
Dk Asha Rose Migiro alizaliwa Julai 9, 1956 katika
Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma. Migiro alianza masomo katika Shule ya
Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam mwaka 1963 hadi mwaka 1966. Akahamia
Shule ya Msingi Korogwe, Tanga na kuendelea na elimu ya msingi mwaka
1967–1969.
Baadaye akajiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne
katika Shule ya Sekondari Weruweru mkoani Kilimanjaro mwaka 1970 mpaka
1973 na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Korogwe mwaka
1974 -1975.
Migiro alikuwa mmoja wa wasichana waliofaulu
vizuri Korogwe Sekondari na alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) mwaka 1977 alichukua masomo ya sheria ambako alitunukiwa shahada
yake (LLB) mwaka 1980.
Baada ya kukamilisha shahada yake ya kwanza,
aliajiriwa UDSM kufundisha masomo ya sheria kama Mhadhiri Msaidizi.
Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili kabla ya kuendelea tena na masomo ya
juu ya sheria mwaka 1982–1984 hapohapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
akatunukiwa shahada ya uzamili (LLM).
Kati ya mwaka 1985–1988, alifundisha UDSM. Mwaka
1988 alikwenda Chuo Kikuu cha Konstanz, Ujerumani ambako alisoma na
kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya sheria mwaka 1992.
Dk Migiro alirejea Tanzania akiwa Mhadhiri Mwandamizi na aliendelea
kufundisha katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
hadi mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa.
Dk Migiro, akiwa UDSM kati ya mwaka 1992 – 1994
alikuwa Mkuu wa Idara ya Sheria za Katiba na Utawala. Kati ya mwaka 1994
– 1997 aliongoza Idara ya Sheria za Makosa ya Jinai (Idara zote zipo
katika Kitivo cha Sheria UDSM). Anaongea vizuri Kiingereza, Kifaransa na
Kijerumani na ni mke wa Profesa Cleophas Migiro na wana watoto wawili
wa kike.
Mbio za ubunge
Tofauti na wanasiasa wengi ambao hufikia ngazi za
juu za uongozi wa nchi kuanzia siasa katika nyadhifa za vyama vyao, Dk
Migiro amekuwa na historia tofauti kidogo. Yeye ameanza siasa za
kujijenga akitokea katika taaluma, akitazamwa na watu wengine kuwa ana
uwezo wa kulisaidia taifa. Hata hivyo, tofauti na wanasiasa wengi ambao
hupaswa kujisukuma wenyewe, yeye tunasema ‘alisukumwa.’
Mwaka 2000, ‘alisukumwa’ na Rais Benjamin Mkapa na
baadaye akateuliwa kuwa waziri kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Wanawake na Watoto. Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 2005 bila
kubadilishwa akisimamia mambo mengi ya kisera na kimiundombinu, bila
kusahau utekelezaji na upiganiaji wa haki za wanawake na watoto.
Wanasiasa wengi wanapoteuliwa kuingia bungeni
kipindi kimoja, kijacho utawaona wakipambana majimboni ili kujiimarisha
na kutosubiri kuteuliwa, kwa Migiro ilikuwa tofauti sana, hakwenda
kuchukua jimbo la mtu na hivyo hakuwa mgombea.
Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka
2005, alimteua Dk Migiro kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje, Januari
2006 na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa huo. Katika
kipindi cha mwaka mmoja tu, alifanya kazi nyingi za kimataifa
zilizomweka katika anga nyingine kisiasa.
Ilipotimu Januari 5, 2007, aliweka rekodi nyingine kubwa
kimataifa; aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban
Ki-moon kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akiwa mwanamke wa
pili kushika wadhifa huo baada ya Louise Fréchette, mwanadiplomasia wa
Canada aliyeongoza kuanzia Aprili 1997 hadi Aprili 2006. Migiro
alichukua nafasi iliyoachwa na George Mark Malloch Brown wa Uingereza
aliyeongoza kuanzia Aprili 2006 hadi Desemba 2006.
Migiro alishikilia wadhifa huo kwa miaka mitano,
akifanya kazi kubwa kimataifa hadi Julai 2012 alipopumzishwa na nafasi
yake kuchukuliwa na mwanadiplomasia wa Sweden, Jan Elliason.
Wakati anateuliwa kushikilia nafasi hii ya
kimataifa, Ban Ki-moon alimtaja kama “….kiongozi anayeheshimika ambaye
ameongoza maendeleo ya nchi masikini kwa miaka kadhaa kupitia huduma
yake iliyotukuka na ameonyesha ujuzi wa usimamizi wa kipekee na uzoefu
wa kutosha kwenye masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi…”
Januari mwaka 2013, Dk Migiro aliteuliwa kuwa Mkuu
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Desemba 2013 aliteuliwa kuwa
mbunge katika Bunge la Tanzania. Mwezi mmoja baadaye yaani Januari 2014
aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nafasi ambayo anatarajiwa
kuendelea nayo hadi Oktoba mwaka huu.
Mbio za urais
Dk Migiro hakuwahi kutamka hadharani kuwa
atagombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ila amekuwa
akipigiwa chapuo sana.
Alipotua uwanja wa ndege mwaka 2012 akitokea
Marekani, baada ya ‘kustaafu’ nafasi ya juu ya UN, waandishi wa habari
walimuuliza kama atagombea urais naye aliwajibu; “ Hivi sasa tunajua
Tanzania inaongozwa na Rais Kikwete hakuna tena mtu mwingine, hivyo si
vizuri kusema ninahitaji kugombea nafasi hiyo wakati muda bado, tuwe na
subira”.
Wachambuzi wengi wanamweka Migiro kwenye orodha ya
wateule ndani ya CCM kwa sababu ya haiba yake ambayo huenda wanasiasa
wengi wakongwe ndani ya chama hicho hawajaifikia. Uzoefu wake kitaifa na
kimataifa, taaluma na utulivu wake vinafanya aonekane kuwa anaweza
kuteuliwa.
Nguvu yake
Dk Migiro ni zaidi ya mwanamke. Kwanza, ni msomi
mahiri ambaye wanaume wengi wanakubali juhudi zake katika nyanja muhimu
kwenye dunia ya sasa. Katika dunia ya sasa, ukiwa mwanamke, tena msomi
unakuwa na nafasi ya kipekee ya kufanikiwa na kuungwa mkono kwa sababu
ya dhana kwamba wanawake wanapaswa kupewa nafasi. Jambo hili linambeba
Migiro.
Pili, ni mtu wa watu, tena wa kawaida sana.
Ukiongea na wanafunzi aliowafundisha UDSM katika kipindi kirefu
kilichopita, wanakueleza namna mama huyu alivyo na roho ya uwajibikaji
na huruma. Mambo haya yanamfanya awe tofauti na wanasiasa wengi ambao
hujawa kiburi na dharau baada ya kupewa nyadhifa fulani kubwa.
Uzoefu wake si jambo la kuchezea. Ni Watanzania
wachache sana na wanasiasa wa kuhesabu nchini ambao wana uzoefu alionao.
Ni mwana taaluma nguli akiwa amefanya tafiti juu ya masuala mengi,
wakati huohuo akiwa na uzoefu wa masuala ya kibunge kwa miaka takribani
minane; amekuwa na uzoefu wa utendaji wa serikali akishikilia dhamana
kubwa kwa karibu muongo mmoja; na zaidi ya yote ameshikia nafasi ya pili
kimamlaka katika chombo kinachoendesha dunia – UN. Huyu ni moto wa
kuotea mbali kwani sifa hizi zinambeba kwa namna yoyote ile.
Udhaifu wake
Migiro ni mpole sana. Kuna wanawake wengi sana
katika siasa za Tanzania ambao wana “roho ya kike” lakini yanapokuja
masuala magumu hubadilika na kuvaa “roho ya kiume” na kupambana nayo.
Migiro hana kaliba hiyo. Tanzania ilipo hivi sasa inahitaji rais
anayeweza kuwa mkali kila itakapohitajika na awe rafiki sana wa watu
wakati itakapoonekana ni muhimu kufanya hivyo.
Jambo la pili linaloweza kumhukumu ni utendaji
wake UN. Gazeti la “New York Times” la Marekani liliwahi kuandika kwamba
UN ilihitaji kuteua mwanamke katika nafasi ile aliyoshikilia kwa miaka
mitano, inawezekana kuwa alitafutwa mwanamke kwa sababu ya jinsia lakini
si kwa maana ya sifa.
Baadhi ya duru zinaonyesha kuwa Migiro alishindwa
kupambana na kasi ya majukumu ya UN, yakiwamo masuala ya kufanya uamuzi
wa haraka na kuusimamia, lakini pia kuongoza majopo ya wataalamu
wanaofanya tafiti wasioweza kuendeshwa kwa ubabaishaji. Mtandao wa Vox
Media unaripoti kwamba “vyanzo ndani ya UN vilieleza kuwa, utendaji
wake usioridhisha na kushindwa kuendana na mazingira yenye mtanzuko na
magumu ndivyo viliifanya UN isimwongezee mkataba mwingine”.
Mtandao huo unaendelea kusisitiza kuwa hata wakati
anapewa nafasi hiyo muhimu na UN ilitokana na sababu za ukaribu wa
Kikwete na Ban Ki-moon, ambao wamewahi kufanya kazi wote kwenye wizara
za mambo ya nje za nchi zao.
Vox Media imeendelea kueleza kuwa Migiro hakuwahi
kuwa mwanadiplomasia maarufu na alishindwa kumsaidia Ban Ki-moon kwa
sababu hakuwa anasikilizwa, hasa ikizingatiwa kwamba hata uteuzi wake
ulipingwa na baadhi ya wanadiplomasia mashuhuri.
Udhaifu mwingine mkubwa wa Migiro ni kusubiri
atafuniwe mambo kila mara. Tatizo lililo dhahiri kwake katika mbio hizi
za urais ni hiyo tabia yake ya kusubiri aambiwe na chama chake “anza
harakati, chukua fomu n.k”. Anataka aendelee kubebwa kama ilivyokuwa
katika nafasi zote alizoshikilia kisiasa – “kupewa”.
Pengine, alipaswa kujifunza kuwa yeye ni mwanamke
wa mfano katika nchi. Alipaswa kusimama kidete na jamii imjue kuwa yu
“mwanamke wa shoka”; uthubutu wa namna hiyo ungempa ujasiri wa kusimama
hata katika jimbo fulani muhimu na kuwaangusha wanaume au wanawake
wenzake. Migiro huyu angeweza kupanda ngazi na kuaminiwa zaidi kuliko
ilivyo sasa, “kuaminiwa kwa kubebwa”.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe
Dhana ya kuwapa wanawake nafasi inaweza kuwa
sababu kuu ya kupenya kwa Migiro kwenye chekecheo la CCM. Tukumbuke kuwa
huu ni wakati wa wanawake kuachiwa nafasi ambazo zimeshikiliwa na
wanaume kwa karne nenda rudi. Hii ni karata muhimu kwake.
Jambo jingine linaloweza kumvusha ni uzoefu wake
wa taaluma na uongozi wa juu wa CCM. Amewahi kuongoza idara ya mambo ya
nje ya chama chake na ukiachilia mbali uwaziri, taaluma yake na uzoefu
wa mambo vinambeba kufikiriwa kwenye kikaango.
Kwa upande mwingine Migiro ni mwanamke anayependa
kujiendeleza. Kitendo cha kutoka katika familia ya kawaida na kusoma
hadi chuo kikuu na kuwa daktari katika miongo kadhaa iliyopita si jambo
dogo.
Ni mwanamke anayeonekana kujiamini na anaweza kupigania ndoto zake hadi zikamilike.
Lakini, kama CCM inatafuta wagombea wasio na makundi na wanaoweza kuunganisha chama kwa dhana hiyo, Migiro ni mmoja wao.
Kutotumia muda kujijenga kumemfanya asiwe na
makundi ndani ya chama chake na hiyo ni faida kwake kwani anafanyiwa
tathmini kama mgombea “neutral”.
Pamoja na kuwa na miaka 59, Migiro anaonekana kuwa
mtu wa kizazi cha sasa kwa maana ya mitizamo yake, tabia zake na hata
marafiki zake. Nakumbuka wakati tuko Bunge la Katiba, ‘angenifuata na
kusalimiana nami kwa sababu ananisikia na kuniona kwenye siasa,
angeniuliza mambo mawili matatu na kucheka, tungegonga mikono kisha
akaenda zake.’ Huyu ndiye Migiro na anaweza kabisa kuvaa viatu na mawazo
ya vijana.
Nini kinaweza kumwangusha
Jambo la kwanza linaloweza kumwangusha katika
safari ya kuusaka ukuu wa nchi ni hofu za kijinsia. Vyama vyote vikubwa
vya siasa hapa nchini bado havijawaamini sana wanawake.
Ukiangalia hata kwenye nafasi za uongozi wa juu wa
vyama, ni Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR Mageuzi tu, labda na sasa
ACT Wazalendo, ndivyo vimethubutu kuwapa wanawake nafasi moja miongoni
mwa nafasi tano za juu. Ndani ya CCM ndiyo kabisa, kwa sasa si rahisi
mwanamke akapewa hata ukatibu mkuu wa chama, achilia mbali fursa ya
kugombea urais. Mwaka 1995 alijitokeza Rose Lugendo, lakini jina lake
lilikatwa mapema.
Pia, CCM ina hofu sana na vyama vya upinzani
hususan Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na ikipiga hesabu inaona
watangaza nia za urais walio tishio ndani ya Ukawa, wote ni wanaume, kwa
hiyo ikimleta mwanamke anaweza kushindwa uchaguzi wa kitaifa kabla ya
kura kupigwa kwa kuzingatia kuwa mitazamo ya Watanzania wengi bado
“inamhukumu mwanamke” na haijamwamini sana kushikilia nafasi muhimu
zaidi za maamuzi ya nchi.
Jambo la pili linaloweza kumwangusha ni kuwa na
ushawishi mdogo kwa makundi ndani ya CCM. Pamoja na kuonekana kama mtu
asiye na makundi, lakini haonekani kama anaweza kuyaunganisha makundi
yaliyojijenga na kujengeka na kusaka urais kwa uhasama.
Kama atapitishwa CCM inahofia jambo hilo na linaweza kuchukuliwa kama kitisho kwa chama na majibu yanaweza kuwa ni kumtosa.
Asipopitishwa (Mpango B)
Migiro hajaonyesha nia ya kugombea ndani ya CCM,
lakini ni ukweli ulio wazi kuwa yeye ni mmoja wa wanawake wachache na
wanaoheshimika ndani ya CCM. Moja ya mipango yake inaweza ikawa ni
kusubiri nafasi ya uteuzi na labda kupewa nafasi ya uwaziri tena ikiwa
chama chake kitashinda.
Mpango mwingine unaoweza kumfanya atoe mchango wake kwenye jamii
ya kimataifa ni kujihusisha na mambo ya kimataifa na usuluhishi wa
migogoro mbalimbali hasa barani Afrika. Atatumia uzoefu wake wa UN na
ule wa kuongoza wizara ya mambo ya nje kutimiza wajibu huu. Jambo
jingine analoweza kufanya ni kufundisha vyuo vikuu. Tanzania hivi sasa
ina vyuo binafsi lukuki na havina walimu madhubuti hasa kwa fani kama
sheria. Migiro anaweza kurudi darasani na akapumzika mbio za huku na
kule ili kuzalisha vijana watakaolisaidia taifa letu.
Hitimisho
Dk Migiro amefanya mambo mengi yanayoweza kumfanya
awe mwarobaini ndani ya CCM, lakini hajajijenga ndani ya chama na
amezungukwa na mazingira ya kuwa katika chama ambacho bado hakiwaamini
wanawake katika wadhifa mkubwa kama “kugombea urais”, achilia mbali hata
“ukatibu mkuu” wa chama. Itampasa kusubiri maamuzi magumu sana ya chama
chake kuona kama ndoto anayootewa ya urais inaweza kutimia.
Hata hivyo, uzoefu katika mambo mengi ya kitaifa
na kimataifa, usomi uliotukuka na ubobezi wa hali ya juu ukichanganya na
utulivu wake katika kufanya maamuzi vinamweka katika orodha ya watu
muhimu. Namtakia kila la heri katika safari yake.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment