Social Icons

Pages

Friday, March 13, 2015

MAMBO MUHIMU KUTATUA TATIZO LA NGUVU ZA KIUME


Baada ya kuona makala zilizoeleza sababu mbalimbali zinazosababisha matatizo ya nguvu za kiume, sasa tuwe pamoja kwa nguvu zote katika kipengele muhimu kinachohusu suluhisho la matatizo ya nguvu za kiume.
Kikubwa unachotakiwa kufanya ili kuweza kupata msaada wa tatizo hili ni kuwa tayari kuweka wazi tatizo lako kwa watoa huduma za afya wa tiba za binadamu, na sio kwa watoa huduma wasiotambulika. Uzoefu unaonyesha wanaume wengi wenye tatizo hili huenda kwa watu wababaishaji wanaofanya ujanja ili kupata fedha.
Ikumbukwe kuwa kuficha tatizo lako na kuendelea kusikiliza maneno ya vijiweni kwa marafiki ambao hawana uelewa na mambo haya kunazidi kukuchanganya na kukuchelewesha katika kupata matibabu sahihi, sehemu sahihi na kwa wakati muafaka. Ni vyema kutokurupuka na kuhangaika kwa matabibu ambao ni matapeli wanaotaka kutumia matatizo yako ya nguvu za kiume kama mtaji wao wa kujipatia fedha.
Wagonjwa wengi huwa na aibu kufika katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo hilo wakihofia kunyanyapaliwa, lakini jambo hilo halipo kwa wataalamu wenye taaluma ya tiba za binadamu. Kumbuka kuwa si wewe pekee uliye na tatizo hilo, ni mamilioni ya watu duniani kote wana tatizo hilo hivyo unatakiwa kujiamini na kujipa moyo kuwa tatizo hili linatatulika.
Hata kama ikitokea kuwa tatizo lako linaweza lisitatulike ni vizuri ukakubaliana na hali hiyo, tambua kuwa kukosa nguvu za kiume si mwisho wa maisha yako. Kuna mambo ya maana na mazuri kwa maendeleo ya maisha yako ya baadaye unayoweza kuyafanya ili kusukuma maisha yako.
Kuwapo kwa matangazo mengi mtaani ya dawa za kuongeza nguvu za kiume hakumaanishi kuwa zinaweza kutatua tatizo lako, hiyo ni biashara ya wajanja mitaani.
Unaweza ukawa unatumia dawa hizo na kupata nafuu na kudhani umepona, lakini kumbe ukawa unaudhuru mwili wako pasipo kujua.
Dawa hizo zisizothibitishwa wala kupendekezwa kama ni salama na Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA), zipo kila mahali mitaani na wengi hujikuta wakinunua na kuzitumia kiholela. Tayari imeishawahi kuripotiwa kupoteza maisha baada ya kunywa dawa hizo kiholela pasipo kuzingatia ushauri wa wataalamu wa tiba za binadamu.
Miaka ya nyuma tatizo hili lilikuwa linaonekana kujitokeza zaidi kwa wanaume wenye umri kati ya miaka 40 na kuendelea. Lakini katika miaka ya siku hizi hata vijana wa kati ya umri wa miaka 20 na 30 wanajikuta wanapatwa na tatizo hilo. Tatizo la nguvu za kiume linaweza kutibiwa au likapunguzwa makali kwa matibabu mbalimbali baada ya kufanyiwa uchunguzi yakinifu.
Yapo matatizo ya nguvu ya kiume ambayo hujikuta hayatatuliki kwa njia yoyote hivyo mtu mwenye tatizo hilo huwa ni ulemavu wa kudumu. Kabla ya kufika huko ni vizuri ukatambua kuwa yapo matibabu salama ambayo unaweza kuyafanya kuimarisha hali ya tendo kabla ya kumfikia daktari.
Mazoezi ni moja ya kitu muhimu kwa mtu mwenye tatizo hili kwani humsaidia mtu kuwa imara na kuwa na ufanisi kwa mwili wake. Yawezekana umekua mtu mzima lakini kufanya mazoezi mepesi ya kutembea yanasaidia. Unene uliopitiliza na mrundikano wa mafuta mwilini huweza kupunguza ufanisi wa homoni ya kiume. Homoni ya kiume ndio inahusika kwa wanaume kuweza kuwa na nguvu hizo.
Unene ndio chanzo cha kupata maradhi ikiwamo kisukari, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na shinikizo la damu. Maradhi haya ndio yanayoharibu mishipa ya damu na mishipa ya fahamu ndio chanzo kikuu cha kupungukiwa nguvu za kiume.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: