
Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu, Salome Kaganda, 
amesema moja ya mambo ambayo walikabiliana nayo wakati wa sakata la 
akaunti ya Tegeta Escrow, ni kwa wanasiasa  kujitetea kwamba  kitendo 
cha kuomba fedha kwao ni jambo la kawaida, kwani kufanya hivyo wanakiuka
 maadili ya utumishi wa umma.
Jaji Kaganda alitoa kauli hiyo katika warsha ya wadau ya kujadili 
rasimu ya mwongozo wa maadili wa viongozi wa umma, iliyofanyika jana 
jijini Dar es Salaam. Warsha hiyo iliwashirikisha  viongozi na  watumishi wa umma, wawakilishi wa asasi za kiraia na wanasiasa.
Akifafanua, Jaji Kaganda alisema tabia ya ukosefu wa maadili ya 
umma imekuwa ikijirudiarudia katika maeneo mengi yakiwamo matumizi 
mabaya ya madaraka, vitendo vya rushwa, kuomba, kushawishi na kupata 
fedha katika mazingira yasiyo halali,  jambo ambalo liliwapa shida 
wakati wakishughulikia wahusika wa sakata la Escrow kutokana na 
wanasiasa wakati wanahojiwa kusema kuwa kwao kuomba fedha ni jambo la 
kawaida.
“Mwongozo huu pia umetaja vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya 
viongozi wa umma…matumizim mabaya ya madaraka, taarifa za serikali, 
vitendo vya rushwa, mgongano wa maslahi, kushindwa kutoa tamko la 
rasilimali na madeni, unyanyasaji wa kijinsia, kuomba, kupokea, 
kushawishi na kujipatia maslahi ya kifedha yasiyostahili..katika hili 
tulipata shida sana wakati wa suala la Escrow…wanasiaasa wakisema kwao 
kuomba fedha ni jambo la kawaida,” alisema jaji Kaganda.
Baadhi ya wanasiasa waliohusika na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya 
Shilingi bilioni 300 kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa 
Benki Kuu (BoT) na kuhojiwa na sekretarieti hiyo  ni pamoja na aliyekuwa
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka; 
Mbunge wa   Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa  Sengerema, 
William Ngeleja.
Hata hivyo, Chenge alikataa kuhojiwa na kuweka pingamizi mahakamani. Kufuatia sakata hilo, Ngeleja, aliondolewa katika nafasi ya 
uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala huku
 Chenge akiondolewa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti.
Kadhalika, Profesa Tibaijuka, Chenge na Ngeleja walisimamishwa 
ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
     CHANZO:
     NIPASHE
    
No comments:
Post a Comment