Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) mkoani hapa,
imekusanya maduhuri ya Sh. 130,110,300 kwa kutoza wafanyabiashara wa
magari na madereva wao kwa kukiuka sheria za matumizi ya barabara kwa
kipindi cha miezi sita iliyopita.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Isack Mwanawima,
wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji katika kikao cha Bodi ya
Barabara Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini hapa mwishoni mwa wiki
iliyopita. Mwanawima alisema makusanyo ya maduhuri hayo ni ya kipindi cha cha
robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 hadi robo ya pili ya mwaka
2014/2015 kwa kutumia mizani iliyopo kijiji cha Nangurukuru wilaya ya
Kilwa na Mingoyo Manispaa ya Lindi.
Mwanawima alisema katika kipindi hicho, malori makubwa yapatayo
110,122 yalipimwa kwenye mizani hizo zilizopo barabara kuu ya
Kibiti-Lindi, kati ya hao, 23,319 yalibainika kuzidisha uzito. Alisema maduhuri hayo yametokana na tozo kwa magari 1,374 yalikutwa
yamezidisha uzito zaidi ya ya asilimia tano ya ile inayoruhusiwa
kisheria na kutozwa kiasi hicho cha fedha.
"Kuna ongezeko kubwa la magari katika barabara ya Dar es
Salaam,Lindi na Mtwara kutoka 49,385 kipindi cha Desemba mwaka 2013 hadi
Mei mwaka jana," alisema. Alisema pamoja na ongezeko hilo, wastani wa kuzidisha uzito ni wa
asilimia 21.18, hivyo kwa mkoa wa Lindi upo chini kwa asilimia tano
ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 26.40.
Mkuu wa mkoa huo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao hicho, Mwantumu
Mahiza, aliwasisitiza wafanyabiashara hao wa malori hao kuzingatia
sheria kwa kupakia mizigo inavyoelekeza ili kuzitunza barabara na kumudu
kwa muda mrefu.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment