Wakati Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema hawezi 
kumtangaza Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwa siyo mbunge 
hadi atakapopata barua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Katibu Mkuu 
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, 
amesema bado hawajaandika barua kuiarifu Nec, kwa kuwa hilo siyo jambo 
kubwa ambalo chama kinapaswa kuhangaika nalo kwa sasa.
Spika Makinda aliwaambia waandishi wa habari nje ya viwanja vya 
Bunge mjini Dodoma jana kuwa ofisi yake haiwezi kufanyia kazi taarifa za
 kwenye vyombo vya habari, badala yake inasubiri taarifa za kiofisi 
kutoka Nec. “Hatuwezi kutangaza sasa kwa sababu hatujapata barua. Tumesikia 
kwenye vyombo vya habari tu. Kwa hiyo hadi hapo tutakapopata barua ya 
Nec ndipo tutakapotangaza,” alisema Spika Makinda.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, chama kikimvua mbunge uanachama anapoteza ubunge wake.
LISSU: SINA TAARIFA
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema hana taarifa 
 kama barua ya taarifa ya kumvua Zitto uanachama imekwishaandikwa kwa 
Nec au la kwa kuwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho ndiyo inahusika 
kuiandika.
DK. SLAA: HATUHANGAIKII ZITTO KWA SASA
Dk. Slaa alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema hatua ya kuandika 
barua hiyo itafuatia baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama kuitishwa na
 kufanyika. Hata hivyo, alisema suala la kuitisha kikao hicho linahitaji
 mchakato na kwamba hivi sasa kuna vitu vikubwa na vyenye athari kubwa 
kwa umma na siyo suala la uanachama wa Zitto ndani ya Chadema.
Alitaja vitu ambavyo Chama kinahangaika navyo kwa sasa kuwa ni pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura. “Sidhani kama waandishi wa habari mnahangaika nalo hilo, kama 
mnavyohangaika na suala hilo la uanachama wa Zitto,” alisema Dk. Slaa.
Kitu kingine ambacho alikitaja kuwa ni katika vitu wanavyohangaika 
navyo kwa sasa kuwa ni mamilioni ya shilingi ‘yanayoteketea’ kwa ajili 
ya kuandaa sherehe za ‘Wiki ya Maji.’ “Hatujaandika hiyo barua, tutaandika ratiba yetu ikituruhusu,” alisema Dk. Slaa.
Zitto alitangazwa kupoteza uanachama katika chama hicho wiki 
iliyopita baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam 
kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Chadema iliyokuwa ikihoji uhalali wa 
uanachama wake ndani ya chama hicho.
Baada ya hukumu hiyo ya Mahakama, Lissu alitangaza kuvuliwa rasmi uanachama wa Chadema. Lissu alisema Katiba ya Chadema inaeleza wazi kwamba endapo 
mwanachama yeyote atakishtaki chama hicho mahakamani na iwapo 
atashindwa, atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye Chama.
Hata hivyo, Zitto anasema kuwa yeye bado ni Mbunge na kwamba 
ataendelea kufanya kazi za ubunge ikiwamo kutekeleza majukumu ya 
Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
CHANZO:
     NIPASHE
    
No comments:
Post a Comment