
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na
Rais Jakaya Kikwete juzi, yamekosolewa na wadau mbalimbali, wengi
wakilalamikia kuondolewa kwa Dk. Harrison Mwakyembe, kutoka Wizara ya
Uchukuzi kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Pia wametilia mashaka utendaji wa Samuel Sitta aliyehamishiwa
Uchukuzi kutoka Ushirikiano wa Afrika Mashariki na William Lukuvi
aliyehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge
kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakisema wizara
hizo zina changamoto nyingi kulinganisha na uwezo wao wa utendaji. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na
Christopher Chiza, aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na
Uwezeshaji) kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, nao wameelezwa
kuwa hawakupaswa kuacha katika baraza hilo kutokana na utendaji
usioridhisha. Yumo pia Anne Kilango aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango.
Aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa masuala ya Biokemia wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa Wakoti Nkya, ameyakosoa mabadiliko
yaliyofanywa na Rais Kikwete ya kumuondoa Dk. Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi na kumhamishia Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki. Alisema kuwa hayana tija kwa taifa kwa kuwa yanalenga kumpunguza
kasi baada ya kutibua ‘madudu’ Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la
Ndege nchini (ATCL) na Kampuni ya Reli (TRL). “Mwakyembe ameondolewa kwa sababu aligusa mizizi ya matajiri
wachache baada ya kuivuruga vuruga Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) ambayo imegeuzwa shamba la bibi na akaanza kuwashughulikia vigogo
hao kwa kuwasimamisha kazi na wengine kuwafukuza…TRL nako alirejesha
imani kwa wasafiri wa treni baada ya kufanya maboresho makubwa, lakini
ukweli kwamba alitoboa mirija ya wajanja, ndiyo maana kapelekwa Afrika
ya Mashariki,” alisema Profesa Nkya.
Profesa Nkya alisema kumuondoa Mwakyembe katika wizara hiyo
kutarejesha nyuma matumaini yaliyokuwa yameonekana ya kulifufua upya
Shirika la Reli nchini ambalo lilikuwa limetumbukia shimoni kutokana na
changamoto mbalimbali ikiwamo uduni wa miundo mbinu yake, kufa kwa
mitambo na kuziua njia za reli za kikaanda.
MHADHIRI IoU
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha
Iringa (IoU), Emanuel Damalo, alisema kwa mabadiliko hayo, Watanzania
wasitegemee mashirika kama ATCL na viwanja vya ndege vilivyokuwa
vikisumbuliwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya huku kukiwa na juhudi
za makusudi za kuyaokoa yasiingie shimoni, zitaendelea kwa kuwa suala la
uzalendo ni la mtu binafsi. Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa
Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi, alisema mabadiliko hayo ya baraza
la mawaziri hayana tija, kwa kuwa baadhi ya Wizara zitalegalega kutoa
huduma kutokana na aina ya wanasiasa waliopewa kuziongoza kukosa utashi
na uzalendo wa kweli wa kutumikia umma.
MWENYEKITI ASAs
Mwenyekiti wa Jumuiya za Wanataaluma Tanzania (ASAs), Paul
Loisulie, alisema mabadiliko hayo ni ya Rais na washauri wake ndio
wanaojua sababu za msingi za kuwaweka wahusika kwenye nafasi husika. Hata hivyo, alisema baadhi ya watu akiwamo yeye amepokea kwa masikitiko uhamisho wa Dk. Mwakyembe kutoka Uchukuzi. “Mnyonge apewe haki yake, alijitahidi sana pamoja na ugumu wa
maeneo kama bandari, viwanja vya ndege (madawa ya kulevya), meli, reli,
mabasi na malori... Maeneo yote haya yanagusa maslahi ya watu binafsi,
sina uhakika wala matumaini kwamba anaeingia Uchukuzi atafanya vizuri
zaidi ya anayeondoka,” alisema Loisulie na kuongeza kuwa wakati ukifika
itajulikana.
Kuhusu Simbachawene kuchukua nafasi ya Prof. Muhongo, Mhadhiri huyo alisema anafaa kushika wizara hiyo kwa sasa. Alisema mamlaka ya uteuzi haijakosea kumpa nafasi hiyo. Hata
hivyo, alisema lazima awe tayari kufanya kazi na watu wote hasa wabunge
bila kujali itikadi za kisiasa na aepuke majigambo kama mtangulizi wake. “Asikilize maoni ya watu na kuyafanyia kazi, unyenyekevu utamsaidia
sana katika Wizara hii ngumu, Lukuvi (William) naye kwenye ardhi ana
kibarua kigumu sana lakini akijipanga anaweza akafanya vizuri,” alisema.
MWENYEKITI THTU-UDOM
Naye Mwenyekiti wa chama wafanya kazi wa Elimu ya Juu tawi la Chuo
Kikuu cha Dodoma (THTU-UDOM), Nashon Maisori, alisema kwa jinsi Bunge
lilivyo Rais anapata wakati ngumu wa kupata mawaziri kutokana na baraza
lake kubadilishwamara kwa mara kufuatia mapungufu ya mawaziri. “Mweshimiwa Rais amejikuta hana watu tena wa kuwapa uwaziri,
inabidi tu sasa awekwe mtu kujaza nafasi na siyo lazima awe ana uwezo...
Ila suala la Mwakyembe, mimi binafsi nimeshtuka sana, sikutarajia
aondolewe Wizara ya Uchukuzi kwa sababu kwa mtizamo wangu alikuwa
anafanya kazi nzuri sana,” alisema.
Aliongeza: “Hata kwenye mpira kocha humpumzisha mchezaji aliyechoka
na siyo mchezaji anayetegemewa uwanjani. Kumpeleka huko Afrika
Mashariki ni kupoteza mchapa kazi mzuri na kumpa kazi laini, mawaziri
ambao walikuwa wakichapa kazi sana ni Magufuli na Mwakyembe tu wengine
business as usual.”
CHAUMMA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma),
Kayumbo Kabutari, alisema Baraza hilo ni la kivivu la bora wamalize
salama inavyoelekea Kikwete amebanwa ndani ya chama chake na makundi ya
urais yanayomhofia Mwakyembe ambaye ametengeneza jina kupitia Wizara ya
Uchukuzi. “Hivyo wamfiche Simbachawene ni mwendelezo wa kuficha uozo wa
wizara husika hakuna asilolijua la kifisadi kwani alikuwa msaidizi wa
karibu wa Muhongo upande wa nishati naibu waziri waliingia pamoja na
Muhongo,” alisema Kabutari.
Kuhusu Lukuvi, alisema ameshindwa kutatua mgogoro mdogo wa ardhi wa
Mamlaka ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) katika Manispaa
ya Dodoma na wananchi, hivyo hataweza kushughulikia migogoro mikubwa ya
ardhi nchi mzima,” alisema. “Hakuwatendea haki Watanzania kwa kumuondoa Dk. Mwakyembe Wizara
ya Uchukuzi ambayo alikuwa anakwenda nayo vizuri na kumuingiza Sitta
ambaye alikuwa Afrika Mashariki,” alisema Wachacha Peter, mkazi wa
Mabatini, jijini Mwanza na kuongeza kuwa Rais Kikwete amerudisha nyuma
maendeleo ya uchukuzi baada ya kumuondoa Dk. Mwakyembe na kumuingiza
Sitta aliyekuwa Wizara ya Afrika Mashariki.
Alisema Wizara ya Uchukuzi ambayo inahitaji waziri mwenye kasi,
inaweza kurudisha nyuma juhudi za wizara hiyo ambazo zilianza kuonyeshwa
na Waziri Mwakyembe katika kufufua reli ya kati. Hata hivyo, mkazi huyo alisema wizara nyingine zimefaanikiwa kupata
watendaji wazuri ingawa wapo mawaziri ‘mizigo’ walioachwa na kupelekwa
wizara nyingine.
Naye mdau wa siasa wa jijini Mwanza na mkazi wa Nyakato, Peter
James, alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete hayana tija kwa
Watanzania kutokana na baadhi ya wizara kiupelekewa mawaziri ‘mizigo’. “Hakuna jipya alilofanya Kikwete zaidi ya kuzidi kuzipa wizara
nyingine mizigo kutokana na kupelekewa watu ‘mizigo’...lakini kwa
kipindi kilichobaki cha miezi sita hawatafanya lolote la maana,” alisema
James.
Alisema kufanya uteuzi wa haraka haraka bila kuwafanya tathmini ya
utendaji wao, Rais Kikwete anazidi kuwaongezea kero wananchi kwa kuwapo
na mawaziri wasiowawajibikaji. Hata hivyo, mkazi wa Buhongwa nje kidogo na Jiji la Mwanza,
Christopher Chacha, alisema hashangazwi na mabadiliko hayo ya Kikwete
kutokana na kushindwa kuwaondoa mawaziri kama Dk. Shukuru Kawambwa na
Christopher Chiza.
JUKATA
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron
Mwakagenda, alisema babadiliko hayo yamefanyika kikiwa kimebaki kipindi
kifupi cha serikali ya awamu ya nne kuondoka madarakani, hivyo watanzania wasitarajie mambo mapya. “Hapo yamefanyika mabadiliko ya sura, hakuna jipya, kipindi kimebakia kifupi sana Watanzania wasitarajie jipya,” aliongeza.
DK. BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana,
alisema zipo Wizara ambazo zinahitaji utendaji wa hali ya juu na uzoefu
katika kazi, hususani Wizara ya Uchukuzi na Nishati ambazo alisema kwa
uteuzi ulifanyika haamini kama kutakuwa na mabadiliko yoyote. Alisema ameshangazwa na mabadiliko katika Wizara ya Uchukuzi kwa kuhamishwa Dk. Mwakyembe ambaye alionyesha mwanga kidogo wa
kushughulikia changamoto zinazoikabili wizara hiyo nyeti.
“Nimeshaganzwa na uteuzi wa Dk. Mwakyembe kupelekwa Wizara ya
Afrika Mashariki, wakati kuna matatizo makubwa ndani ya Wizara ya
Uchukuzi ambayo alikuwa ameanza kuyashughulikia ambayo alipaswa aendelee
ili ayamalize, ikiwamo suala la ATC, Bandari na kashfa zilizokuwa
zinaendelea Uwanja wa Ndege,” alisema Dk. Bana na kuongeza:
“Ninavyoamini Wizara ya Afrika Mashariki anakwenda kupumzika tu kwa
sababu haina kazi nyingi kama ilivyo ya Uchukuzi, ninashindwa kuelewa
ni kwa nini ametolewa pale anajua Rais mwenyewe, lakini mimi naona Dk.
Mwakyembe alifaa sana Uchukuzi.”
Aliongeza kuwa Sitta ni mtendaji mzuri, lakini kwa sababu Dk.
Mwakyembe alikuwa ameanza kufanya kazi nzuri, ni vema angeendelea nayo
ili kuhakikisha inakaa sawa. Akizungumzia Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzi ya Ufundi, Anna
Kilango, alisema haamini kama ataweza kuimudu wizara hiyo kwa kuwa uwezo
wake ni mdogo. Alisema hana imani kama Kilango ataweza kumshauri vizuri waziri
wake kwa kuwa ni mwanaharakati na kwamba uharakati na kazi aliyopewa
haviwezi kwenda pamoja.
Kuhusiana na Wiazara ya Nishati na Madini, ambayo amepewa
Simbachawene, alisema Wizara hiyo ni muhimu na ambayo inahitaji mtu
mzoefu na mchapakazi, lakini anaamini endapo atafanya kazi kwa bidii
ataiweza.
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willbrod Slaa, alisema watanzania wasitarajie matumaini yoyote katika
uteuzi huo. Akimzungumzia Lukuvi, alisema wakati akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge) alikuwa chanzo cha kukwamisha mchakato wa
Katiba, hivyo kumpeleka katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ni
kusababisha matatizo. “Kwa ujumla hata kwa hatua ambayo Tanzania imefikia kwa sasa
huwezi kutegemea kwamba yupo kiongozi yeyote wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ambaye atawaletea matumaini Watanzania, wote, ni matatizo matupu
hakuna mwenye nafuu, eti unamtoa Waziri ambaye hata chama chake
kinamwita mzigo unamhamishia Wizara nyingine,” alisema Dk. Slaa bila
kuwataja.
Hata hivyo, tangu mwaka juzi Katibu Mkuu wa CCM, Abdurlahman
Kinana na Katibu Mwenezi, Nape Nnauye katika ziara zao za kuhimiza
utekelezaji wa Ilani, wamekuwa wakiwataja kwa majina baadhi ya mawaziri
kuwa ni mizigo. Miongoni mwao ni Chiza na Kawambwa. Dk. Slaa alimtolea mfano Anna Kilango kwamba anadaiwa kuwa na
kashfa ya kuuza kiwanda cha Tangawizi katika Jimbo la Same Mashariki,
lakini anashangaa kuteuliwa kuongoza wizara muhimu.
PROF. BAREGU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa
Mwesiga Baregu, alisema uteuzi wa Rais umeonyesha wazi kuwa amekosa
timu ya mawaziri wa kufanya nao kazi. Alisema ni mara ya tano Rais anabadilisha Baraza la Mawaziri na kila anapofanya hivyo hakuna mabadiliko yeyote yanayoonekana. “Mabadiliko haya ya Baraza la Mawaziri, yanaonyesha kuwa Rais
amekosa timu ya Mawaziri wa kufanya nao kazi, hana uwanja mpana wa
kumsaidia kupata watendaji, hii ni kwa sababu ya Katiba ambayo
inamruhusu kuteua ndani ya Bunge tu wakati watendaji wengine wazuri wako
nje ya Bunge,” alisema Profesa Baregu.
Aliongeza: “Na ndiyo maana wananchi walipendekeza kwa iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Mawaziri wasiwe Wabunge, hii ingempa
Rais wigo mpana na angepata watendaji wazuri, tofauti na ilivyo sasa,
Rais anakosa watendaji kwa hiyo anakuwa anazunguka mle mle, anamteua
Waziri anashindwa hapa, anamjaribu pengine kwa sababu tu anakosa watu,
na jambo hili ni hatari. Kwa hiyo hata mimi siwezi kusema nani ataweza
na nani atashindwa kwa sababu wengine tulisema wanaweza, lakini
wameshindwa.”
DK. SEMBOJA
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji
Semboja, aalisema ana imani na Sitta kutokana na uadilifu na utendaji
wake kazi serikalini na kuwa lisema ili Sitta afanye kazi kwa usahihi,
anahitaji ushirikiano kati yake na watendaji wa wizara nzima. “Mawaziri wengi wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa
sababu ya kutopewa ushirikiano na watendaji, hali inayopelekea
kuenguliwa nafasi zao,” alisema Dk. Semboja.
Kuhusu Simbachawene, alisema kinachotakiwa kufanyika ndani ya
wizara hiyo ni kumpa ushirikiano ili aweze kutatua changamoto zilizomo
na kufufua matumaini ya Watanzania. Aidha, alisema hana wasiwasi na utendaji kazi wa Wasira kwa kuwa anafahamika kwa umakini wake kazini.
Aliongeza kuwa, bado ana wasiwasi na uteuzi wa Lukuvi kwa kuwa mara nyingi amekuwa akituhumiwa kwa utendaji usioridhisha. “Natilia shaka utendaji wa kazi wa Lukuvi, ni bora Rais angemteua
Naibu Waziri wake (Angela Kairuki) kuchukua nafasi, hapo nisingetilia
shaka uteuzi uliofanyika,” alisema.
NYAKEKE WA TRAWU
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania
(Trawu), alisema haungi mkono mabadiliko hayo hususan wale waliohamishwa
kwenye wizara zao akiwamo Dk. Mwakyembe na Sitta aliyepelekwa kuchukua
nafasi yake. Alisema kubadilishwa kwa mawaziri wenye utendaji mzuri kama Dk.
Mwakyembe kunarudisha nyuma utendaji na maendeleo ya wizara husika
ambayo yalikuwa yameanza kuonekana na kwamba kwa kuwa uchaguzi mkuu
umekaribia, ingekuwa vizuri kuwaacha katika wizara zao.
Kubadilishwa kwa Baraza hilo la Mawaziri kumetoka na Waziri
aliyekuwa anaiongoza Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo kujiuzulu na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kufutwa kazi kutokana na
kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment