Mchungaji Christopher Mtikila, ameiondoa
mahakamani kesi ya kupinga serikali kupeleka bungeni Muswada wa
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, baada ya jopo la majaji kumshauri
kufanya hivyo kutokana na taarifa za kuondolewa bungeni.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Watendaji wakuu wa serikali akiwamo Warizi Mkuu, Mizengo Pinda. Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya jopo la majaji watatu,
likiongozwa na Mwenyekiti, Richard Mziray, akisaidiana na Jaji Lawrence
Kaduri na Said Kihio katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es
Salaam.
Jaji Kaduri alihoji kama kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo
mahakamani wakati Ikulu imesema serikali haina mpango wa kuanzisha
Mahakama hiyo na Bunge limeshauondoa muswaada huo. Alisema kusikiliza kesi inayozungumzia muswada huo uliondolewa
bungeni haina maana na hata maamuzi yake yatakuwa hayana mashiko
kisheria.
“Watanzania hatujaelimishwa nini kinaanzishwa na kitakuwa na
majukumu gani hali ambayo imetuacha tumechanganyikiwa kuna mgawanyiko
mkubwa mara maaskofu wanasema hili mara wabunge na wananchi pia wanasema
mengine ili mradi tu kila pande inashindwa kuelewa nini haswa kipo
mbele yetu,” alisema Mwenyekiti na kuongeza: “Tuache kwanza wananchi wapate elimu ya kutosha ili wajue nini
kinajadiliwa na hata kitapopitishwa wajue kuna faida gani wanapata.”
Akizungumza na Majaji hao, Mtikila alidai kuwa lengo la kufungua
kesi hiyo ni pamoja na kunyoosha mkondo wa sheria kwa sababu wapo
wanaovunja sheria na kupuuza kazi za Mahakama. Jopo hilo lilimshauri Mtikila kwamba kama ana nia ya kuendelea na
maombi mengine yaliyopo kwenye kesi hiyo aiondoe mahakamani na kwenda
kuandaa upya maombi yake yasiyokuwa na kipengele cha Muswada wa Mahakama
ya Kadhi.
Mtikila alikubaliana na ushauri wa jopo hilo liliondoa kesi iliyosajiliwa kwa namba 14, ya mwaka huu.
Akizungumza na NIPASHE nje ya Mahakama, Mtikila alisema baada ya
kuliondoa shauri hilo mahakamani anatarajia kuandaa maombi mapya dhidi
ya Waziri Mkuu, Pinda na wenzake ili waende waieleze mahakama kwa nini
waliandaa muswada huo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment