Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ametoa msaada
wa Sh. milioni tano kwa waathirika wa mafuriko katika kata ya Lamadi
Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa,
Raphael Chegeni, aliwasilisha msaada huo kwa niaba ya Lowassa. Chegeni alisema Lowassa ametoa msaada hguo baada ya kuguswa na janga hilo.
Chegeni alifafanua kuwa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa kitanunua mafuta ya kula, unga, mchele na sukari. Wakati huo huo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani
Mwanza, umetoa magodoro 50, mablanketi 70, kilo 500 za maharage na dawa
za binadamu vyote vikiwa na thamani ya Sh. 500,000.
Meneja wa NHIF mkoani Mwanza, Dk. Mathias Sweya, alikabidhi msaada
huo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya, Paul Mzindakaya, ambaye
pia ni Mkuu wa wilaya hiyo. Dk. Sweya alisema NHIF imeguswa na janga hilo na hivyo kuamua kutoa msaada huo kwa jamii.
Aidha, Taasisi ya Mkapa Foundation na Mamlaka ya Bima Kanda ya Ziwa (Tira), walitoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao. Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo, Mzindakaya aliwashukuru
wote walioguswa na janga hilo na kuamua kutoa misaada kwa waathirika.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoishi mabondeni kuhama ili kuepukana na majanga ya mafuriko mara kwa mara. Zaidi ya kaya 178 ziliathiriwa na mafuriko baada ya kunyesha mvua kubwa Jumamosi iliyopita.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment