Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
Serikali imesema haikubaliani na uamuzi wa Serikali
ya Kenya ya kuendelea kuzuia magari ya Tanzania kuingia katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata kupeleka na kupokea watalii
wanaokuja Tanzania.
Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliyasema
hayo wakati akizugumza na wasafirishaji wa abiria na watalii katika
maegesho ya Mezaluna. Alisema serikali imeshtushwa mno na hatua hiyo ambayo imeleta
usumbufu mkubwa kwa wasafiri hasa watalii wanaokuja Tanzania kupitia
uwanja huo.
Nyalandu alisema hatua hiyo inahatarisha mahusiano mazuri ya muda mrefu ya kibiashara kati ya Kenya na Tanzania. “Tunafahamu tulikuwa na mkataba na Kenya kuhusu mwingiliano katika
biashara kwenye sekta ya utalii. Serikali ya Awamu ya Kwanza ilifunga
barabara Bologonja iliyopo kusini mwa hifadhi ya Serengeti na Kenya
walituomba tufungue barabara hiyo tukawaaambia watupe nafasi ya kufanya
utafiti iwapo inawezekana,” alisema Nyalandu.
Alisema baada ya Tanzania kuonyesha msimamo huo, wakaamua kuzuia magari kuingia Uwanja wa Ndege kama kulipiza kisasi. "Ni jambo la ajabu sana kwani uwanja wa ndege hauwezi kuwa sehemu ya vivutio vya utalii," alisema. Aliongeza: “Wiki ijayo nitakwenda Nairobi kuzungumza na Waziri wa
masuala ya utalii wa Kenya kuhusu jambo hili ili tujue hatua za
kuchukua."
Awali wasafirishaji walimwambia Waziri Nyalandu kuwa toka Desemba
22, mwaka jana, magari yao yalizuiwa kuingia katika Uwanja wa Ndege wa
Jomo Kenyata na kusabababisha adha kubwa kwa watalii. Mkurugenzi wa kampuni ya Riverside, Mosses King’ori, alisema kuwa
watalii wamekuwa wakihofu usalama wao kila wanaposhushwa na mizigo yao
nje ya uzio wa uwanja. “Biashara yetu ipo katika tishio kubwa, lakini hata kwa utalii
wakwetu. Wageni wanaogopa sana hali hii...napata maswali mengi kutoka
kwa mawakala wa Ulaya ambao tunafanya kazi wanadai wageni wanalalamika
na wengine wana hofu kuja Tanzania,” alisema King’ori.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Rainbow, Mathew Mollel, alieleza kuwa
serikali imechelewa mno kufuatilia jambo hilo na kusababisha madereva
na Watanzania wengine kupata shida kubwa kutokana na katazo hilo. “Serikali sasa ituambie ukweli utalii ni sehemu kubwa ya uchumi wa
nchi yetu, ni eneo linalopaswa kulindwa sana,” alisisitiza Mollel.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment