
Wasomi na
wananchi kadhaa jana walizungumzia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wengi wakihoji sababu za kumhamisha
Dk Harrison Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Rais alifanya mabadiliko kwenye baraza hilo baada
ya mawaziri wawili kuanguka kutokana na kashfa ya uchotwaji takriban
Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow. Ikiwa imesalia miezi isiyozidi sita kabla ya
Baraza la Mawaziri kuvunjwa na akitakiwa kujaza nafasi mbili zilizoachwa
wazi na Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Wizara ya Nishati na Madini
na Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko 13, yakihusisha
mawaziri wanane na manaibu watano.
Miongoni mwa mabadiliko hayo manane ya mawaziri,
ni uhamisho wa Dk Mwakyembe kutoka Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki huku
Samuel Sitta, ambaye aliwahi kumwelezea mbunge huyo wa Kyela kuwa ni
mmoja wa “marafiki wa kweli”, akihama kutoka Wizara ya Afrika Mashariki
kwenda Uchukuzi.
Watu wengi walioongea na gazeti hili, walisema
hakukuwa na haja ya kumhamisha Dk Mwakyembe kutokana na kazi nzuri
ambayo ameshaifanya kwenye wizara hiyo, ambayo ina tatizo kubwa la
usafiri wa reli, kuyumba kwa Shirika la Ndege (ATCL) na utendaji mbovu
kwenye bandari, mambo ambayo Dk Mwakyembe alionekana kuyashughulikia kwa
nguvu zote.
Sitta, mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki,
alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, pia aliwahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa
Kituo cha Uwekezaji (TIC). “Tulikuwa tunaziona jitihada za Dk Mwakyembe,”
alisema mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Frank
Tily. “Na kuhamishwa kwake kunamaanisha kuwa mambo yote yaliyokuwa
yanaendelea yatatakiwa kuanza upya. Nashindwa kuelewa ni kwa nini waziri
huyu amebadilishwa… ingekuwa bora zaidi kama angeachwa.”
Dk Frank Tily alisema kuwa kutokana na haja ya
kuongeza mawaziri ili kuziba nafasi mbili zilizoachwa wazi, hakukuwa na
haja ya kuwabadilisha wale waliofanya vizuri katika wizara zao.
Aliongeza kuwa nafasi ya uwaziri isiwe inajazwa
bila ya sababu za msingi, bali ifanywe tu endapo kuna haja kweli ya
kufanya mabadiliko na akasisitiza kuwa “wizara ya uchukuzi haikuwa na
sababu za kubadilishiwa waziri.” Naye mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Samwel
Chacha alisema kuwa, mabadiliko hayo yatakuwa na athari japo zinaweza
zisionekane kwa muda mfupi.
“Mwakyembe alikuwa na mipango ambayo ilianza
kuonekana na kudhihirisha uzalendo katika Wizara ya Uchukuzi. Kama
angeachwa aendelee nayo, kungekuwa na mabadiliko ambayo
yangetutambulisha Watanzania kwa kuwa na vitu vyetu kwa manufaa ya nchi
nzima,” alisema Chacha.
Ofisa Mikopo wa Benki ya NMB, Tito Mwanjala
alisema mabadiliko yaliyofanywa, yamekosa mwonekano mpya kutokana na
wabunge wengi kukosa sifa zinazotumika kuwapata mawaziri hao.
CHANZO: MWANANCHI
“Baada ya Bunge kupitisha maazimio, Rais hakuwa na jinsi zaidi
ya kutekeleza. Sura zimeendelea kuwa zile zile kutokana na kukosekana
kwa watu wenye sifa kwa sababu waziri lazima awe mbunge ambaye anatoka
chama tawala. Nadhani Rais atakuwa ametumia muda mwingi kuwapata
mawaziri wapya aliowaingiza katika baraza lake,” alisema Mwanjala. Aliongeza kuwa, mabadiliko yaliyofanyika katika
Wizara za Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Uchukuzi, yanaweza yakawa
na athari za kiutendaji kwani “viatu vya Mwakyembe vinaweza visimwenee
Sitta” kutokana na muda mfupi uliobaki kwa waziri huyo kuonyesha tofauti
iliyofanywa kwa muda mrefu na mtangulizi wake.
Hata hivyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Alhaji Musa Salum alikuwa na maoni tofauti kwa kueleza kuwa, mabadiliko
hayo ni sahihi na kwamba anaamini kutakuwa na ufanisi katika wizara zote
kutokana na wateule wake kuwa watendaji wazuri. “Mabadiliko ya Waziri Mwakyembe na Sitta yatakuwa
na faida kwa wizara zote mbili kwa kuwa hawa wote wanafanya kazi kwa
kujituma. Kila mmoja ataanzia pale alipoishia mwenzake na kufikia
malengo yanayotarajiwa,” alisema Alhaji Salum.
Alifafanua kuwa hata mawaziri wengine nao watakuwa
na mchango mkubwa kutokana na jitihada walizozionyesha walikotoka na
kumtolea mfano George Simbachawene kuwa alijituma vya kutosha alipokuwa
naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment