Licha ya ujenzi maghorofa marefu 
kutajwa kuwa kielelezo cha maendeleo katika miji mikubwa, jijini Dar es 
Salaam hali ni tofauti kutokana na hofu iliyopo kuhusu ubora wa majengo 
hayo, mfumo wa majitaka, mipango miji na ukosefu wa maeneo ya maegesho.
Miaka 20 iliyopita, ilikuwa vigumu kuzungumzia maghorofa marefu jijini Dar es Salaam bila ya kutaja majina kama Kitega Uchumi (NIC House), kumaanisha jengo la Shirika la Bima la Taifa lenye ghorofa 16 na urefu wa mita 57.40, IPS lenye ghorofa 12 na urefu wa 43.05, au Extelecom House, kumaanisha jengo la Shirika la Posta lenye ghorofa 14 na urefu wa mita 50.23.
Miaka 20 iliyopita, ilikuwa vigumu kuzungumzia maghorofa marefu jijini Dar es Salaam bila ya kutaja majina kama Kitega Uchumi (NIC House), kumaanisha jengo la Shirika la Bima la Taifa lenye ghorofa 16 na urefu wa mita 57.40, IPS lenye ghorofa 12 na urefu wa 43.05, au Extelecom House, kumaanisha jengo la Shirika la Posta lenye ghorofa 14 na urefu wa mita 50.23.
Lakini anga la Dar es Salaam sasa limepambwa na 
minara ya maghorofa marefu, yakiongozwa na jengo jipya la PSPF Towers 
ambalo urefu wake ni mara tatu ya kimo cha maghorofa yaliyokuwa 
yakisifika miaka 20 iliyopita. Jengo hilo lililo mbioni kukamilika lina 
urefu wa mita 152.85 likiwa na ghorofa 35.
Maghorofa mengine yaliyochomoza miaka michache 
iliyopita ni Uhuru, lenye ghorofa 27, jengo la Kakakuona lenye ghorofa 
37, Benjamin Mkapa lenye ghorofa  37.
Mengine ni PSPF Golden Jubilee Towers lenye 
ghorofa 24 na urefu wa mita 103.2, jengo la uhuru Heights lenye ghorofa 
27 na urefu wa mita 102.6, Umoja wa Vijana  lenye ghorofa 26, Viva Tower
 lililoko Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambalo lina ghorofa 21 na urefu 
wa mita 75.34, BOT Towers lenye ghorofa 20 na urefu wa mita 100 na PPF 
Tower lenye ghorofa 16 na urefu wa mita 57.40.
Majengo marefu, ambayo kwa kawaida hupatikana 
kwenye miji mikubwa ambako hujengwa kutokana na ukosefu wa ardhi kubwa, 
yanatumika kwa ajili ya shughuli za kiofisi, makazi na kibiashara, hasa 
hoteli na klabu za usiku.
Lakini majengo hayo yameongezeka kwenye sehemu 
ndogo ya katikati ya jiji yakitegemea miundombinu iliyowekwa miaka 150 
iliyopita, isipokuwa majengo machache kama Mawasiliano House, Millenium 
Towers na Ubungo Plaza yaliyo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mahitaji ya umeme sasa ni makubwa kuliko wakati 
mwingine wowote, hali kadhalika majisafi wakati kuingia katikati ya jiji
 nyakati za asubuhi na kutoka jioni ni shughuli kubwa kutokana na 
misululu mirefu inayosababishwa na idadi kubwa ya magari yanayobeba 
wafanyakazi wanaoenda kwenye ofisi zinazoendelea kuongezeka.
“Master plan (ramani kuu) ya Dar es Salaam iliisha
 muda wake miaka 36 iliyopita,” alisema meya wa Halmashauri ya Wilaya ya
 Ilala, Jerry Silaa hivi karibuni.
Alisema kukosekana kwa mpango huo, majengo marefu 
yanajengwa kiholela katikati ya jiji na kusababisha matatizo mbalimbali 
yakiwamo ya mafuriko na foleni kutokana na maji kujaa barabarani wakati 
wa mvua.
Silaa alisema baadhi ya sehemu ya zilizokuwa kwa 
ajili ya mashamba na makazi holela ya watu, hivi sasa zimegeuzwa viwanja
 vya kujenga majengo marefu.
Hata hivyo, alisema kutokana na ongezeko la watu 
katikati ya jiji, baadhi ya ofisi zimeanza kuhamishiwa sehemu za kando 
ili kukwepa foleni.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alikiri kuwa 
miundombinu iliyopo hailingani na mahitaji ya ongezeko la maghorofa. “Ni kweli kuwa miundombinu yetu ina walakini 
wakati maghorofa nayo yakichipuka kila siku,” alisema mkuu wa Sadiki 
alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kushamiri kwa majengo marefu. “Hata hivyo, ni dalili ya maendeleo ya kiuchumi kwa upande mwingine,” alisema.
Sadik alishauri maghorofa haya kujengwa katika miji mipya au ‘satelite cities’ ili kuepusha msongamano katikati ya Jiji.
Majengo hayo mengi yanamilikiwa na taasisi za 
fedha, kampuni za ujenzi na mifuko ya hifadhi ya jamii, matajiri 
wakubwa na mashirika mengine. Imeelezwa kuwa kiasi cha Sh800 bilioni 
zimewekezwa kwenye miradi mikubwa mitano, ukiwamo wa PSPF Towers.
Maghorofa ni lazima
Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya makazi ya 
Watumishi Housing, Dk Fred Msemwa alisema ongezeko la maghorofa jijini 
halizuiliki kutokana na mahitaji makubwa ya maeneo ya kufanyia biashara 
na ofisi. “Kasi ya kuongezeka kwa maghorofa ilitokana na 
kuwepo tofauti kubwa kati ya huduma za makazi na mahitaji, hivyo kampuni
 nyingi ziliwekeza eneo hilo ili kutoa huduma inayokosekana. Mpaka sasa 
bado kuna tofauti ndiyo maana majengo yanaendelea kujengwa na yanajaa 
haraka,” alisema.
Ripoti ya Kituo cha Makazi ya Gharama Nafuu (CAHF)
 ya 2014 inaeleza kuwapo kwa miradi mingi mikubwa ya ujenzi ambayo 
itaongeza wingi ya maghorofa hayo kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo inasema Shirika la Nyumba (NHC) pekee 
lina miradi lukuki ya ujenzi wa maghorofa  na inaeleza kuwa shirika hilo
 lina miradi minne na wabia kutoka China ya ujenzi wa majengo pacha 
yenye ghorofa 26 yatakayojengwa kwa Sh70 bilioni.
Inaongeza kuwa yapo majengo matatu yenye ghorofa 
16 yatakayojengwa kwa gharama ya Sh30.3 bilioni kila moja na Group Six 
International na mengine mawili ya ghorofa 16 yanayojengwa na Estim 
Construction.
Pia ipo miradi mingine inayoendelea kama jengo la 
Kakakuona lenye ghorofa 36 litakalokamilika 2017 na Mzizima Tower 
litakalokuwa na ghorofa 33.
Hata hivyo, bado wasiwasi mkubwa ni kasi ya ujenzi huo 
kutolingana na kasi ya uboreshaji huduma hizo kwa jamii kama miundombini
 mibovu ya majitaka ambayo hufurika muda mfupi tu baada ya mvua kubwa 
kunyesha yakiacha takatakla zikizagaa barabarani, wakati ufinyu na 
uchache wa barabara hufanya kuwe na misululu mirefu ya magari wakati 
wakazi wakiwahi kwenye ofisi zinazoongezeka katikati ya jiji kutokana na
 ujenzi wa majengo hayo.
Athari zake
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa baadhi ya
 majengo yanajengwa chini ya kiwango kutokana na ujuzi mdogo, uzembe na 
rushwa na watu kadhaa wameshapoteza maisha kutokana na majengo hayo 
kuporomoka.
Machi 2013, jengo lililozidishwa urefu kinyume cha
 taratibu Mtaa wa Indira Gandhi liliporomoka na kuua watu zaidi ya 30. 
Maofisa wa Manispaa ya Ilala, mmiliki na mkandarasi walishtakiwa.
Ukiacha miradi mikubwa, majengo mengi yamejengwa 
sehemu zisizo na nafasi ya kutosha na hivyo kutoruhusu kirahisi magari 
ya uokoaji.
Mfano mwaka 2013 moto uliposhika ghorofa ya 17 ya 
jengo la PPF Tower, ilichukua saa kadhaa kwa Kikosi cha Zimamoto 
kukabiliana nao.
Matumizi ya umeme
Hadi kufikia Februari, 2014 Tanesco ilikadiria 
kuwa majengo manne tu ya PSPF Twin Tower, Uhuru Height, Viva Tower na 
Benjamin Mkapa Tower kwa pamoja yatatumia megawati 12 za umeme, ambazo 
ni zaidi ya megawati nane zinazotumika na mkoa mzima wa Mtwara.
Kiasi hicho cha umeme ni sawa na umeme unaotumiwa na mkoa huo na Lindi.
Afisa habari wa Tanesco, Adrian Severin alisema 
kuwa idadi ya maghorofa haijawa kubwa kiasi cha kuzidi kiwango cha 
mwisho cha ugavi, lakini akaongeza “tuna hofu tutazidiwa siyo muda refu 
ndiyo maana tunakamilisha ujenzi wa substation ya zaidi ya megawati 100 
kuongeza nguvu kwa iliyokuwepo Barabara ya Sokoine”.
Ofisa Uhusiano wa Shirika la Majisafi na Majitaka 
Dar es Salaam (Dawasco), Everlasting Lyaro alisema baadhi ya majengo 
katikati ya jiji yalijengwa kwa ajili ya makazi ya watu nane, lakini 
yamebadilishwa kuwa ya biashara hivyo kutumiwa na zaidi ya watu 500 huku
 mfumo wa maji taka ukibaki kuwa ule ule wa zamani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment