Pages

Thursday, April 30, 2015

BAJETI YAWACHANGANYA WABUNGE


Wakati Serikali imetangaza mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi yake kwa mwaka 2015/16 yenye vipaumbele vinne, baadhi ya wabunge, akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu wameiponda wakisema haikuwashirikisha wadau katika uandaaji na kwamba haina kipya.
Tofauti na alivyoliambia gazeti la Mwananchi juzi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya alitaja moja ya vipaumbele hivyo vinne kuwa ni Uchaguzi Mkuu, ambao awali alisema haungekuwamo kwenye bajeti ya 2015/16 kwa kuwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zilishatengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika.
Vipaumbele vingine ni kuweka msukumo kwenye miradi ya umeme vijijini na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Lakini Dk Limbu alisema Serikali haikuwashirikisha wadau katika uandaaji wa bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, wala kamati yake kabla ya kuja na mapendekezo hayo.
“Sisemi kwamba kazi yao ni mbaya. Wamejifungia kule wakakamilisha kazi ndiyo wakaileta. Kwa mara ya kwanza mimi kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti nimeikuta hii ‘figure’ ya Sh22.4 trilioni humu, nataka nieleze masikitiko yangu,” alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ilipaswa kuwashirikisha ili kujaribu kupunguza mjadala mkali bungeni na kwenye kamati. Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo jana, Waziri Mkuya alisema Serikali imepanga kutumia Sh22.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2015/16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ya bajeti iliyopita iliyokuwa Sh19.8 trilioni.
Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh16.7 trilioni na matumizi ya maendeleo ni Sh5.7 trilioni, sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote.
Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh 14.8 trilioni sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh13.3 trilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani. Alisema mapato yasiyo ya kodi yatakuwa Sh949.2 bilioni na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh521.9 bilioni.
Aliongeza kuwa washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia Sh1.8 trilioni katika bajeti sawa na asilimia 8.4 ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15.
Mkuya alisema Serikali ilipanga kutumia Sh5 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, lakini hadi kufikia Machi, mwaka huu ilikuwa imetoa Sh2.4 trilioni tu.

Misaada na mikopo
Waziri Mkuya alisema washirika wa maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa kiasi cha Sh2.9 trilioni sawa na asilimia 14.8 ya bajeti lakini hadi kufikia Machi, ni Sh1.5 trilioni tu ndizo zilizopokewa ambazo ni sawa na asilimia 54 ya kiasi kilichoahidiwa.
Akiwasilisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/16, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Uhusiano na Uratibu, Dk Mary Nagu alisema Serikali itaongeza mtaji katika Benki ya Kilimo ili ikianza iweze kutoa mikopo kwa wakulima.
Alisema itaendelea kuboresha mazingira ya kibiashara na uwekezaji ili kuvutia sekta binafsi kuongeza kasi ya uwekezaji.
Wabunge walonga
Akizungumzia bajeti hiyo, Dk Limbu alihoji vigezo zilivyotumiwa kuongeza fedha kwenye bajeti kutoka Sh19.8 trilioni mwaka jana hadi Sh22.4 trilioni.
Alisema wakati ongezeko hilo ni sawa na Sh2.9 trilioni, utekelezaji wa bajeti iliyopo upo chini ya asilimia 80 na hivyo kutia shaka malengo ya kuongeza fedha huku bado kukiwa na changamoto ya kufikia kiwango cha bajeti kinachotakiwa.
“Katika taarifa ya waziri ya leo (jana) hadi Machi, kulikuwa na asilimia 38 tu ya fedha za maendeleo zilizotolewa, sasa mpaka robo mwaka unapotekeleza asilimia 38 hujafika hata asilimia 50, bado unaongeza Sh2.9 trilioni wakati fedha ya maendeleo pekee yake ni Sh2.4 trilioni. Watatueleza kwenye kamati vigezo walivyotumia,” alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina alisema kwa kuwa miradi mingi iliyokuwa imetengewa fedha kwenye bajeti inayomalizika haijafanikiwa kwa kiasi kilichokusudiwa, hakuna matumaini kwamba mipango ya sasa inaweza kufanikiwa.
“Hapa kuna mgogoro mkubwa wa kibajeti kwamba inawezekana tunapanga mipango mikubwa wakati uwezo wa kifedha hatuna. Lakini bado hatujaelezwa vizuri tukaelewa kwamba ni kwa nini licha ya mapato tunayokusanya ambayo ni zaidi ya asilimia 80, fedha zinazopelekwa kwenye maendeleo zipo chini ya asilimia 38,” alisema Mpina.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa jambo baya zaidi ni kuwa mpaka sasa mikoa yote nchini haijapelekewa fedha za matumizi mengineyo, jambo linalozua maswali kuwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa wapi.
“Siyo sahihi kusema kwamba safari hii tutakuwa makini na kwamba bajeti yetu itatekelezeka, kuna tatizo kubwa labda tutakapokuwa tunaendesha vikao vya kamati tutaelezwa na Serikali, labda kuna matumizi nje ya bajeti ya Serikali, tutaelezwa,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Hamis Kigwangalla alisema mapendekezo ya bajeti yanashtua kwa sababu fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinazidi kupungua kila mwaka ikilinganishwa na zilizowekezwa kwenye matumizi ya kawaida... “Nadhani haya si mambo mazuri katika uchumi wetu. Tunawekeza zaidi kwenye mambo ya kawaida, kulipa mishahara, gharama za safari, mafunzo lakini hatuwekezi kwenye miradi ya maendeleo. Ni upungufu mkubwa kwenye bajeti.”
Alisema kutokana na matatizo yaliyomo kwenye bajeti hiyo, hadhani kama inaweza kupitishwa na wabunge na kwamba kama itapitishwa itakuwa ni kwa sababu ya wabunge kuwaza Uchaguzi Mkuu.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema bajeti hiyo haina matumaini kwa wananchi kwa kuwa bado inategemea wafadhili ambao wamekuwa ‘wakiiangusha’ Serikali kila wakati.
“Serikali imetenga fedha, haikuzipata lakini imeongeza fedha kwenye bajeti. Mwaka jana, fedha za matumizi ya kawaida ilikuwa ni Sh13 trilioni, leo tunapeleka Sh19 trilioni halafu tunapunguza kwenye bajeti ya maendeleo,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment