Pages

Tuesday, January 13, 2015

KINGUNGE AFUNGUKA URAIS CCM

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, amefunguka na kusema kuwa hakuna aliye msafi katika makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa wote wanatumia fedha na kufanya faulo mbalimbali katika kusaka nafasi hiyo nyeti katika uongozi wa nchi, kinyume cha maadili.
Alisema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha ‘Kumekucha’, kilichorushwa hewani na kituo cha Independent Television (ITV) jana asubuhi. Alisema wakati nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, mpaka sasa wote wanaotaka kuwania urais wanakabiliwa na matatizo mawili; ukiwamo ukosefu wa uadilifu na matumizi ya fedha. “Nikwambie ukweli. Waliojitokeza kugombea urais, wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua hilo,” alisema Kingunge bila kumtaja ‘mgombea’ yeyote aliyetangaza na anayetajwa kutaka kuwania nafasi hiyo.
Mzee Kingunge mmoja wa viongozi wastaafu wafuasi wakubwa wa itikadi ya Ujamaa na Azimio la Arusha aliongeza: “Badala ya kutafuta mchawi, tutazame namna ya kushughulikia hilo la maadili sababu hakuna msafi.” Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kuliko zote nchini ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.  Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta namawaziri  wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wanatajwa pia Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Kati ya makada hao, sita waliwahi kuitwa na Kamati Ndogo ya Nidhamu iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, na kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao kabla ya wakati. Baada ya mahojiano hayo, Februari, mwaka jana, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilitangaza uamuzi mzito dhidi ya makada wake hao baada ya kutiwa hatiani, kwa kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku pia wakiwa chini ya uangalizi.
Makada hao ni pamoja na Sumaye, Lowassa, Membe, Wasira, Ngeleja na Makamba, ambao mwezi ujao, wanatarajiwa kukamilisha kutumikia kifungo chao huku chama kikisubiriwa kutangaza hatma yao wakati wowote kuanzia wiki hii baada ya kipindi cha uangalizi kupita.
Kauli hiyo ya Kingunge imetolewa siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete juzi ‘kuwaangukia’ viongozi wa dini nchini akiwaomba kusaidia kudhibiti makundi ya wagombea urais yaliyoanza mbio za kujipitisha kwenye nyumba za ibada kunadi sera zao ili kujisafishia njia ya kwenda Ikulu. Rais Kikwete alisema iwapo viongozi hao wa dini watakataa kuhadaiwa na wanasiasa hao ili wawape nafasi ya kujitengenezea kete ya kisiasa ya kutekeleza dhamira zao kupitia nyumba za ibada, watalisaidia taifa kupata kiongozi mzalendo na mwadilifu. Alisema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni mstaafu, George Mkuchika, kwenye ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu mpya wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaoatarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu, kuwaruhusu wanasiasa kunadi sera zao ndani ya nyumba za ibada ni kuruhusu tatizo. “Rai yangu kwenu viongozi wote wa dini, Mheshimiwa Baba Askofu, Mkuu wa Kanisa la KKKT (Malasusa), msiwakaribishe tena wanasiasa kutumia maeneo ya kanisa kwa shughuli za kisiasa. Na ninyi wanasiasa, acheni kuchanganya dini na masuala ya kisiasa,” alisema.
Kauli ya Rais Kikwete ilitolewa baada ya Nchemba kukaririwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akisema masheikh na maaskofu wamemuomba awanie urais katika kinyanyang’iro hicho. Kadhalika, makada wengi miongoni mwa wanaousaka urais wamekuwa wakihudhuria katika shughuli mbalimbali makanisani na misikitini na kupewa nafasi za kuzungumza.
Awali, Kingunge alisema makada wote waliojitokeza kutangaza nia ya kutaka kugombea urais, hawajatenda dhambi, kwani waamuzi wa mwisho watakuwa ni wananchi kwa kuwa ndiyo wanaomjua kila mtu alichonacho na uwezo alionao. Hata hivyo, alisema hatua hiyo imekuwa ikiwafanya wananchi kushangaa kuona kila mtu amekuwa akijitokeza na kutangaza kutaka kuwania nafasi hiyo.
“Kwa sababu Rais hachaguliwi kama wachezaji,” alisema Mzee Kingunge.
Alisema anaamini Rais anayefaa ni yule tu atakayeweza kumudu kuwaunganisha pamoja Watanzania kama taifa, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero zinazowakabili, hasa umaskini, kwa vitendo na siyo anayejali nafsi yake. Kuhusu maendeleo tangu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Kingunge alisema Zanzibar, Bara na Afrika kwa jumla zimepiga hatua, lakini iliyopo haitoshi kwa kuwa mwendo wake ni wa konokono.
“Mwalimu (Nyerere) alisema wakati wenzetu (duniani) wanatembea, sisi tukimbie. Bahati mbaya Afrika tunatembea, wenzetu wanakimbia, wanatuacha nyuma,” alisema Komredi Kingunge.
Kuhusu ajira kwa vijana, alisema kuna tatizo siyo kwa Tanzania tu, bali Afrika kwa jumla. Hivyo, akasema unahitajka mkakati mpya wa kujikwamua, ikiwamo kuhakikisha sekta ya uchumi na elimu zinakwenda sawasawa. Alisema ajira siyo kuajiriwa tu, bali pia kujiajiri, hivyo akashauri kuwapo mkakati mahsusi kuwajengea vijana uwezo ili wajiajiri na kwamba, iwapo hilo litatekelezwa kwa vitendo suala la ajira halitaweza kusumbua.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment