Social Icons

Pages

Wednesday, January 21, 2015

PAC YAITAKA TRA KUFIKISHA MAPATO YA 25% YA GDP

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac), Zitto Kabwe.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafikia asilimia 20 hadi 25 ya Pato la Taifa.
Kadhalika, imetaka kuharakishwa utekelezaji wa sheria ya ongezeko la Thamani (VAT), ili kukabiliana na ongezeko la misamaha ya kodi ambayo inaendelea kupaa na kwa mwezi Novemba, mwaka jana ilikuwa asilimia 41 ya mapato yaliyokusanywa. Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alitoa maelekezo hayo baada ya kuhojiana na TRA kwa siku mbili mfululizo katika ripoti zao mbalimbali walizowasilisha mbele ya kamati na utekelezaji wa maagizo ya Kamati kipindi kilichopita.
Alisema wabunge walishasema sheria inapopelekwa Bunge na kupitishwa ni lazima sheria zake ziwe tayari na kwamba kuchelewa kwa kanuni kumefanya isitangazwe kwenye gazeti la serikali (GN), ili ianze kutumika. “Misamaha ya kodi imechangia ukwepaji kodi kwa makampuni makubwa, juhudi zifanyike kupunguza misamaha hii, pia ipo haja ya kudhibiti misamaha hii,” alisema.
Zitto aliitaka TRA kuhakikisha kila ripoti yao inaonyesha misamaha ya kodi iliyotolewa kila eneo na wahusika wake, ili wananchi wajue VAT ni kiasi gani na serikali isipotoa misamaha ni kiasi gani kinapatikana. “Tukiongeza makusanyo na kuziba mianya tutaacha tabia ya kuwapigia magoti wafadhili, siyo kuwa na misamaha mingi huku fedha inahitajika,” alibainisha Zitto.
Kamati hiyo imetaka TRA kushirikiana na Mamlaka ya Bandari (TPA), kuhakikisha ‘flow meter’ zinafungwa, ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu kutoka Bandari ya Kenya na Daban Afrika Kusini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: