
Wakati Serikali ikijiandaa kuwasilisha muswada wa
Mahakama ya Kadhi katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajia kuanza leo,
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila
amefungua kesi ya madai Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam,
akipinga hatua hiyo.
Mtikila anapinga kuanzishwa Mahakama ya Kadhi, kwamba ni kinyume cha Katiba ya nchi. Kadhalika, Mtikila ameiomba mahakama itoe amri kwamba wale walio
kwenye mamlaka ya Serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu; Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
na wenzao watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka
mitano endapo watashindwa kujieleza.
Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14
ya mwaka huu, ameomba Mahakama itoe amri vigogo hao kufungwa kifungo
hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi. Katika hati hiyo, Mtikila pia anaiomba, mahakama itoe amri kwamba
Mahakama ya Kadhi na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), zitangazwe
kuwa ni haramu nchini.
Pamoja na mambo mengine, Mchungaji Mtikila anadai kuwa hatua
serikali kuandaa muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo
cha Bunge kukubali badala ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa
na wale walioupeleka muswada huo.
Anadai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya
viongozi hao. “Viapo ambavyo Pinda na wenzake waliapa wakati wa kushika
madaraka ya umma vinakiuka ibara ya 19 ya katiba ya nchi inaosisitiza
kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kwamba
uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya
nchi,” anaeleza katika madai yake.
Hati hiyo inaeleeza kuwa mamlaka ambazo zimepigwa marufuka na
Katiba kujiingiza, kujihusisha au kuchezea mambo kama ya kadhi na
uanachama wa taasisi za kidini au uanachama wa uislamu ni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu au viongozi wote wa kiserikali ambao baada
ya kula viapo hujifunga kulinda katiba ya nchi na si vingevyo.
Mtikila anaendelea kueleza kupitia hati hiyo kwamba muswaada wa
mahakama ya kadhi na uanachama wa OIC havikubaliki katika ardhi ya
Tanzania kwa sababu zinabagua na ni ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Alieleza kuwa sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo ni kwa ajili ya
kuilinda katiba ya nchi kwamba ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania, inasema kwamba kila mtu ana haki kwa mujibu wa
taratibu zilizoanishwa na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la
kuhakikisha kwamba Katiba ya nchi inalindwa.
Alidai kuwa ametumia haki hiyo kufungua kesi hiyo akiitaka mahakama
itoe adhabu kwa mamlaka za nchi zilizochezea Katiba na wengine. Mtikila anaiomba Mahakama kumwamuru walalamikiwa kulipa gharama zote za kesi pamoja na amri nyingine itakayoona zinafaa.
KUTIKISA BUNGE
Wakati Mkutano wa 19 wa Bunge ukianza leo, baadhi ya wabunge
wameeleza kuwa mambo makuu matatu yanatarajia kulitikisa Bunge hilo
likiwamo muswada wa Mahakama ya Kadhi iwapo utawasilishwa na kwamba
busara na hekima visipotumika litaleta mpasuko mkubwa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE mjini Dodoma, wabunge
hao walisema mbali na mahakama hiyo, mambo mengine yanayoweza kuibua
mvutano bungeni ni mchakato wa kura ya maoni kwa ajili ya katiba
inayopendekezwa na mabehewa feki yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL).
Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, alisema kama muswada wa
Mahakama ya Kadhi utapelekwa bungeni utaleta mvutano mkali na kwamba
kinachohitajika ni hekima itumike ili kufikia muafaka. “Suala la Mahakama ya Kadhi bila shaka likiletwa bungeni litakuwa
moto sana kwa sababu masikio ya wananchi ni kutaka kusikia nini
kitaamuliwa katika suala hili,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema
serikali inatakiwa kuliangalia suala la Mahakama ya Kadhi kwa undani
zaidi kabla ya kulifikisha bungeni. Kafulila alisema kinachotakiwa kufanyika kwanza ni pande zote
zinazovutana katika suala hilo na serikali ichukue hatua kusuluhisha ili
ziafikiane kabla ya kukimbilia kulipeleka bungeni.
Alisema suala lingine ambalo wabunge watataka kupata majibu kutoka serikalini ni ununuzi wa mabehewa feki yaliyonunuliwa na TRL. “Tunasikia kuna tume iliundwa kuchunguza suala hili, lakini hadi
sasa majibu ya tume hiyo bado hayajawekwa wazi, tutataka kujua kwa nini
suala hilo limekuwa hivi,” alisema Kafulila.
Kuhusu kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa, alisema
inasikitisha kuona fedha za umma zinapotea bure kufanya maandalizi
wakati inafahamika kuwa suala hilo kamwe haliwezi kufanyika kutokana na
muda uliobaki kuwa mfupi. Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, alisema serikali isifanye mchezo katika suala la Mahakama ya Kadhi.
“Tangu uhuru serikali iliweka wazi kuwa haina dini, sasa suala la
kuleta muswada wa Mahakama ya Kadhi ni kutaka kuondoa amani iliyopo
katika nchi,” alisema. Alisema serikali isifanye dhihaka katika suala hilo na kuwa
inachotakiwa kufanya ni kuwaeleza ukweli Waislamu na Wakristo kwamba
suala hili haliwezekani kuliko kuwahadaa, hali inayoweza kuleta
machafuko nchini.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Bunge, Propers Minja, akizungumza na
NIPASHE, alisema katika ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge kuhusiana
na mambo yatakayofanyika katika mkutano huo suala la Mahakama ya Kadhi
halimo. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa, mkutano huo utakuwa mahsusi kwa ajili ya
kushughulikia miswada ya sheria.
Imeeleza kuwa miswada ya sheria sita itawasilishwa kwa mara ya kwanza na 15 kwa mara ya pili. Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliviambia vyombo vya
habari kuwa muswada wa Mahakama ya Kadhi utawasilishwa katika Mkutano wa
19, akisema hatua hiyo imechukuliwa na serikali baada ya kukutana na
wadau wote.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment