Mashirika au vyama vya kijamii yanasimamiwa na
Sheria ya Vyama vya Kijamii (The Societies Act). Usajili wa mashirika
haya hufanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia ofisi ya Msajili
wa Vyama.
Ofisi hii ndiyo inapokea maombi ya usajili na kuyapitisha na kuidhinisha juu ya usajili wa shirika hilo au hapana. Ili kufanikiwa kusajili shirika au chama cha
kijamii, unahitaji vitu kadhaa, mfano ni katiba. Katika zitahitajika
ziandaliwe nakala kulingana na uhitaji uliopo.
Kwa kuwa katiba hiyo yaweza kuhitajika katika
ngazi ya kata na wilaya, kabla ya kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi. Ni vyema zikaandaliwa nakala tano au zaidi. Mwishoni zinatakiwa
zibaki nakala tatu za katiba hiyo ambazo zitapelekwa Wizara ya Mambo ya
Ndani kwa ajili ya kuwasilisha maombi ya usajili. Vilevile, wahusika watapaswa kujaza fomu mbili,
yaani SA. 1 na SA. 2 na kutoa nakala nyingine mbili za fomu hizo. Fomu
hizo zinapatikana katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi ya
msajili wa mashirika ya kijamii.
Katika fomu hizo, mtahitajika kujaza taarifa mbali
mbali ikiwemo; jina la shirika, mahali ofisi za shirika zilipo au
zitakapokuwepo, anwani ya shirika, madhumuni ya shirika na sahihi za
viongozi.
Muhtasari wa kikao cha wanachama ni muhimu pia.
Muhtasari huu utaonyesha kwamba kikao kilifanyika na kuamua kuanzisha
shirika hilo, kuteua viongozi wa shirika pamoja na kupitisha rasimu ya
katiba ya shirika hilo na kila aliyehudhuria kikao hicho anapaswa
kusaini kuonyesha kuwa alikuwapo.
Orodha ya wanachama waanzilishi pia ni muhimu. Wanachama hawa waanzilishi hawapaswi kuwa siyo chini ya 10. Wasifu wa viongozi wa shirika (CV) na picha zao.
Pia ni jambo muhimu. Hii itajumuisha wasifu wa viongozi pamoja na picha
zao (passport size). Wasifu huo wa kila kiongozi unapaswa kuwa nakala
mbili au zaidi kulingana na uhitaji uliopo.
Barua ya utambulisho ikiashiria kuungwa mkono, inapaswa kutoka kwa mkuu wa wilaya ambayo ofisi ya shirika ilipo. Wataambatanisha pia barua ya maombi ya usajili
kutoka kwa uongozi wa shirika. Barua hiyo ndiyo inayowasilisha maombi ya
shirika katika wizara ili ianze mchakato wa kushughulikia usajili.
Ada ya usajili inalipiwa katika ofisi za wizara
ili kusaidia mchakato wa usajili upate kuendelea. Ada imegawanyika
katika mafungu mbalimbali ikiwamo; ya usajili, usajili na ya kila mwaka
baada ya kusajiliwa.
Baada ya kusajiliwa shirika hilo linakuwa na nguvu za kisheria
za kushtaki na kushtakiwa, kuajiri, kumiliki mali na kuendelea na
shughuli za shirika hilo.
Jambo la kuzingatia baada ya usajili ni kwamba,
shirika linapaswa kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa katiba na sheria
za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shirika pia halipaswi kujihusisha kwenye shughuli
zozote za kisiasa na linapaswa lidhihirishe kweli limesajiliwa ili
kuisaidia na kuinufaisha jamii na siyo kuwanufaisha watu wachache.
Mnapaswa kuanzisha miradi na kuwa na mipango yenye
kuleta mguso katika jamii husika kwa kuangalia ile inayoweza
kuharakisha maendeleo kulingana na malengo ya shirika.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment