
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini, Victor Mwambalaswa, anaonekana kung’ang’ania nafasi hiyo huku
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
William Ngeleja, akisema anaheshimu kauli ya Spika wa Bunge, Anna
Makinda, kwamba wenyeviti wa kamati za bunge ambao walihusika katika
kashfa ya Tegeta Escrow, wameshajiuzulu.
Juzi Makinda alisema kwamba anachojua wenyeviti hao wameshajiuzulu
kufuatia azimio namba nane la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka
uliopita la kuwataka kufanya hivyo. Jana NIPASHE lilishindwa kumpata Mwambalaswa wakati wa mapumziko ya
kikao cha Kamati baada ya kuelezwa kwua alikuwa anajiandaa kuendelea na
kikao.
“Mwambalaswa yupo…kwa sasa hivi huwezi kumuona kwa sababu anaongoza kikao,” alisema mmoja wa wabunge wa kamati hiyo na kuongeza: “Asubuhi Mwambalaswa aliongoza kikao kwa sababu makamu mwenyekiti
alikuwa hayupo...lakini sasa ameshafika ataendelea kuongoza kikao,”
alisema ofisa huyo.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Mwambalaswa alishajiuzulu muda mrefu hata
kabla ya kutolewa kwa kauli ya Spika Makinda na kwamba aliyekuwa
anaongoza vikao vya kamati hiyo ni makamu mwenyekiti wake ambaye ndiye
mwenye taarifa zote za vikao. Hata hivyo alisema hadi wakati huo walikuwa hawajapokea taarifa
kamili ya maandishi kutoka kwa Spika na kuwa huo ndiyo utaratibu.
Pamoja na Mwambalaswa, wenyeviti wengine waliotakiwa kujiuzulu ni
Mwenyekiti wa Kamati ya za Bajeti, Andrew Chenge na Katiba, Sheria na
Utawala, Ngeleja. Hata hivyo, Ngeleja alipoulizwa jana, alijibu kwa kifupi kuwa kauli
ya iliyotolewa na Spika Makinda ni sahihi bila kutaka kufafanua kama
atajiuzulu ama la.
Alitoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC),
jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, akizungumza na
waandishi wa habari, alisema, kikao cha jana cha kamati hiyo kiliongozwa
na mjumbe, Nyambari Nyangwine kutokana na Ngeleja na Makamu wake,
Gosbert Blandes kutokuwapo. Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk. Festus
Limbu, alisema, mwenyekiti wake Chenge, hajajiuzulu hajajiuzulu ingawa
kamati ilikuwa imemweka pembeni asiongoze vikao kwani alikuwa anasubiri
taarifa kutoka kwa Spika.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment