
Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (Cegodeta)
imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuinusuru nchi kwa kumwajibisha Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na wale wote waliohusika na
kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya
Tegeta Escow kwa kupelekwa mahakamani na kuzirudisha fedha hizo ili
kuondokana na kifungo cha kunyimwa misaada na wafadhili.
Aidha, Cegodeta imesema kiporo ambacho Rais Kikwete alimuweka Prof.
Muhongo kimechukua muda mrefu, hivyo wananchi wanatarajia kuona waziri
huyo akifukuzwa kazi. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Cegodeta, Thomas Ngawaiya, na kufafanua kuwa sheria inasema
kuwa kwa yeyote aliyetoa rushwa na aliyepokea wote wana kesi ya kujibu
kwani ni kinyume cha sheria.
Ngawaiya alisema wote waliotajwa kuhusika na uchotwaji wa fedha
hizo wanapaswa kushitakiwa na kuzirudisha kwani wafadhili wanataka
kuliona hilo na sio kujiuzulu pekee. “Prof. Muhongo anapaswa kujiuzulu kwani taratibu za uongozi bora
anazijua, hivyo sioni sababu ya yeye kung’ang’ania wizarani kwani uchafu
wote huu umetokea katika ofisi yake,” alisema Ngawaiya.
Ngawaiya alisema Serikali inapaswa kufahamu kuwa wananchi
hawataelewa kuona wale wote waliotanjwa hawajiuzulu bila kufikishwa
mahakamani. “Hivi sasa kuna miradi mbalimbali inaweza kuwa imekwama kutokana
na kusitishwa misaada na wafadhili, mishahara itakwama na hata
maendeleo yatasimama hivyo kutengeneza bomu katika suala la ajira,”
alisema.
Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa Mbuge wa Moshi Vijijini na Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro,
alisema hivi sasa wananchi wamejenga chuki dhidi ya CCM kutokana na
kashfa hii ya ya Escrow, hivyo Serikali inabidi kuirudisha imani kwa
kuwawajibisha waliohusika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment