Kampuni ya Huduma za utalii ya Leisure Tours,  
Holidays Wellworth Hotels na Lodges Limited na Kampuni ya pembejeo ya 
Tanzania Bags Corporation (TBC),  zimeiomba Mahakama Kuu Kitengo cha 
Biashara kulipiga mnada jengo la Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ili 
kufidia madeni ambayo zinalidai shirika hilo.
Kampuni hizo zinalidai ATCL  Dola za Marekani 1,182,595.38 (Sh. bilioni 2.06) kufuatia kesi zilizolifungulia na shirika hilo.
Leisure Tours and Holidays inalidai ATCL Dola za Marekani 477,506.38 
(Sh. milioni 830.86),  Wellworth Hotels & Lodges Limited inalidai 
Dola za Marekani 661,089 (Sh. bilioni 1.15)na TBC inadai Dola za 
Marekani 44000 (Sh. milioni 76.56).Kampuni hizo zimefikia hatua ya kuomba mahakama iamuru jengo hilo lipigwe mnada baada ATCL na Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kushindwa kutekeleza makubalino ya ulipwaji wa madeni hayo yaliyofanyika baina yake na kampuni hizo Septemba mwaka jana. Katika makubaliano hayo, Serikali na ATCL ziliahidi kulipa madeni hayo yote kwa awamu tatu, kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2014, lakini hadi sasa mdaiwa hajalipa madeni hayo.
Baada ya ATCL na Serikali kushindwa kutekeleza makubaliano hayo, kampuni hizo ambazo zinawakilishwa na kampuni ya Uwakili ya Msemwa Company Advocates, zimeiandikia barua Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara zikiomba iendelee na utekelezaji wa tuzo zake za uuzaji wa magari. Katika barua hiyo ya Januari 8, mwaka huu, iliyosainiwa na Wakili Jerome Msemwa, kwenda kwa Msajili wa mahakama hiyo, wadai hao wanaiomba mahakama iendelee na utekelezaji wa tuzo hizo kwa kuamuru jengo la ATCL lililoko katika mtaa wa Ohio kupigwa mnada.
Hivyo kupitia barua hiyo wadai hao wanaiomba mahakama imteue dalali wa mahakama kwa ajili ya kuuza jengo hilo, ili kufidia deni linalodaiwa bila kuchelewa. Februari 2013, Leisure iliwasilisha maombi ya kupigwa mnada kwa jengo hilo ili kufidia deni lake hilo, baada ya ATCL kushindwa kutekeleza makubaliano waliyofikia nje ya mahakama katika kesi yake ya madai namba 56 ya mwaka 2009.
Kampuni hiyo ilikuwa ikimdai mshindwa tuzo Dola za Marekani 716,259.25 (Sh. bilioni 1.25) baada ya kushindwa kulipia huduma za ukodishaji wa magari. Lakini baadaye walikubaliana kuzungumza nje ya mahakama na kufikia makubaliano kuwa mshindwa tuzo amlipe mshinda tuzo kiasi cha Dola 596,882.97 (Sh. bilioni 1.04) kwa awamu tatu, na kila awamu alipe Dola 198,960.99 (Sh. 317 milioni) kwa kadri anavyopata fungu kutoka Hazina.
Pia, walikubaliana mshindwa tuzo amlipe mshinda tuzo kiasi cha Dola 119, 376.97 (Sh. milioni 207.71) kikiwa ni riba ya asilimia 10 kwa mwaka ya malipo ya msingi, kwa kipindi cha mwaka wa 2009 na 2010, kwa awamu tatu. Aprili 8, 2011, makubaliano hayo yaliwasilishwa mahakamani na pande zote ziliyasaini na mahakama hiyo iliyaidhinisha kuwa hukumu yake na mshindwa tuzo hakutekeleza makubaliano hayo.
Novemba 20, 2012, Mahakama hiyo ilimwamuru mshindwa tuzo kuwasilisha mahakamani jedwali la malipo ndani ya mwezi mmoja tangu tarehe ya amri hiyo, lakini pia mshindwa tuzo bado hakutekeleza amri hiyo na hivyo mshinda tuzo akafungua maombi ya kupiga mnada jengo hilo. Februari 11, 2013, mahakama hiyo katika amri yake iliyotolewa na Jaji Robert Makaramba ilimwamuru mshinda tuzo kufanya uthamini wa jengo hilo na ilibainika kuwa lina thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 12.
CHANZO:
					NIPASHE
				
No comments:
Post a Comment