Pages

Saturday, January 03, 2015

RAIS AMTEUA DK. MANYAHI KUWA M'KITI BODI YA TANESCO

Rais Jakaya Kikwete, amemteua, Dk Mighanda Manyahi, kuwa mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava, bodi hiyo itakuwa na wajumbe nane. Kufuatia uteuzi huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewateua wajumbe nane ambao ni Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Dk. Haji Semboja, Shabaan Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro kuiongoza  Tanesco.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, wajumbe hao watafanya kazi na bodi hiyo kuanzia Januari  mwaka huu hadi Desemba 31, mwaka 2017. Uteuzi huo unachukua nafasi ya bodi iliyomaliza muda wake  na kukumbwa na kashfa ya Escrow iliyohusisha uchotaji wa Shilingi bilioni 300 kwenye akaunti hiyo ya escow wakati huo ikiongozwa na  Mwenyekiti , Jenerali Robert Mboma aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi. Bodi hiyo ilianza kazi   mwaka 2011.
Baadhi ya wajumbe wa bodi iliyomaliza muda wake ni aliyekuwa Mkurugenzi  mstaafu wa Tanesco  Baruany Luhanga  wengine ni Ridhiwan Masudi, Leonard Msanja, Vintan Mbiro, Victor Mwambalaswa, Abdul Kitula na Beatus Segeja. Katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, Bunge la Jamhuri la Muungano, lilipendekeza kuvunjwa kwa bodi ya Tanesco kutokana na kusababisha fedha kuchotwa na kushindwa kusimamia kikamilifu maslahi ya taifa.
Hata hivyo, Rais Kikwete wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam , alisema bodi hiyo imemaliza muda wake na kwamba ipo katika mchakato wa kuundwa bodi nyingine mpya na tayari alikwisha teua mwenyekiti. Hakusema watachukuliwa hatua gani mbali na kueleza kuwa muda wake ulimalizika.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment