwa
mujibu wa sheria.
Alipoulizwa kuhusu kampuni zilizoomba zabuni ya kuleta BVR, alisema
aulizwe Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba. Hata hivyo, Malaba,
alipoulizwa, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa
ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
Kuhusu madai kuwa uandikishaji unapendelea CCM, Jaji Lubuva alisema
uandaaji wa ratiba hauangalii vyama bali waliangalia mikoa jirani na
Mkoa wa Njombe ambao ulikuwa wa kwanza kuandikisha wapigakura.
AONYA UCHAGUZI MKUU
Dk. Slaa akizungumzia suala la uchaguzi mkuu unaoatarajia kufanyika
Oktoba mwaka huu, alisema serikali isithubutu kuuahirisha kwa kuwa upo
kwa mujibu wa katiba na kama inataka kufanya hivyo ijifunze katika nchi
nyingine ambazo zimekumbwa na machafuko kwa sababu watawala wake
wamekuwa ving’ang’anizi wa madaraka. “Tunataka kumwambia Kikwete muda wake unaisha Oktoba 28, mwaka huu mpaka pale atakapoapishwa rais mpya,” alisema.
Alimtaka Rais Kikwete apunguze ziara za nchi na badala yake atumie
fedha kwenye daftari la kudumu la wapigakura ili wananchi wengi wapate
fursa ya kupigakura.
ACT HAWANA UBAVU KWA CHADEMA
Akizungumzia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo, alisema hakiwezi kuitisha Chadema hata kidogo. “Chadema tumeijenga kuanzia ngazi za chini kwa miaka mingi,
hatumuogopi yeyote. Dk. Slaa, Mbowe na timu nzima tumezunguka Tanzania
nzima kijiji kwa kijiji, hivyo hakuna mtu yeyote atakayekuwa tishio
kwetu,” alisema.
AUPINGA MUSWADA WA MAKOSA YA MTANDAO
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015,
alisema sheria hiyo haifai na kwamba atakuwa tayari kuwa mtu wa kwanza
kufungwa kwa sababu haiwezekani mtu atumiwe ujumbe mfupi wa maneno
katika simu yake halafu anakamatwa na kushitakiwa. “Hatuogopi kufungwa, mimi nitakuwa wa kwanza kwenda kupelekwa
gerezani kwa sababu ninaamini kama nitaletewa meseji au jambo lolote
litakalohusiana na hiyo sheria na nikapelekwa mahakamani ndiyo utakuwa
ukombozi wa Taifa hili utaanzia hapo hapo,” alisema.
Alisema ni kitu ambacho hakiwezekani kwenda kumshtaki mtu kwa
kuandika mawazo yake, fikra zake kwenye mtandao bila kueleza ni fikra
hizo zinakiuka vipi fikra za mwingine kwani kosa ni kukiuka haki ya mtu
mwingine, lakini siyo kuandika fikra kwenye mtandao.
VURUGU AFRIKA KUSINI
Alisema vurugu nchini Afrika Kusini wanazofanyiwa raia wa kigeni
zimetokana na serikali ya chama cha ANC kushindwa kuwahudumia vijana
wake na kwamba hilo bomu linaweza kutokea hata Tanzania. “Kuna vijana wengi hawana ajira, na ndiyo maana yanazaliwa makundi kama Panya road, Mbwa mwitu chanzo ni kukosa ajira,” alisema.
Dk. Slaa alisema: “Ifike mahali Waafrika wawe watu wa demokrasia,
mwenzao akikosea akavuruga demokrasia, unamwambia kwamba amekosea bila
kuoneana aibu.” Alisema msingi wa ziara yake ni kwenda kujenga mahusiano Marekani na kwamba amejifunza mambo mengi.
ZIARA YAKE MAREKANI
Dk. Slaa alifanya ziara hiyo kufuatia mwaliko wa Gavana wa Jimbo
la Indiana, Mike Pence, pamoja na taasisi mbalimbali za Marekani
vikiwamo vyuo vikuu kutokana na kutambua mchango wake na chama chake
kisiasa na kijamii katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Akiwa nchini humo alishiriki mijadala mbalimbali inayohusu
uwekezaji, elimu na uongozi iliyoandaliwa kwa ajili yake ambayo
lengo lake kuu ni kuitangaza Tanzania na mihadhara kwenye vyuo vikuu
vya Purdue, Indiana na Marion.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment