Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dar es Salaam, Daniel Mtuka
 
            
Wakati viongozi wa CCM 
wanaendelea kupiga kelele bila ya kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya 
rushwa wanavyodai vinafanywa na makada wanaotaka uongozi wa nchi, 
Takukuru iko tayari kukisaidia chama hicho kikongwe kupambana na uhalifu
 huo kama kitakuwa tayari kutoa ushirikiano.
Karibu viongozi wote wa CCM wameshanukuliwa wakilalamikia kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho, hasa nyakati za uchaguzi, lakini wamekuwa wakieleza tu kwamba wahusika watawajibishwa na vyombo vya maadili vya chama hicho, licha ya vitendo hivyo kuwa vya uhalifu.
Karibu viongozi wote wa CCM wameshanukuliwa wakilalamikia kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho, hasa nyakati za uchaguzi, lakini wamekuwa wakieleza tu kwamba wahusika watawajibishwa na vyombo vya maadili vya chama hicho, licha ya vitendo hivyo kuwa vya uhalifu.
Juzi, akiwa kwenye vikao vya ndani na viongozi wa 
chama hicho wa Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangulla
 alisema fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”,
 zitakuwa kitanzi chao kwenye uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa wanachama 
hao watang’olewa.
Lakini wakati wasomi waliohojiwa na Mwananchi 
wanahoji sababu za chama hicho kutowashitaki makada hao kwenye chombo 
kinachojishughulisha na kupambana na rushwa, ofisa huyo wa Takukuru 
amesema inawawia vigumu wao kuwashughulikia wahalifu hao bila ya 
viongozi kutoa ushirikiano.
“Taasisi iko tayari hata kama viongozi au 
wanachama watatuletea malalamiko hayo leo (jana). Bila ushirikiano wa 
viongozi inakuwa vigumu kufuatilia,” alisema kamanda wa Takukuru wa Dar 
es Salaam, Daniel Mtuka.
“(Iwapo watatoa ushirikiano) Itakuwa rahisi kuona 
tunaanzia wapi, pia (kwa kuangalia) mfumo wa chama, taratibu zake, 
katiba na ilani yake wanafanyaje kazi,” alisema.
“Kwa kesi ya rushwa kwa wagombea hao, ni vigumu 
kwani tuliwahi kukutana na changamoto ya kushindwa kufanya kazi yetu 
miaka iliyopita tulipomnasa mgombea fulani wa ubunge CCM ambaye pia 
alikuwa kiongozi wa chama. Sisi tulidhani ni tatizo, lakini hali hiyo 
ikaonekana kuwa siyo tatizo, akasema ni sahihi na ataingia kutekeleza 
ilani ya chama.”
Alisema kutokana na mazingira hayo ni muhimu zaidi
 kupata ushirikiano wa chama ili kurahisisha kazi yao hasa katika 
kipindi cha kuelekea uchaguzi ambacho kinatazamiwa kuwa na matukio mengi
 ya rushwa kuanzia ndani ya vyama vya siasa.
“Lakini kwa sasa tumeshaanza kufanya uangalizi wa ndani ya vyama ili kuhakikisha rushwa haichukui nafasi katika uchaguzi huu.”
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa 
Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata 
mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia 
rushwa ndani ya chama hicho. Alisema rushwa inayoendelea kwa sasa iko 
wazi na kwamba sheria ya gharama za uchaguzi 2010 inawapatia mamlaka ya 
kufanya kazi bila vikwazo.
“Sheria hiyo inawapa mamlaka ya kuchunguza 
mazingira haya. Hakuna asiyeona wazi mazingira ya rushwa kwa wagombea 
kwani kama mtu anataka kugombea kisha anawachukua makada kwa ajili ya 
kula nao chakula nyumbani kwake, unadhani kuna nini kinaendelea hapo? 
Hilo mpaka waambiwe, nadhani huko ni kukwepa majukumu yao,” alisema 
Nape.
Mbali na Mangula, wengine waliowahi kulalamikia 
rushwa ndani ya chama hicho ni Mwenyekiti Jakaya Kikwete ambaye 
alitahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kukiuangusha chama. Kadhalika, 
Nape amekuwa akilalamika dhidi ya makada wanaotaka urais kuwa wanahonga 
wanachama.
Aidha, Bernard Membe na Fredrick Sumaye ambao wanatajwa kuwa na 
nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, wameshawahi kulalamika 
kuwa rushwa imezidi ndani ya CCM hasa kipindi cha uchaguzi na kuonya 
kuwa ikiendelea chama hicho kinaweza kuanguka.
Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Baadhi ya wasomi na wanachama wa CCM waliozungumza
 na gazeti hili, walisema kama uongozi CCM una hakika na matukio ya 
rushwa ni vyema ukachukua hatua.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), 
Richard Mbunda alisema tatizo la viongozi wa CCM kutochukua hatua dhidi 
ya rushwa, linachangiwa na kukosekana kwa ushahidi wa watuhumiwa. Alitoa
 mfano wa mkakati wa CCM ulioitwa Kujivua Gamba, ulivyoshindwa kuwaondoa
 viongozi wasio waadilifu kwa kukosa ushahidi. “Kama wanatambua kuna rushwa kwa nini wamekuwa 
wakilalamika wakati kuna vyombo vya kuchunguza? Walitakiwa kufanya 
uamuzi huo muda mrefu, lakini matokeo yake rushwa imeendelea kusambaa 
ndani ya chama mpaka serikalini, kwa wagombea wanaoamua kufidia rushwa 
zao walizotoa ndani ya vyama,” alisema Mbunda.
Profesa Abdul Sheriff, ambaye ni Mwenyekiti wa 
Baraza la Katiba Zanzibar, alisema kama rushwa imekithiri ndani ya 
Serikali, CCM haitakuwa na uwezo wa kuiondoa ndani ya makada wake.
“Viongozi kuzungumza pekee kwenye vyombo vya 
habari haisaidii kabisa na kama wangekuwa na uwezo, basi wangekuwa 
wameshachukua hatua ila kwa sababu ya nguvu za wanasiasa wa Serikali 
sidhani kama wataweza,” alisema Profesa Sheriff.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), 
Bashiru Ally alisema: “Chama hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa 
kujivua gamba na matamko katika vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa 
mifumo imara, fikra sahihi, dira na historia yake nzuri. “Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda 
mambo kinyume na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua. 
(Katibu mkuu wa zamani, Horace) Kolimba aliwahi kusema kuwa CCM haina 
dira wala mwelekeo. Hilo linaonekana sasa, imeshindwa kukemea rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe. Jimbo la Bukoba
 Vijijini limegawanyika kwa sababu ya rushwa inayotolewa na wanaotaka 
ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na kukimbilia yanayotokea Zanzibar,” 
alisema Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana.
Alisema: “CCM ni chama ambacho kinajibu mapigo ila
 hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni dalili mbaya kwake kwani kimekuwa 
dhaifu katika kuwashughulikia wanachama wake wasio waadilifu.”
Mwishoni mwa mwaka jana, Mangula alikaririwa na 
gazeti hili akisema kuwa suala la rushwa linafuatiliwa kwa karibu na 
dawa yake itapatikana baada ya vikao vya kamati ya maadili.
Mangula alitoa kauli yake huku kukiwa na madai kuwa baadhi ya 
wanachama wanagawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu 
ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.
Mangula pia aliwahi kukaririwa na gazeti la CCM 
mwishoni mwa mwaka jana, akisema: “Hakuna mwanachama aliye juu ya 
katiba, kanuni na miongozo ya chama na hivyo hakitamvumilia mtu yeyote 
atakayebainika kutumia fedha.”
Oktoba 25, mwaka juzi, Rais Kikwete alisema endapo
 rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM, chama hicho kitaanguka vibaya katika
 Uchaguzi Mkuu 2015 na iwapo kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Sumaye aliyewahi 
kuliambia gazeti hili kuwa iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM 
itaendelea kulalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya
 kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza mkakati wa 
‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa 
ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata baada ya 
muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili
 maudhui yake.
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya CCM, mbunge 
wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki alisema kwenye akaunti yake ya 
twitter: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM ni 
kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo wa 
uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki 
alisema: “Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku zote, lakini 
nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka wengine 
wanatumia lugha kali... Sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu wengi 
wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki.
aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment