
Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM kutoka Tanzania Bara na Visiwani 
Zanzibar wakishiriki matembezi ya kuwaenzi viongozi wa Kitaifa katika 
kuadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyofanyika mjini 
Unguja juzi.
Wakati 
Wazanzibari leo wakiadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi, wanasiasa na wasomi
 wametaka wananchi hao kufanya mikakati muhimu ya maendeleo na kuacha 
fikra mgando zinazoathiri maendeleo yao na nchi yao. Wasomi na wanasiasa hao amesema Zanzibar imepiga 
hatua kubwa za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa lakini zinaweza 
kuendelezwa au kuharibiwa na Wazanzibari wenyewe iwapo wataendekeza 
tofauti zao za kihistoria zinazohusiana na mapinduzi.
Zanzibar inaadhimisha sherehe hizo huku kukiwa na 
matukio mawili makubwa ya kitaifa yanayoisubiri ikiwamo Kura ya Maoni ya
 Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo kwa namna moja au 
nyingine yanatajwa kuwa kipimo kikuu cha mwelekeo wa visiwa hivyo 
kisiasa.
Maadhimisho hayo yatakayoongozwa na Rais wa 
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye Uwanja wa Amaan, yatahudhuriwa pia
 na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya 
Mapinduzi na ile ya Muungano.
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha 
Zanzibar, Ali Uki alisema pamoja na kwamba Zanzibar imepiga hatua katika
 ujenzi wa miundombinu, huduma za kijamii, sheria, kilimo na maendeleo 
ya kisiasa kudumisha amani ndilo jambo la msingi. “Suala la maendeleo hayo yamefikiwa kwa kiwango 
gani? Kila mtu anatazama kwa jicho na mtazamo wake,” alisema Uki na 
kuongeza kuwa kisiasa kuna mafanikio makubwa.
Alisema tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 
1992, Zanzibar imekuwa ikijitahidi kuhimili misukosuko mbalimbali ya 
kisiasa ukiwamo upinzani mkali baina ya CCM na CUF uliosababisha kuundwa
 kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Alisema mbali na mafanikio hayo, kuna haja ya 
kufanya mkutano wa kitaifa wa kukubaliana kiwango cha sera za kufuatwa 
kutoka katika kila chama kwani licha ya kuwa na SUK hivi sasa, sera za 
CCM ndizo zinazofuatwa.
Iwapo itaonekana hili ni tatizo katika mwaka huu 
wenye changamoto za Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, Uki alisema kila 
chama kinaweza kukaa katika kamati zake na wataalamu na kuamua kuhusu 
kujumuisha sera zao ili kujenga mustakabali bora wa kisiasa Zanzibar. “Watu waache fikra mgando kwamba hili ni suala 
langu na lile ni la yule, wafanye maendeleo kwa ushirikiano kwa kuwa 
mustakabali wa Zanzibar utatengenezwa na wao wenyewe,” alisema.
Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo 
Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema Mapinduzi ya Zanzibar 
yana mafanikio makubwa na yameendelea kuwapo bila mapinduzi mengine, 
jambo linaloonyesha yalikubalika vizuri. Alisema mapinduzi yalifanikiwa kuendana na 
misukosuko ya kisiasa ukiwamo mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulioleta 
uga wa kisiasa usiotabirika wa nani atakuwa mshindi katika uchaguzi mkuu
 wowote. Kuhusu mwaka huu wa uchaguzi, Mbunda alisema CUF na CCM vina nguvu sawa, hivyo ni lazima hali hiyo itawagawa Wazanzibari.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu
 alisema mustakabali wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika upo 
mikononi mwa wananchi wote na kwamba Kura ya Maoni ya Katiba inaweza 
kuamua hatima yake. “Wananchi wenyewe ndiyo watakaoamua lakini lazima 
mazingira yote ya upigaji kura yawekwe sawa. Utaratibu wa kampeni uwe 
sahihi, watu wote wazungumze kwa uhuru, vyombo vya habari vitumike 
vizuri bila kuunga mkono upande wowote hapo ndipo tutasikia Wazanzibari 
wanataka Muungano wa aina ipi,” alibainisha Lissu.
Maadhimisho
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa 
Pili wa Rais, Dk Khalid Mohamed Salum alisema milango ya Uwanja wa Amaan
 itafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi na viongozi wataanza kuwasili na 
saa tatu asubuhi. Viongozi wengine wa kitaifa wanaotarajiwa 
kuhudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim 
Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha. Dk Shein atapokea heshima na salamu kutoka kwa 
askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kabla ya kukagua gwaride na 
kulihutubia Taifa.
Tofauti na miaka ya nyuma, Baraza za CUF pamoja na
 ofisi zake, zimepambwa katika maeneo mbalimbali kama Michenzani huku 
vijana wa chama hicho wakishiriki kufanya usafi wa mazingira kwa ajili 
ya shughuli hiyo. Dk Shein anatarajiwa kuzungumzia mwelekeo wa 
uchumi wa Zanzibar, huduma za kijamii, hali ya kisiasa katika kuelekea 
Kura za Maoni, Uchaguzi Mkuu pamoja na mafanikio ya SUK na changamoto 
zake.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment