
Rais Jakaya Kikwete, amelitaka Jeshi la Polisi
kuacha kutumia nguvu kubwa katika kukamatwa wahalifu, badala yake
kuweka mbele suala la haki za binadamu.
Rais alitoa angalizo hilo jana jijini Dar es Salaam katika Chuo
Kikuu cha Polisi, wakati wa hafla ya kuwapandisha vyeo askari 290 wa
Zanzibar na Bara waliomaliza mafunzo ya miezi sita. “Ipo haja ya kutumia mbinu mbalimbali katika kuwakamatwa watuhumiwa
kuliko matumizi ya nguvu kubwa, jitahidini sana kutumia nguvu kiasi ili
kuhakikisha hamvunji haki za binadamu,” alisema.
Rais Kikwete aliwataka polisi kujenga mazingira rafiki na wananchi
ili kurahisisha utendaji kazi ikiwamo kukabiliana na uhalifu nchini kwa
kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi. Rais Kikwete pia alisema wizi wa mtandaoni ni tatizo kubwa na
zinahitajika nguvu za ziada kupambana nalo na polisi wanapaswa kujipanga
kikamilifu na kwamba kwa sasa kuna matumizi mabaya ya mitandao ya
kijamii ambayo inatumika kutukana, kukashfu watu jambo ambalo ni kinyume
cha sheria.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya wahusika wote wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,” alisema. Aidha, alisema mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria
mkononi yameongezeka kutoka 2,075 mwaka 2005 hadi 3,775 mwaka 2015, hasa
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo yameliabisha Taifa na
kwamba zinahitajika jitihada kuyamaliza.
Awali, Mkuu wa Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, alimuomba Rais
kuangalia uwezekano wa kuongeza vifaa vya kisasa kwa jeshi hilo ili
liweze kutekeleza majukumu yake vizuri hasa kwa kipindi hiki ambako
Taifa litashiriki kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa na uchaguzi
mkuu Oktoba mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment