Palestina inatazamiwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kufuatia hatua ya Rais Mahmoud Abbas
kusaini mkataba wa mahakama hiyo mjini The Hague.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliitolea wito ICC
kulikataa ombi la Palestina kujiunga na mahakama hiyo, aliloliita la
kinafiki. Kwa mujibu wa Netanyahu, serikali ya Mamlaka ya Palestina si
dola, bali kundi lililounda ushirikiano na kundi jengine la kigaidi,
Hamas, ambalo linafanya uhalifu wa kivita.
"Israel ni dola linalofuata sheria na lenye jeshi lenye maadili
linaloheshimu sheria zote za kimataifa. Tutawalinda wanajeshi wetu kama
wao wanavyotulinda sisi." Ilisema taarifa iliyotolewa na ofisi ya
Netanyahu, baada ya kikao cha dharura kwenye makao makuu ya wizara ya
ulinzi hapo Alhamisi.
Siku ya umatano, Rais Abbas alisaini mkataba wa ICC na makubaliano
mengine 19 ya kimataifa, kufuatia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa siku moja nyuma, kulikataa pendekezo la Palestina kuitaka
Israel ikomeshe ukaliaji wake kufikia mwaka 2017.
"Tunataka kulalamika. Israel inatushambulia sisi na ardhi yetu kila
siku. Sasa tulalamike kwa nani, ikiwa Baraza la Usalama limetuangusha?"
Abbas aliuambia umma wa waandamanaji mjini Ramallah hapo juzi, baada ya
mkutano wa dharura na serikali yake.
Marekani, Israel zakasirika
Marekani na Israel zilichukizwa sana na hatua ya Abbas kusaini
mkataba huo, ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani,
Jeffrey Rathke, alisema ni hatua isiyo na manufaa kabisa, na ambayo
haipiganii matakwa ya Wapalestina ya kuwa na dola huru yenye mamlaka
kamili.
Kwa mujibu wa kanuni za ICC, uwanachama wa Palestina utairuhusu
mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, kuchunguza
tuhuma za uhalifu wa kivita uliotendwa ndani ya ardhi ya Palestina, bila
ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambako Israel
inakingiwa kifua na Marekani.
Ingawa Israel si mwanachama wa mahakama hiyo, raia wake wanaweza kushitakiwa kwa matendo yao katika ardhi ya Wapalestina.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment