Social Icons

Pages

Thursday, April 02, 2015

ACT YAHIMIZA KURA YA HAPANA KWA KATIBA

Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira.
Chama cha ACT -Wazalendo, kimewataka Watanzania kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa kwa sababu imeleta mgawanyiko katika taifa kutokana na kupatikana kwa njia zisizo za kiuadilifu na mchakato wake kuendeshwa kibabe.
Kadhalika, kimesema katiba hiyo haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala ya mbalimbali, ikiwamo muundo wa serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais na uwiano wa muhimili wa dola.
Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira, alisema jana kwa  waandishi wa habari, kuwa: “Suala la Katiba, tumeamua kuwa tutaanza nalo mara ya kukamata dola, tutaanzia pale alipoishia Jaji Joseph Warioba, hii inatokana na ukweli kwamba mchakato wa uundaji wa Katiba mpya ulifanywa batili na hatua zilizofuatwa baada ya rasimu ya pili kukamilika.”
Anna, alisema azimio lingine la mkutano wa Kamati Kuu ni kumuagiza Katibu Mkuu wake, Samson Mwigamba, kutangaza nafasi ya kuwapata wajumbe watakaoingia kwenye kamati ya uadilifu ya chama taifa, mchakato ambao utaanzia ngazi za chini za chama.
Pia, kamati hiyo iliazimia kuanza ziara  katika mikoa 10 mara baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Pasaka, lengo likiwa ni kukitangaza chama, kutambulisha viongozi na kutangaza Azimio la Arusha lililohuishwa baada ya kupitishwa na vikao vya chama na kwamba kwa sasa linachapwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: