Social Icons

Pages

Thursday, January 15, 2015

VIPAUMBELE VYA KIUCHUMI KITAIFA MWAKA 2015


Nchi waisani ziko njia panda kuendelea au kutoendelea kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea.
Kuongezeka kwa mbinu hizi ni bora kuliko kuendelea kutarajia “sera za msamaria mwema (donor-aid syndrome)” tulizo zizoea kwa kipindi kirefu.
Nchi nyingi za wahisani hivi sasa zimefika njia panda. Ama zipunguze kiwango cha misaada kwa nchi zinazoendelea baada ya kujiridhisha kwamba kiwango kikubwa cha misaada yao kwa nchi hizo haziwafikii kabisa walengwa halisi wa misaada hiyo. Au zibadilishe mfumo wa utoaji misaada kwa nchi maskini duniani, ili kuhakikisha misaada hiyo inakwenda moja kwa moja kwa walengwa badala ya kupitia taasisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs). Kutokana na mabadiliko ya kimtazamo kutoka kwa wahisani yanayo tarajiwa kuongezeka nguvu katika miaka ya karibuni, Tanzania inashauriwa ijipange upya katika kusimamia vyema matumizi sahihi ya maliasili na rasilimali zake kwa manufaa ya watu wake.
Vipaumbele mwaka 2015
Miongoni mwa vipaumbele vya kiuchumi kitaifa katika mwaka 2015 ni hivi vifuatavyo;
Moja, kudhibiti mfumuko wa bei nchini ili kuleta unafuu wa maisha kwa kila Mtanzania. Utakuwa ujinga wa hali ya juu kuendelea kufikiri kwamba kwa kuzidi kudhibiti ujazo wa fedha peke yake katika uchumi (control/regulate money supply) na hatimaye kupunguza kasi ya mzunguko wa fedha, ni hatua tosha ya kudhibiti mfumuko wa bei nchini. Ikiwa sehemu kubwa ya mahitaji ya msingi ya nchi yanatokana au kutegemea uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje, huwezi kuzuia au kudhibiti kiwango fulani cha mfumuko wa bei kitakachopenya nchini kupitia bidhaa zitokazo nje. Huwezi kuwa na uwezo wa kudhibiti mfumuko wa bei nchini, ikiwa kiasi kikubwa cha bidhaa muhimu katika maisha ya kila siku kitaendelea kusafirishwa kwa malori kwa njia ya barabara kutoka pembe moja ya nchi kwenda mipakani na pembe nyingine za nchi. Ni kweli, hatuwezi kuwa na mfumo wa reli nchi nzima, lakini tunautumiaje mfumo wa reli uliopo hivi sasa? Bidhaa muhimu kama sukari, mahindi na nafaka nyingine, saruji, mabati, mbao ni rahisi kusafirishwa kwa reli kuliko barabara.
Mbili, uimarishwaji wa thamani ya shilingi yetu.
Tusipokisifia chetu wenyewe, nani atakayekisifia kwa niaba yetu? Lazima tuonyeshe jitihada za dhati kiuchumi katika kuilinda shilingi isizidi kuporomoka na kupoteza zaidi thamani yake. Njia mojawapo ya kuimarisha zaidi thamani ya shilingi ni kuimarisha na kuongeza zaidi sekta ya biashara au mauzo ya bidhaa zetu nchi za nje. Lazima mauzo ya nje yaongezeke na wakati huohuo, Serikali idhibiti zaidi uagizaji kutoka nje wa bidhaa duni zisizo na kiwango cha ubora wa kimataifa, ambazo pengine ingewezekana kabisa kuzitengeneza hapa hapa nchini.
Tatu, ongezeko katika tija na ufanisi katika uzalishaji mali.
Ili mauzo yetu ya nje yaongezeke zaidi, lazima kiwango cha uzalishaji, hususan viwandani kiongezeke zaidi. Ili uzalishaji viwandani uongezeke zaidi, lazima wafanyakazi viwandani na sekta nyingineziwe na stadi husika za ufundi. Pia wapewe mafunzo ya mara kwa mara ya stadi kwa vitendo, walipwe mishahara na marupurupu au motisha inayolingana na ujuzi wa michango yao katika uzalishaji mali. Lazima pawapo na mageuzi makubwa na ya kimsingi katika mitalaa ya elimu ya ufundi na biashara katika vyuo vyetu itakayowezesha upatikanaji wa wahitimu wanaoajirika au kuhitajika kulingana na nguvu na hali halisi ya soko la ajira nchini.
Nne, tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Kukithiri kwa ukosefu wa ajira, hususan miongoni mwa vijana ni tatizo lililoendelea kuumiza vichwa vya watunga sera na watendaji pamoja na vijana wenyewe. Kukithiri au kuongezeka kwa ukosefu wa ajira nchini ni dalili tosha ya kuzorota au kudorora kwa uchumi wetu. Uchumi unaoimarika zaidi utajidhihirisha katika kutengeneza nafasi nyingi zaidi za ajira mpya nchini. Ukuaji wa uchumi kwa kigezo cha ongezeko la Pato la Taifa tu bila ya kupungua kwa kiwango cha ukosefu wa ajira, kuboreka kwa thamani ya shilingi au bila ya kuambatana na unafuu wa maisha kwa Watanzania, hauna maana yoyote katika maana halisi ya kuimarika kwa uchumi.
Tano, mfumo wa utozaji kodi nchini
Mfumo wa utozaji kodi nchini usipokuwa rafiki kwa wawekezaji au katika uwekezaji, unaweza kuwa kikwazo katika kuongeza uzalishaji mali na kuzorotesha jitihada za kuongeza mauzo nje ya nchi. Mfumo wa utozaji kodi usiojali gharama au utakaopuuzia gharama halisi za uzalishaji mali viwandani (kwa kuipendelea zaidi Serikali itunishe mapato yake) na katika sekta nyingine zote za uchumi, lazima utafifisha kiwango cha uwekezaji na uzalishaji viwandani. Mfumo wa utozaji kodi utakao ingilia mchakato mzima wa upangaji bei kwa walaji uliopendekezwa na wawekezaji au wazalishaji mali ili kuinufaisha zaidi Serikali katika kutunisha mapato yake, utazorotesha tija na ufanisi katika uzalishaji. Mfumo kandamizi wa utozaji kodi usiozingatia mifumo inayotumika katika nchi majirani, utakimbiza wawekezaji. Utaongeza ukosefu wa ajira nchini na utapunguza mauzo yetu nchi za nje.
Sita, mapambano dhidi ya kukithiri kwa rushwa na ufisadi nchini.
Kukithiri kwa rushwa na ufisadi kutakimbiza wawekezaji na kuzorotesha kiwango cha uzalishaji mali nchini.
Saba, masoko.
Nguvu za soko zitakaposhindwa kupanga bei halisi za soko zitakazoakisi thamani halisi ya bidhaa husika katika uchumi ni dalili ya udhaifu wa sera na utendaji mbovu. Fikiria nchi imevuna mchele kupita mahitaji na mpunga mwingine unaharibikia mashambani kwa kukosa soko. Cha ajabu, bado utakuta bei za rejareja kwa walaji bado ziko palepale na hazina dalili ya kushuka kwa kipindi cha msimu mzima.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: