Pages

Thursday, April 02, 2015

TANZANIA NI MHIMILI MKUU WA UCHUMI AFRIKA MASHARIKI NA KATI


Kutoka kushoto ni Rais wa Uganda ,Yoweri Museveni, Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza walipokutana jijini Dar es Salaam kuhimiza uimarihshaji wa miundombinu ya barabara na reli ili kuimarisha uchumi wa nchi hizo.
Mkutano wa marais wa nchi zinazounda Ukanda wa Kati wa Kibiashara, Barani Afrika, wamekutana jijini Dar es Salaam na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza sekta ya miundombinu ya barabara na reli, kwa manufaa ya mataifa hayo.
Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Justine Kanumba kwa niaba Rais Joseph Kabila.

Uzinduzi wa reli
Rais Kikwete na Rais Nkurunziza wamefungua ukurasa mpya wa kuzindua safari za moja kwa moja za treni za mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Uganda. Nyuso za furaha zinatawala wakati wa uzinduzi huo. Katika kulionyesha hilo, marais hao wanainua bendera za rangi ya kijani juu kuonyesha kuruhusu treni hiyo yenye uwezo wa kubeba makontena kati ya 10 na 15.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini kwa sasa zitakuwa zinachukua siku mbili pekee,” anasema Rais Kikwete.
Rais Nkurunziza anasema kuanza kwa safari hizo za kuelekea nchini kwake ni jambo la kujivunia kwa kuwa awali mizigo ilikuwa ikichukua muda mrefu, lakini uamuzi wa Serikali ya Tanzania kupunguza muda wa safari hizo kutoka wiki mbili hadi siku mbili una faida kwa pande zote mbili. “Safari hizo zitasaidia nchi yangu kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa haraka,” anasema Rais Nkurunziza.
Rais Kikwete anasema Serikali yake imenunua injini 13 za treni na kwamba, kati ya hizo mbili ziliwasili nchini wiki mbili zilizopita. Zingine tano, anasema zinatarajia kuwasili nchini mwezi huu na zilizobaki zitaletwa mwezi ujao. Zaidi ya hayo anasema wamenunua mabehewa 274 na kati yake, 150 yaliwasili nchini Februari mwaka huu. Rais Kikwete anasema anatamani ifike siku moja, Tanzania iwe na treni ya mizigo ya ghorofa tatu, yenye mabehewa mia, inayoweza kuchukua makontena mia tatu, ili kurahisisha usambazaji wa mizigo toka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi jirani.
Hata hivyo, anasema ili kutekeleza mipango hiyo yenye manufaa kwa nchi za ukanda wa kati kwa ufanisi, ni vyema kuwa na wazo la Serikali kuwa mmiliki wa reli, lakini biashara isimamiwe na sekta binafsi.

Kuondoa vikwazo
Katika ufunguzi, Rais Kikwete anaainisha mikakati mbalimbali iliyowekwa na Tanzania kuhakikisha miradi ya ukanda wa kati iliyopo nchini inafanikiwa kwa faida ya nchi zote wanachama. Rais Kikwete anasema Serikali yake inakusudia kuondoa kila kikwazo kilichokuwa kinakwamisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani.
Anasema pia, Serikali imeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura (Kagera). “Kuna wakati tulikuwa na vizuizi 47 kila sehemu unatoa kitu kidogo, lakini sasa tumeamua viwe vitatu. Pia, tutaanza kutumia mizani ya barabarani ya kisasa,” anasema Rais Kikwete.

Reli ya kisasa
Ukanda wa kati unatarajia kutekeleza miradi 23 kwenye sekta ya uchukuzi. Kati ya hiyo, kilomita 2,707 za reli, kilomita 2,406 za barabara na bandari kubwa tatu zilizopo nchini.
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta anasema ujenzi wa reli hiyo utaanza mwaka huu. “Tunatarajia kuanza ujenzi huo ndani ya mwaka huu. Ifikapo Juni Rais Jakaya Kikwete atakwenda kuweka jiwe la msingi katika kituo cha stesheni kule Mpiji ambako reli itaanzia,” anasema Sitta, akifafanua kuwa mradi huo utagharimu Sh14 trilioni. Anasema ujenzi huo unatarajia kukamilika ndani ya miaka mitano na utasaidia kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji wa mizigo kwenda nchi za jirani kama Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Reli hiyo yenye uwezo wa kubeba treni yenye mabehewa umbali kilomita moja kwa safari moja itasaidia pia katika usafirishaji wa wananchi,” anasema Sitta. Anasema ujenzi huo ni mradi mkubwa zaidi kuwahi kuwekezwa nchini na utatekelezwa na kampuni mbalimbali za China.
Sitta anasema hadi sasa, Kampuni ya Rasilimali za Reli (Rahco) imekamilisha taratibu za kumpata mshauri wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Rothschild ya Marekani ambayo itawezesha kupata fedha za ujenzi wa reli hiyo. Rais Kagame anapongeza mpango huo, akisema, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya uchukuzi hasa reli inaboreshwa.
Anasema maboresho na mikakati ya miundombinu hasa wa kujenga reli ya kisasa ni hatua nzuri lakini jukumu hilo lisiachiwe nchi moja pekee bali wahusika wote washiriki kikamilifu.
“Mkakati huu unahitaji ushirikiano kati ya Serikali za nchi washirika pamoja na sekta binafsi kwa sababu inahitaji uwekezaji mkubwa,” anasema Rais Kagame mbele ya wawekezaji zaidi ya 300 wa miradi 23 ya ukanda wa kati.
Rais huyo anasema umefika wakati kwa nchi wanachama kuhakikisha kuwa mipango yote inatekelezwa kwa wakati. “Siyo mara ya kwanza tunakutana kujadili masuala kama haya. Lakini sasa umefika wakati wa sisi kwenda mbele na siyo kurudi nyuma tena. Ukanda huu ni muhimu sana kwani unawaunganisha watu wetu pamoja, unasaidia kuchochea na kuongeza fursa mbalimbali za uchumi kwa nchi zetu,” anasema.
Anasema nchi wanachama wa ukanda wa huu wanapaswa kutambua mchango wa uwekezaji katika ukanda huo kwani matunda yake yataliwa kwa ujumla. Rais Museveni anasema hakuna namna ujenzi wa reli unaweza kuepukika kwa kuwa barabara zinaharibika mara kwa mara huku zikigharimu fedha nyingi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed anasema miradi iliyoanzishwa chini ya jumuiya, itachangia sehemu kubwa kuimarisha hali ya kiuchumi iliyokuwa imekwama kutokana na miradi ya miundombinu kushindikana.

Bandari
Kuhusu ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, Rais Kikwete anasema idadi ya mizigo inayosafirishwa imeongezeka kutoka tani milioni 9.2 mwaka 2010 hadi milioni 14, mwaka jana na kufikia mwishoni mwa mwaka huu inatarajiwa kufikisha milioni 18.
“Idadi ya siku za kutoa mzigo bandarini zimepungua kutoka siku 21 hadi 9 na bado tunataka zipungue zaidi. Kuhusu wizi hakuna taarifa ya tukio lolote kwa miaka miwili sasa…Pia Serikali ina mpango wa kujenga bandari mpya Bagamoyo itakayoweza kuhifadhi tani milioni 240 kwa mwaka,” anasema Rais Kikwete.
Kuhusu ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, marais Kikwete na Rais Kagame wanasema ufanisi uliopo bandarini hapo hivi sasa unaridhisha na kwamba unaongeza kasi ya kukua kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

Usalama bandarini
Rais Kikwete anazihakikishia nchi za Afrika Mashariki na Kati kuwa kuna usalama wa uhakika wa mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam.
Wakiwa katika kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS bandarini hapo, Rais Kikwete anasema uongozi wa bandari uliamua kuwatimua wafanyakazi ambao hawakuwa waaminifu. “Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” anasema Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Rais Kagame anasema amefurahishwa na mafanikio yaliyofikiwa bandarini hapo kwa kuwa ni faida kwa Rwanda pia. “Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu Rwanda tunafaidika,” anasema Rais Kagame.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadhi Massawe anasema ipo tofauti kubwa ya utendaji kazi kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ‘pinzani’ ya Mombasa nchini Kenya.
Anasema ingawa nchi za Maziwa makuu zinatumia bandari hizo mbili, Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inayosafirisha mizigo mingi zaidi. Massawe anasema tangu kufanyika kwa maboresho bandarini hapo, idadi ya mizigo inayopelekwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda, imeongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TICTS, Walles Paul anaiomba Serikali kuongeza eneo la kufanyia kazi kwa maelezo kuwa uamuzi huo utasaidia kuendeleza mafanikio yanayopatikana hivi sasa. “Nafasi haitoshi tunahitaji kuongezewa ili tusirudi nyuma tulikotoka,” anasema Paul.

Vikwazo vya kibiashara
Kwa upande wake, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni anatumia mkutano huo kuwakumbusha wanachama wa nchi za ukanda wa kati kuvitazama kwa makini vikwazo vya kibiashara vinavyoweza kuwakwamisha.
Kiongozi huyo anataja vikwazo hivyo kuwa ni ukosefu wa usalama katika nchi, wafanyakazi kukosa ujuzi unaostahili, ukosefu wa masoko na kutopatikana kwa faida iliyokusudiwa.
Anasema ili mipango ya kibiashara inayopangwa na nchi hizo ifanikiwe lazima vikwazo vijulikane na kutafutiwa ufumbuzi mapema. “Wataalamu wa uchumi wanasema gharama ya usafiri katika biashara inapaswa kuwa asilimia 40, mtaji asilimia 20, kazi asilimia 10, ukilitimba asilimia tano, lazima tujiulize kikwazo kipi kinatukwaza,” anasema Museveni.
Ukanda wa kati wa kibiashara ulianzishwa mwaka 2006 chini ya mapatano ya nchi tano za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Tanzania na Uganda.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment