Pages

Wednesday, January 28, 2015

TANROADS YATOZA MALORI MAMILIONI

Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) mkoani hapa,  imekusanya maduhuri ya Sh. 130,110,300 kwa kutoza  wafanyabiashara wa magari na madereva wao kwa  kukiuka sheria za matumizi ya barabara kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Isack Mwanawima, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita. Mwanawima alisema makusanyo ya maduhuri hayo ni ya kipindi cha cha robo ya nne ya mwaka wa fedha wa  2013/2014 hadi robo ya pili ya mwaka 2014/2015 kwa kutumia mizani iliyopo kijiji cha Nangurukuru wilaya ya Kilwa na Mingoyo Manispaa ya Lindi.
Mwanawima alisema katika kipindi hicho, malori makubwa yapatayo 110,122 yalipimwa kwenye mizani hizo zilizopo  barabara kuu ya Kibiti-Lindi, kati ya hao, 23,319 yalibainika kuzidisha uzito. Alisema maduhuri hayo yametokana na tozo kwa magari 1,374 yalikutwa yamezidisha uzito zaidi ya ya asilimia tano ya ile inayoruhusiwa kisheria na kutozwa kiasi hicho cha fedha.
"Kuna ongezeko kubwa la magari katika barabara ya Dar es Salaam,Lindi na Mtwara kutoka 49,385 kipindi cha Desemba mwaka 2013 hadi Mei mwaka jana," alisema. Alisema pamoja na ongezeko hilo, wastani wa kuzidisha uzito ni wa asilimia 21.18, hivyo kwa mkoa wa Lindi upo chini kwa asilimia tano ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 26.40.
Mkuu wa mkoa huo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao hicho, Mwantumu Mahiza, aliwasisitiza wafanyabiashara hao wa malori hao kuzingatia sheria kwa kupakia mizigo inavyoelekeza ili kuzitunza barabara na kumudu kwa muda mrefu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment