Uwanja wa Kambole leo unakupa fursa ya kusoma na
kuelewa juu ya sheria za mirathi hasa kwenye kipengele cha wasia, watu
wengi wanaweza kudhani wanajua juu ya wasia lakini si kweli.
Wasia ni tamko la mdomo au maandishi anayotoa mtu
wakati wa uhai wake kueleza jinsi atakavyotaka mali zake zigawanywe au
mwili wake utendewe, atakapokuwa amefariki. Wasia ni siri ambayo hufichuliwa pale marehemu
anapofariki. Mtu anayekufa kistaarabu ni yule anayeacha wasia. Mtu
yeyote anaweza kuandika wasia iwapo ana umri wa zaidi ya miaka kumi na
nane na ana akili timamu. Mtu anayeumwa sana au amezeeka sana unapaswa
kuhakikisha anaelewa nini anachoandika kwenye wasia. Kuandika wasia siyo
lazima uwe na mali nyingi. Watu wanadhani kuandika wasia ni mpaka uwe
na mali nyingi au fedha nyingi.
Tunakosea sana. Mali siyo sifa ya kukufanya
uandike wasia, hata ukichagua sehemu ya kuzikwa ni wasia tosha. Faida za
kuandika wasia zipo nyingi. Baadhi ya hizo ni pamoja na kuweka mambo
bayana na kuondoa utata wowote kwenye familia na jamii yako.
Unapata fursa ya kumchagua msimamizi wa mirathi
unaye mtaka, pia unatoa maelekezo juu ya mwili na mali zako kama
unavyopenda wewe na kwa mujibu wa sheria. Pia ni ustaarabu kuandika
wasia.
Wasia unaokubalika kisheria una sifa zifuatazo:
unaweza kuwa wa maandishi au mdomo. Wasia wa maandishi unatakiwa uwe na
mashahidi wawili, na ule wa mdomo unatakiwa uwe na mashahidi wanne.
Ni muhimu mmoja wapo wa mashahidi awe ndugu wa
karibu ila asiwe mrithi. Wasia uwe ni wa mali zako binafsi, siyo za watu
wengine, yaani, huwezi kuandika wasia kugawa mali za watu. Pia,
haikubaliki wasia kumnyima mali mrithi halali wa kisheria. Lakini anaye
andika wasia awe na akili timamu na asiwe mgonjwa sana kiasi cha
kushindwa kuelewa anapotoa wasia. Wasia ulioandikwa kwa kulazimishwa,
siyo halali.
Warithi halali kisheria ni mke ama mume, watoto
waliozaliwa ndani ya ndoa, watoto waliohalalishwa kisheria, pia watoto
wa nje wanaweza kurithi, inategemeana na mila na desturi za marehemu,
lakini siyo ustaarabu kuwanyima maana siyo kosa lao.
Wasia ulioandikwa vizuri ni ule unaoweza kugawa
mali zilizopo na zile zitakazofuata kabla ya kifo, lakini wasia unaweza
kubadilishwa muda wowote kabla ya mhusika kufa na mwenye uwezo wa
kubadili wasia huo ni yeye mwenyewe aliyeuandika.
Mgawanyo wa mali ya marehemu utategemea wasia
ulivyoandikwa. Wasia unapaswa kuheshimiwa, maana yale ni matakwa na nia
ya marehemu kwa hiyo, unapaswa kuheshimiwa kwa kila namna, labda awe
marehemu ametaka vitu visivyowezekana.
Iwapo mtu ambaye marehemu amemtaja kwenye wasia
usimamie mali zake, kama huwezi ni bora kujitoa na sio kukubali halafu
baadaye unachezea mali za marehemu na kujinufaisha mwenyewe.
Hiyo ni kinyume cha sheria na anaweza kushtakiwa
na kudaiwa au kufunguliwa kesi. Wasia unaweza kuhifadhiwa kwa wakili,
mahakamani, benki, taasisi za dini kama kanisani au msikitini, pia wasia
unaweza kutunzwa kwa mtu yeyote ambaye anaaminika na anaweza kutunza
siri, lakini asiwe ni mnufaikaji wa wasia husika. Tuwekane sawa kuwa kuandika wasia siyo uchuro, bali ni kuweka
mambo sawa baada ya wewe kufariki, mali zako zitumike kuwanufaisha na
kuwasomesha watoto na ndugu wa karibu kama wapo.
Hata hivyo, aina za wasia zinategemea mila na
desturi za marehemu na kwa mujibu wa sheria husika. Uhalali wa wasia
unategemea pia sheria husika. Kuna sheria za kiislamu, Kikristo na
kimila.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment