Tundu Lisu
Mchakato wa Katiba Mpya, hatua ya Kura ya Maoni umegubikwa na wingu zito kutokana na kuibuka utata na ukiukwaji wa sheria.
Wakati hali ikiwa hivyo, jana Ofisi ya Rais, Ikulu
iliibuka na kutoa ufafanuzi kuwa Rais Jakaya Kikwete hajakiuka Sheria
ya Kura ya Maoni kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi
karibuni. Juzi, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema kuna mwingiliano unaoleta
mkanganyiko katika mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura na Sheria
ya Kura ya Maoni.
Jaji Warioba alisema sheria inaweka utaratibu
maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao hautaendana na ratiba ya
uandikishwaji katika daftari hilo.
Alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya mwaka 2014
inasema wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya maoni kwa miezi
miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi sasa, hakuna ratiba
inayoeleweka, jambo ambalo alisema linaleta mwingiliano. “Hii ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza
kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na
Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura
itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa
zimepamba moto,” alisema.
Mkanganyiko huo umeibua maswali kutoka kwa
wanasiasa, wanasheria na wanaharakati wakisema hali hiyo inaweza
kuathiri kura ya maoni ambayo imepangwa kufanyika Aprili 30. Kwa upande mwingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema),
John Mnyika amewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ili ijadiliwe na kutoa maazimio kutokana na
kutokuwapo uwezekano wa kufanyika kura ya maoni Aprili 30.
Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory
Rweyemamu alisema katika mchakato huo, Rais Kikwete alifuata taratibu
zote zilizopo katika sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kutangaza katika
Gazeti la Serikali tarehe ya kuanza kwa upigaji wa kura hiyo. “Sheria inasema Rais atatangaza tarehe hiyo wiki
mbili baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa na alitekeleza hilo na
baadaye alieleza jinsi ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
itakavyosimamia suala hilo,” alisema.
Katika hotuba yake kwa wazee wa Dodoma Novemba
mwaka jana, Rais Kikwete alisema, “Ninaomba Watanzania wenzangu
tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri
lini kura ya maoni itapigwa, lini kampeni zitafanyika na lini wadau
watatoa elimu, naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna
ugomvi,” alisema Rais Kikwete. Alisema licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku
60 kabla ya kura za maoni, kwa mamlaka yake ya kiuongozi, kura na
kampeni vitafanyika ndani ya siku 30 tu. “Kampeni zitaanza Machi 30 na kumalizika Aprili 29
ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura ya maoni. Muda huo ndiyo
utakuwa wa kufanya hivyo,” alisema Rais Kikwete.
Hoja ya Mnyika
Mbunge huyo wa Ubungo alisema mpaka sasa Nec
ilitakiwa iwe imetangaza ratiba ya uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapigakura lakini haijafanya hivyo, pia Sheria ya Kura ya Maoni inasema
kabla ya kufanyika kwa kura hiyo kutakuwa na miezi miwili ya kutoa elimu
ambayo haitatosha. “Hakuna haja ya kuuharakisha mchakato huu kwani
unaweza kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu, unajua baada ya mjadala, Bunge
litakuja na maazimio ambayo yatakuwa suluhisho la mchakato huu
unaoharakishwa na chama tawala.”
Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
(Bara) alisema; “Hata Rais Kikwete anatakiwa kutengua kauli yake kuwa
kura ya maoni itafanyika Aprili 30 kwani hali ilivyo hakuna uwezekano wa
kufanyika.” Akifafanua baadaye, Mnyika alisema anazo taarifa
za ndani ya Nec kuwa vifaa vinavyotakiwa havijakamilika na Serikali
haijatoa fedha za kutosha na ndiyo sababu haijatangaza ratiba ya
uboreshaji daftari. Alisema kwa muda uliotangazwa kati ya Februari 15
na Machi 15 kufanya uboreshaji huo, hauwezekani kwa kuwa hakutakuwa na
muda wa kuhakiki daftari hilo kabla ya kura ya maoni. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Julius Malaba alipoulizwa alisema atazungumzia suala hilo leo.
Msimamo wa Makamba
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba akizungumzia suala hilo alisema; “Kama
tukijipanga vizuri kwa Tume na Serikali tunaweza kufanikiwa na hakuna
sababu ya kuharakisha kitu.
Katiba itapata uhalali kama mchakato wa kuipitisha utakuwa halali.”
Wanasheria waponda
CHANZO: MWANANCHIWanasheria waponda
Wanasheria mbalimbali wamesema Sheria ya Kura ya
Maoni 2013, ina upungufu mkubwa na inaweza kuathiri Wazanzibari wengi
kutoshiriki katika upigaji kura ya maoni. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema
miongoni mwa udhaifu wa sheria ni pamoja na mwingiliano wa Sheria ya
Kura ya Maoni ya 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni ya 2010 ya Zanzibar.
Alisema katika utaratibu wa kupatikana wapigakura, kila upande wa Muungano utatumia daftari lake kuwasajili. “Kwa upande wa Bara kuna daftari linaloandaliwa
lakini kwa upande wa sheria ya kura ya Zanzibar ya 2010, ili Mzanzibari
atambuliwe na kusajiliwa kwenye daftari la wapigakura ni lazima awe ni
mkazi aliyeishi Zanzibar kwa miaka isiyopungua mitatu,” alisema na
kuongeza:
“Kutokana na sheria hiyo, kuna Wazanzibari wengi
ambao wanaishi Bara kwa muda mrefu ambao hawatakuwa na sifa za
kuandikishwa kwenye daftari hilo. Nilitoa hoja hiyo bungeni lakini
wabunge wa CCM walikataa kwa kuhofia Wazanzibari wakipata nafasi ya
kuandikishwa, wataikataa Katiba hiyo.” Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
Deus Kibamba alisema mbali ya udhaifu huo alioutaja Lissu, mpaka sasa
hakuna dalili zozote za kufanyika kura ya maoni kutokana na muda
uliobakia.
Alisema katika tathmini yake, hatua zote za
maandalizi ya tukio hilo zitakamilika Mei, kinyume na tarehe iliyopangwa
na Serikali. “Mpaka sasa haijulikani daftari kama litakamilika
kutokana na muda uliopangwa na ukosefu wa fedha kwa Tume, Pili hatua ya
kampeni na maandalizi mengine yanaweza kukamilika Mei,” alisema Kibamba. Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Nec haitaweza kukamilisha uandikishaji kabla ya Aprili 30.
“Tulikutana kwenye kikao cha TDC ambacho
kilihusisha viongozi wote wa vyama na Jaji Lubuva alikuwapo, aliahidi
kutimiza ahadi hiyo lakini mpaka sasa hajapata fedha za kununulia vifaa
vingine vilivyobakia,” alisema Nyambabe. Mashine za BVR zinazohitajika ni 7,750 na
zilizopatikana ni 250 tu, vituo vya kuandikishia viko 40,500 nchi nzima
na Watanzania wanaotarajiwa ni milioni 23, kwa hivyo hakuna uwezekano wa
kufanikiwa shughuli hiyo kwa mwaka huu.”

No comments:
Post a Comment