
Kitendo cha kutupiana mpira kati ya Ofisi ya Bunge, Tume ya Taifa ya 
Uchaguzi (NEC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu 
hatima ya Zitto Kabwe, kimeufanya ubunge wa mbunge huyo kuendelea 
kuning’inia huku mwenyewe akitazamiwa leo kueleza anachoita ‘maamuzi 
magumu’.
Kutupiana mpira kulijitokeza jana baada ya Spika 
wa Bunge, Anne Makinda kusema Bunge linasubiri taarifa rasmi ya 
kufukuzwa uanachama kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kutoka NEC, 
ambayo hata hivyo, nayo ilisema inasubiri taarifa kutoka Chadema huku 
chama hicho kikisema kinashughulikia kwanza kesi zinazowakabili 
wanachama wake wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu 
wake, Dk Willibrod Slaa.
Wakati Makinda akieleza hayo, taarifa kutoka kwa 
watu wa karibu wa mbunge Zitto zilieleza kuwa leo ataibuka bungeni kwa 
nia ya kuwaaga wabunge kama alivyoahidi wiki iliyopita. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Zitto alishindwa 
kukubali wala kukataa, lakini akathibitisha kuwa atahudhuria kikao cha 
Bunge leo.
Chadema ilimvua Zitto uanachama wiki iliyopita saa
 chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka 
chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa 
nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote. Alipata amri 
ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akifafanua suala hilo, Makinda alisema, “Unajua 
suala hili lilikuwa mahakamani, hivyo ni lazima tupewe taratibu zote za 
kimahakama. Kama kila kitu kikiwasilishwa moja wa moja uamuzi huo 
utatangazwa wazi. Unajua suala hili lipo wazi na sisi kama Bunge 
tunachokisubiri ni taarifa tu.”
Hata hivyo, alisema kwa muda uliobaki wa miezi 
saba kabla ya uchaguzi mkuu, haiwezekani ukafanyika uchaguzi mdogo 
katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, “Labda kama ingekuwa imebaki miezi 12 
au zaidi kabla ya uchaguzi mkuu, hapo ungeweza kufanyika uchaguzi 
mdogo.” Katika mkutano wake na waandishi wa habari 
alioufanya muda mfupi kabla ya kuwaaga wananchi wa jimbo lake Jumapili 
iliyopita, Zitto alisema hatima yake ya ubunge itajulikana wiki hii kama
 Bunge likipata taarifa za yeye kufukuzwa uanachama.
Alisema iwapo hatua hiyo itakamilika, ataeleza 
hatua ambazo atazichukua na kufafanua kuwa mpaka sasa hajapata barua ya 
wito wa kwenda kujitetea katika Kamati Kuu ya Chadema, hivyo mpaka sasa 
bado ni mwanachama wa Chadema. Alisema ataendelea kuwatumia Watanzania akiwa 
mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini na kusisitiza kuwa atatoa 
kauli iwapo atagombea ubunge katika jimbo lipi na kwa tiketi ya chama 
kipi cha siasa. Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba aliliambia 
gazeti hili jana kwa simu kwamba bado hawajapata taarifa ya maandishi ya
 kufukuzwa kwa Zitto, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.
Gazeti hili lilipowasiliana na Naibu Katibu Mkuu 
wa Chadema – Bara, John Mnyika kama chama hicho kimetoa taarifa za Zitto
 NEC kuhusu kuvuliwa kwake uanachama, alijibu kuwa viongozi wakuu wa 
chama hicho wanashughulikia kesi zinazowakabili wanachama wa chama hicho
 wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk 
Slaa. “Kipaumbele chetu leo (jana) ni mahakamani kutokana na ukubwa wa
 yanayoendelea katika tukio hili,” alisema Mnyika kupitia ofisa habari 
wa chama hicho, Tumaini Makene.
                
              
Chadema Kigoma wampania
Chadema Kigoma wampania
Katika hatua nyingine, Baraza la Vijana Chadema 
(Bavicha) Mkoa wa Kigoma, limesema litamshughulikia   Zitto Kabwe iwapo 
ataamua kugombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini badala ya Kigoma 
Kaskazini.
Akihutubia wakazi wa Kata ya Gungu mjini hapa 
juzi, mwenyekiti wa baraza hilo, Omary Gindi alisema wamejiandaa 
kushinda ubunge na kutetea nafasi ya kuongoza Halmashauri ya Kigoma 
Ujiji kama walivyofanya mwaka 2010.
Gindi alisema watambana baada ya Zitto kudai 
hatagombea kwenye jimbo alilokuwa anaongoza kupitia Chadema na badala 
yake amejipanga kugombea katika Jimbo la Kigoma Mjini kubadilisha na 
Peter Serukamba (CCM). “Zitto aje tu hapa Kigoma Mjini. Tutamuuliza 
aliwafanyia nini watu wa jimbo lake kiasi kwamba amemaliza kero zao na 
kuamua kuhama, vinginevyo tutawaeleza wananchi kwamba hafai na amekimbia
 kwao kwa sababu wananchi wamemwambia hawatamchagua tena kutokana na 
kushindwa kushirikiana na wapiga kura wake,” alisema Gindi.
Alisema watu wa Kigoma wanaipenda na kuiunga mkono
 Chadema kwa vile baadhi yao walifungwa jela, kupoteza mali, kujeruhiwa 
na kupata ulemavu na wengine kukosana na wake au waume zao, jambo 
lililowafanya kujiona ni sehemu ya chama hicho. Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shaaban Madede 
aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la 
wapiga kura.
“Lazima mhakikishe CCM inang’oka madarakani ili 
Chadema iweze kuongoza dola na kupigania masilahi ya watu, kwa vile 
sehemu nyingi kuna kero ya huduma mbovu za elimu, afya, maji na 
miundombinu ya barabara vijijini, suluhisho pekee ni kuiondoa CCM 
madarakani,” alisema Madede.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment