
Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Kigogo Fresh B ,
 Mariano Bungala (CCM),  akisaidiwa na askari Polisi baada ya kuvamiwa 
na kundi la wananchi jijini Dar es Salaam baada ya kutaka kuingia kwenye
 ukumbi wa Manispaa ya Ilala wa Arnatoglou jana kuapishwa kwa madai 
uchaguzi haukufanyika katika mtaa huo baada ya kuahirishwa.
Uapishaji wenyeviti wa serikali za mitaa katika 
Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine umekumbwa na 
vurugu zilizosababisha aliyekuwa mgombea uenyekiti kupitia Chama Cha 
Mapinduzi (CCM) kupewa kipigo na wananchi mbele ya askari polisi na 
kuchaniwa nguo zake kwa madai alitaka kuapishwa kinyemela.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda , ametajwa na kulalamikiwa kuwa chanzo 
cha vurugu hizo kwa kudaiwa kutoa maagizo ya kuapishwa kada kutoka CCM 
katika mtaa wake bila kushinda uchaguzi. Aidha,Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani kata ya Segerea, Japhet 
Kembo, hivi karibuni aliapishwa na wananchi kupitia wakili wa kujitegema
 baada ya uongozi wa manispaa kushindwa kumuapisha kwa wakati, jana 
aliapishwa rasmi na Mwanasheria wa Manispaa hiyo.
Mwingine aliyeapishwa ni Mwenyekiti mteule wa mtaa Minazi mirefu, Ubaya Chuma. Wakati wa zoezi hilo, Mariano Bungala ambaye aligombea mtaa wa 
Kigogo Fresh ‘B’ kata ya Pugu, anakoishi Waziri Mkuu, alipewa kichapo na
 wananchi wakiwamo wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo 
(Chadema) kwa madai kuwa hakushinda kwenye uchaguzi wa serikali za 
mitaa, lakini kwa sababu anatoka mtaa anakoishi Pinda, hivyo ulifanyika 
ujanja ili aapishwe kinyemela.
Vurugu hizo ziliibuka katika ofisi za Manispaa ya Ilala saa saa 
3:30 asubuhi muda mfupi baada ya Bungala kuitwa na maofisa wa manispaa 
ili kuingia ukumbini kuapishwa, lakini alipotaka kuingia tu alidakwa na 
wananchi na kuanza kupewa kichapo. Vurugu hizo zilisababisha watumishi wa Manispaa hiyo kusitisha kwa 
muda kazi hiyo katika ofisi zao kushudia vurugu hizo ambazo zilizimwa 
baada ya polisi kumuokoa Bungala aliyekuwa akiendelea kupewa kipigo.
Mgombea wa Chadema katika mtaa huo, Patricia Mwamakula, ambaye 
alipambana na Bungala katika uchaguzi huo, alisema wakati wa uchaguzi 
Desemba 14, mwaka jana hakuna mshindi aliyetangazwa baada ya kutokea 
vurugu. Alisema kutotangazwa kwa matokeo hayo kulifuatia wanachama wa CCM 
kuchoma masanduku baada ya kubaini kadri kura zilivyokuwa zinaendelea 
kuhesabiwa ushindi ulikuwa unaelekea kwa mgombea wa upinzani. “Hakuna aliyeshinda kwenye uchaguzi kwenye mtaa wetu, tatizo 
tunakaa mtaa anaoishi Waziri Mkuu ambaye amesema kuwa hawezi akaongozwa 
na mwenyekiti anayetoka chama cha upinzani,” alisema.
Mwanachama mwingine wa Chadema, Mayama Mkwizu, alisema wananchi wa 
mtaa wa Kigogo Fresh “B” hawako tayari kuongozwa na mwenyekiti wa CCM 
ambaye hakushinda kwenye uchaguzi kwa sababu tu ya shinikizo la Waziri 
Mkuu. “Kura zilipigwa vizuri, lakini CCM walichoma masanduku kabla ya 
matokeo kutangazwa, kutaka kuapishwa Bungala, ni shinikizo la Waziri 
Mkuu, kama wanataka kusema alishinda wa CCM walete majivu hapa 
yaliyotokana na kuchomwa kwa masanduku ya kura au kama Pinda anaona 
chama chake kimeshinda aje yeye aapishwe,” alisema.
Hata hivyo, Bungala akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa 
chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wamemzunguka huku mkono wa 
shati lake ukiwa umechanwa na kuondolewa kabisa, alisema ana uhakika 
alishinda uchaguzi huo.
KAULI YA BUNGALA
“Nilishinda kwa kupata kura 233 na matokeo yalitangazwa na Afisa 
Mtendaji Kata ya Pugu ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi na ndiye 
aliyeniambie nije niapishwe,” alisema Bungala huku akichechemea kutoka 
na kipigo alichokipata. Bungala alisema tukio lililompata la kupigwa na ataliwasilisha kwa 
viongozi wake wa chama na kwamba waliomfanyia vurugu hizo ni wahuni 
ambao wanataka kuendesha siasa za vurugu. Alipoulizwa kama kuna shinikizo kutoka kwa Waziri Mkuu na kuamua 
kuja kuapishwa wakati anafahamu kuna utata katika matokeo kwenye mtaa 
wake, alisema hizo taarifa ni za uongo. 
MWANASHERIA WA MANISPAA ANENA
Naye Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu, 
alisema licha ya mwenyekiti wa mtaa Kigogo Fresh “B’ kupigwa na 
kusababisha asiapishwe, lakini manispaa itahakikisha inafanya kila 
liwezekanalo aapishwea kwa sababu ndiye mshindi halali katika uchaguzi 
huo. “Anayetambuliwa na Manispaa kuwa ndiye mshindi ni Mariano Bungala 
na kama kuna mtu hajaridhika anaruhusiwa kwenda mahakamani kudai haki,” 
alisema.
Nao wananchi na wafuasi wa Chadema walitoa thadhari kwamba kama 
viongozi wa Manispaa watamuapisha mgombea wa CCM na wao watamuapisha  wa
 Chadema ili mtaa huo uwe na wenyeviti wawili kutoka vyama tofauti. Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh  ‘B’ kata
 ya Pugu ambayo NIPASHE ilionyeshwa na  maofisa wa Manispaa ya Ilala 
yanaonyesha kuwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM alipata kura 134, 
Chadema 127, CUF 17 na mgombea wa NCCR-Mageuzi alipata kura tisa.
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, 
alipoulizwa kuhusu madai dhidi ya Waziri Mkuu, hakutaka kueleza zaidi ya
 kusema kuwa ofisi ya Tamisemi ndiyo inayosimamia masuala ya uchaguzi wa
 serikali za mitaa hivyo ndiyo inayoweza kutoa jibu kuhusu utata wa 
matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’. “Uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na Tamisemi, wasiliana 
na Katibu Mkuu wa Tamisemi au Waziri watakupa majibu, kwanza mimi sipo 
ofisini tangu jana,” alisema Irene.
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alipotafuta simu yake ilikuwa 
ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) 
hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
MGOMBEA CCM  SEGEREA  ALALAMIKA
Wakati huo huo;  aliyekuwa  mgombea wa serikali ya mtaa wa 
Migombani Jimbo la Segerea kupitia CCM, Uyeka Idd, amemtupia lawama 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, kwa kupingana na 
tangazo lake la kuahirisha uchaguzi.
Tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyika 
Desemba 14, mwaka jana  lilitaka uahirishwe kutokana na dosari 
mbalimbali zilizojitokeza katika kituo hicho zikiwamo vurugu. Alisema Desemba 16, tangazo lilitoka kwa Mkurugenzi kuwa uchaguzi 
uairishwe, lakini jana walishangazwa na kitendo cha kuapishwa kwa 
mgombea wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo.
“Tangazo lilisema marudio ya uchaguzi ni Desemba 21, uchaguzi 
ulifanyika, lakini ulifanyika ndani ya dosari za awali na kukwamisha 
baadhi ya wananchi kupiga kura, ” alisema Idd alipozungumza na waandishi
 wa habari.
Januari 20, mwaka huu, wananchi walimwapisha Japhet Kembo wa 
Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo  baada ya ukimya wa serikali 
kitomwapisha. Aliongeza kuwa madai ya shinikizo toka kwa wananchi kuapishwa kwa 
kiongozi huyo hayana tija kwani cha msingi ni uchaguzi kufanyika na 
ushindi upatikane kwa haki. “Madai ya wananchi kwamba kuna shinikizo la Mbunge wa Segerea,  Dk.
 Makongoro Mahanga, kuhusu ushindi wa CCM katika Mtaa huo sio kweli 
kwani mbunge (Mahanga) anakaa mtaa tofauti na huo,” alisema Idd. 
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Christina Mwakangale na Adela 
Josephat.
CHANZO:
     NIPASHE
    
No comments:
Post a Comment