Mkurugenzi wa Takukuru, Edward Hosea
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula yuko
katika ziara ya kichama mkoani Dar es Salaam. Moja ya ajenda ya ziara
hiyo ni kukemea rushwa ndani ya chama hicho tawala. Kwa msisitizo
alitamka kuwa yeyote anayetafuta uongozi kwa kutumia fedha, kununua
wanachama ili apigiwe kura au apitishwe, akiona jina lake halikutoka
ajue limemezwa na kanuni na sheria za uchaguzi.
Hii siyo kauli ya kwanza kwa Mangula, kwani
Novemba 2012 akiwa kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wakati
wa sherehe zilizoandaliwa na CCM Mkoa kuwapongeza viongozi wapya,
alisema walioshinda katika chaguzi za chama hicho kwa rushwa wajiandae
kung’olewa ndani ya miezi sita.
Kauli hiyo iliamsha malumbano na wanasiasa wengine
wa upinzani, wakimtuhumu hana ubavu wa kupambana na wala rushwa ndani
ya CCM. Lakini naye kwa haraka aliwajibu kwa kutamba wanaombeza kuwa
hawezi kuitokomeza rushwa CCM wanasahau rekodi yake akiwa Katibu Mkuu wa
chama hicho.
Miezi sita aliyoitaja Mangula ilimalizika rasmi
Mei 2013, leo ni zaidi ya miaka miwili, hakuna aliyeng’olewa. Mangula
aliwalenga viongozi wa jumuiya za CCM za Wazazi, UWT na UVCCM, ambao
uchaguzi wake ulidaiwa kushamiri vitendo vya rushwa kutoka kwa makundi
ya urais, yaliyodaiwa kupanga safu zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Ni dhahiri suala la rushwa bado ni mfupa mgumu,
itakumbukwa kuwa Serikali iliwahi kupeleka bungeni marekebisho ya Sheria
ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kuongeza kipengele cha takrima katika
uchaguzi, kwamba mgombea anaweza kuwakirimu wafuasi wake. Sheria hiyo
iliyofurahiwa zaidi na wana-CCM iliongeza uhasama kwa wananchi na pia
kuzichukiza nchi wahisani na mwaka 2006 nchi hizo zilitishia kuipunguzia
Tanzania misaada kwa maelezo kwamba imeshindwa kurekebisha sheria ya
kukomesha rushwa.
Baada ya tishio hilo, Serikali ilifanya haraka
marekebisho ya sheria na kuunda chombo kipya kiitwacho Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) badala ya Taasisi ya
Kupambana na Rushwa (Takuru). Mwaka huohuo, Mahakama Kuu ilitangaza wazi
kuwa takrima ni rushwa.
Mahakama ilifikia uamuzi huo kwa kuwa vifungu
hivyo vinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.
Wakati wa sherehe za miaka 34 ya CCM, Rais Jakaya
Kikwete alisema CCM inalazimika kuachana na wanachama na viongozi mzigo
kwa mtindo wa kujivua gamba. Lakini tangu wakati huo suala la kujivua
gamba limekuwa gumu ndani ya CCM, ndiyo maana tunamshangaa Mangula
anapoibuka tena akidai kanuni na sheria zitawameza watakaotumia fedha
kununua uongozi.
Tunajiuliza CCM ndiyo iliyoshika Serikali na
katika kupambana na rushwa, kanuni na taratibu nyingi zilifanyiwa
mabadiliko na nyingine kutungwa. Mfano, mabadiliko ya Kanuni za Maadili
ya Viongozi na Watumishi, wakala nyingi za Serikali zilianzishwa
kupunguza urasimu na kuongeza uwazi, kama vile Tanroads na Ewura,
nyingine ziliimarishwa na kupewa uwezo zaidi, kama Takukuru.
Pamoja na yote hayo bado viongozi wetu wameendelea
kulalamika kuhusu kushamiri kwa rushwa, tunajiuliza kama hali ndiyo
hiyo nani atapambana na tatizo hilo, utekelezaji wa mipango yote hiyo
umekwama wapi. Tunaiomba CCM iisaidie Takukuru kukamata wala rushwa
inaowalalamikia kwa sababu inawajua.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment