Wakati Serikali imetangaza
mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi yake kwa mwaka 2015/16 yenye
vipaumbele vinne, baadhi ya wabunge, akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya
Bajeti, Dk Festus Limbu wameiponda wakisema haikuwashirikisha wadau
katika uandaaji na kwamba haina kipya.
Tofauti na alivyoliambia gazeti la Mwananchi juzi,
Waziri wa Fedha Saada Mkuya alitaja moja ya vipaumbele hivyo vinne kuwa
ni Uchaguzi Mkuu, ambao awali alisema haungekuwamo kwenye bajeti ya
2015/16 kwa kuwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zilishatengwa kwenye
bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika.
Vipaumbele vingine ni kuweka msukumo kwenye miradi ya umeme vijijini na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Lakini Dk Limbu alisema Serikali haikuwashirikisha
wadau katika uandaaji wa bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, wala kamati
yake kabla ya kuja na mapendekezo hayo.
“Sisemi kwamba kazi yao ni mbaya. Wamejifungia
kule wakakamilisha kazi ndiyo wakaileta. Kwa mara ya kwanza mimi kama
mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti nimeikuta hii ‘figure’ ya Sh22.4
trilioni humu, nataka nieleze masikitiko yangu,” alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ilipaswa kuwashirikisha ili kujaribu kupunguza mjadala mkali bungeni na kwenye kamati. Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo jana,
Waziri Mkuya alisema Serikali imepanga kutumia Sh22.4 trilioni katika
bajeti ya mwaka 2015/16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya
maendeleo ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ya bajeti iliyopita iliyokuwa
Sh19.8 trilioni.
Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh16.7
trilioni na matumizi ya maendeleo ni Sh5.7 trilioni, sawa na asilimia
25.9 ya bajeti yote.
Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa
Sh 14.8 trilioni sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Serikali
inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh13.3 trilioni sawa na
asilimia 90.1 ya mapato ya ndani. Alisema mapato yasiyo ya kodi yatakuwa Sh949.2 bilioni na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh521.9 bilioni.
Aliongeza kuwa washirika wa maendeleo wanatarajia
kuchangia Sh1.8 trilioni katika bajeti sawa na asilimia 8.4 ya bajeti
ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15.
Mkuya alisema Serikali ilipanga kutumia Sh5
trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika bajeti
iliyopita, lakini hadi kufikia Machi, mwaka huu ilikuwa imetoa Sh2.4
trilioni tu.
Misaada na mikopo
Waziri Mkuya alisema washirika wa maendeleo
waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa kiasi cha Sh2.9 trilioni sawa
na asilimia 14.8 ya bajeti lakini hadi kufikia Machi, ni Sh1.5 trilioni
tu ndizo zilizopokewa ambazo ni sawa na asilimia 54 ya kiasi
kilichoahidiwa.
Akiwasilisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka
2015/16, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Uhusiano na Uratibu, Dk Mary
Nagu alisema Serikali itaongeza mtaji katika Benki ya Kilimo ili ikianza
iweze kutoa mikopo kwa wakulima.
Alisema itaendelea kuboresha mazingira ya kibiashara na uwekezaji ili kuvutia sekta binafsi kuongeza kasi ya uwekezaji.
Wabunge walonga
Akizungumzia bajeti hiyo, Dk Limbu alihoji vigezo
zilivyotumiwa kuongeza fedha kwenye bajeti kutoka Sh19.8 trilioni mwaka
jana hadi Sh22.4 trilioni.
Alisema wakati ongezeko hilo ni sawa na Sh2.9
trilioni, utekelezaji wa bajeti iliyopo upo chini ya asilimia 80 na
hivyo kutia shaka malengo ya kuongeza fedha huku bado kukiwa na
changamoto ya kufikia kiwango cha bajeti kinachotakiwa.
“Katika taarifa ya waziri ya leo (jana) hadi
Machi, kulikuwa na asilimia 38 tu ya fedha za maendeleo zilizotolewa,
sasa mpaka robo mwaka unapotekeleza asilimia 38 hujafika hata asilimia
50, bado unaongeza Sh2.9 trilioni wakati fedha ya maendeleo pekee yake
ni Sh2.4 trilioni. Watatueleza kwenye kamati vigezo walivyotumia,”
alisema Dk Limbu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na
Biashara, Luhaga Mpina alisema kwa kuwa miradi mingi iliyokuwa
imetengewa fedha kwenye bajeti inayomalizika haijafanikiwa kwa kiasi
kilichokusudiwa, hakuna matumaini kwamba mipango ya sasa inaweza
kufanikiwa.
“Hapa kuna mgogoro mkubwa wa kibajeti kwamba
inawezekana tunapanga mipango mikubwa wakati uwezo wa kifedha hatuna.
Lakini bado hatujaelezwa vizuri tukaelewa kwamba ni kwa nini licha ya
mapato tunayokusanya ambayo ni zaidi ya asilimia 80, fedha zinazopelekwa
kwenye maendeleo zipo chini ya asilimia 38,” alisema Mpina.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa jambo baya zaidi ni
kuwa mpaka sasa mikoa yote nchini haijapelekewa fedha za matumizi
mengineyo, jambo linalozua maswali kuwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa
wapi.
“Siyo sahihi kusema kwamba safari hii tutakuwa
makini na kwamba bajeti yetu itatekelezeka, kuna tatizo kubwa labda
tutakapokuwa tunaendesha vikao vya kamati tutaelezwa na Serikali, labda
kuna matumizi nje ya bajeti ya Serikali, tutaelezwa,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Dk Hamis Kigwangalla alisema mapendekezo ya bajeti yanashtua
kwa sababu fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinazidi
kupungua kila mwaka ikilinganishwa na zilizowekezwa kwenye matumizi ya
kawaida... “Nadhani haya si mambo mazuri katika uchumi wetu. Tunawekeza
zaidi kwenye mambo ya kawaida, kulipa mishahara, gharama za safari,
mafunzo lakini hatuwekezi kwenye miradi ya maendeleo. Ni upungufu mkubwa
kwenye bajeti.”
Alisema kutokana na matatizo yaliyomo kwenye
bajeti hiyo, hadhani kama inaweza kupitishwa na wabunge na kwamba kama
itapitishwa itakuwa ni kwa sababu ya wabunge kuwaza Uchaguzi Mkuu.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema
bajeti hiyo haina matumaini kwa wananchi kwa kuwa bado inategemea
wafadhili ambao wamekuwa ‘wakiiangusha’ Serikali kila wakati.
“Serikali imetenga fedha, haikuzipata lakini
imeongeza fedha kwenye bajeti. Mwaka jana, fedha za matumizi ya kawaida
ilikuwa ni Sh13 trilioni, leo tunapeleka Sh19 trilioni halafu
tunapunguza kwenye bajeti ya maendeleo,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment